1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfumo wa uchaguzi wa Ujerumani

22 Septemba 2013

Wagombea wa ukansela ndio wanaosikikana kwenye kampeni, bali si wao wanaochaguliwa moja kwa moja katika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani ambapo kipaumbele hasa ni vyama vya kisiasa.

https://p.dw.com/p/19WKe
Mgombea wa chama cha upinzani SPD - Peer Steinbrück na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wa CDU
Mgombea wa chama cha upinzani SPD - Peer Steinbrück na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wa CDUPicha: picture-alliance/dpa

"Kama si mwanachama, basi huna nafasi ya kuingia bungeni na huwezi kamwe kuwa miongoni mwa wabunge takriban 600." Hivyo ndivyo msimamizi mmoja wa kike anayewashughulikia wageni alivyokuwa akimueleza msichana mmoja aliyekwenda kulitembelea bunge hilo hivi karibuni.

Msichana huyo alitaka kujua mtu anaweza vipi kuwa mbunge ili kuamua kuhusu mustakbali wa kisiasa wa raia. Katika sheria ya msingi imetajwa kama ifuatavyo: "Vyama vya kisiasa vinachangia katika kupatikana ridhaa".

Lakini kwa sasa wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wanakiri vyama vya kisiasa sio tu vinachangia bali zaidi kuliko yote vinaamua hasa nani anaweza kuwa mwanasiasa.

Unahitaji ridhaa kubwa, unapokuwa mgombea huru kuweza kuingia bungeni bila ya kuegemea nguzo ya chama cha kisiasa. Hali hiyo inatokana na mfumo wa Kijerumani wa kupiga kura unaofungamanisha kura ya kwanza na kura ya pili.

Mfumo ulivyo

Mpigakura kwenye uchaguzi mkuu wa 2009 nchini Ujerumani.
Mpigakura kwenye uchaguzi mkuu wa 2009 nchini Ujerumani.Picha: John Macdougall/AFP/Getty Images

Tuanzie mwanzo. Wanaoruhusiwa kupiga kura ni wanawake na wanaume wenye uraia wa Ujerumani na ambao wana umri wa miaka 18 au zaidi. Kwa sasa idadi yao inafikia milioni 61 na laki nane, miongoni mwao wanakutikana watu takribani milioni tatu ambao hii ni mara yao ya kwanza kupiga kura. Takwimu hizi zimekusanywa na Idara kuu ya Takwimu ambayo kiongozi wake ndiye anayeandaa pia uchaguzi mkuu.

Na ni kwa kiongozi huyo huyo anaeandaa uchaguzi mkuu ambako vyama vya kisiasa hutuma maombi yao vinapotaka kugombea viti vya bunge. Ikiwa vyama hivyo vya kisiasa vinaheshimu na kufuata katiba, demokrasia na misingi ya taifa linalofuata sheria, basi havikabiliwi na kitisho cha kukataliwa maombi ya kupigania viti vya bunge. Hata kama baadhi ya malengo yao yanaonekana kana kwamba ni ya kutatanisha. Septemba 22, 2013 kwa hivyo vyama 34 vya kisiasa vitapigania viti vya bunge.

Kanuni zinazotumika tangu miaka 60 iliyopita bado ni imara

Kijuu juu mbali na vyama vikuu, hata vyama kadhaa vidogo vidogo vinaweza kuwakilishwa bungeni. Lakini kwa kuwa katika mfumo wa demokrasia, sheria hupitishwa kwa kura za walio wengi,vyama hivyo vidogo vidogo kila mara hulazimika kusaka washirika.

Namna mpiga kura wa Ujerumani anavyopiga kura yake.
Namna mpiga kura wa Ujerumani anavyopiga kura yake.Picha: Fotolia/MaxWo

Waasisi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani walikuwa wakihofia zisizuke vurugu na kusababisha madhara kama ilivyowahi kutokea katika miaka ya 20. Walitaka kuhakikisha kupitia uchaguzi kunachaguliwa bunge litakalopelekea kuundwa serikali imara itakayosalia madarakani miaka minne.

Hiyo ndio maana ikaamuliwa chama kiwakilishwe bungeni kikifanikiwa kukiuka "kiunzi cha asili mia 5 ya kura."

Zaidi ya hayo walitaka pawepo mchanganyiko kati ya wingi na wezani wa kura. Haikutakiwa pawepo vyama vya kisiasa vinavyojichaguliwa wenyewe wagombea wao. Wananchi pia wamepewa fursa ya kuwachagua moja kwa moja wanasiasa. Wazo hapo ni kwamba imedhihirika wanapochaguliwa watu wanaotokea katika eneo wanakoishi wapiga kura, basi wanasiasa hao huwajibika zaidi kwa masilahi ya wananchi.

Hali hiyo inawafanya wananchi wajione wanachangia zaidi katika siasa. Nchini Ujerumani kuna majimbo 299 ya uchaguzi ambako wawakilishi wa vyama hupigania moja kwa moja kiti. Kwa namna hiyo cheti cha kupiga kura kina sehemu mbili -sehemu ya kura ya kwanza na sehemu ya kura ya pili. Utaratibu huo wa kupiga kura haujafanyiwa marekebisho makubwa tangu ulipoanzishwa miaka 60 iliyopita.

Cheti cha kupiga kura cha sauti mbili

Kila mpiga kura wa Ujerumani ana sauti mbili. Sauti ya kwanza anamchagua mwanasiasa wa kutoka chama anachokitaka na ambaye anahisi anawakilisha vyema masilahi ya eneo lake bungeni.

Alama ya chama cha Die Linke cha Ujerumani.
Alama ya chama cha Die Linke cha Ujerumani.Picha: Getty Images

Hapo anahusika mtu maalum. Mtu huyo sio lazma awe anatoka katika kile chama ambacho mpiga kura anakipa sauti yake ya pili. Sauti ya pili kimsingi ndio muhimu zaidi. Kwa sababu sauti hiyo ya pili ndio inayoamua hatima ya chama fulani.

Chama kinapojipatia sauti nyingi zaidi ndipo kinapowakilishwa kwa nguvu zaidi bungeni na hivyo kuweza kutuma wawakilishi wengi zaidi bungeni. Hapo wapiga kura ndio wanapoamua kuhusu wezani kati ya vyama vya kisiasa. Vile vyama ambavyo vimeshindwa kukiuka kiunzi cha asili mia tano ya kura havina nafasi ya kuwakilishwa bungeni.

Matukio ya kura ya kwanza na ya pili hupelekea-yanapogawiwa nusu bin nusu, kupatikana idadi jumla ya wabunge wanaowakilisahwa katika Bunge la Shirikisho - Bundestag.

Mwandishi: Dick Wolfgang
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Mohammed Khelef