1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiEthiopia

Mfumuko wa bei ´wakamua mifuko´ ya familia Ethiopia

5 Aprili 2023

Mfumuko wa bei nchini Ethiopia unazifanya familia nchini humo kila wakati kuangalia namna ya kupanga upya bajeti zao za kila mwezi.

https://p.dw.com/p/4PjOb
Ethiopia | Soko la vyakula kwenye mji wa Bahir Dar
Bei za vyakula imepindukia bei za kawaida nchini EthiopiaPicha: Alemenew Mekonnen/DW

Bei za vyakula na bidhaa mbalimbali zilizopanda kwa kiasi kikubwa kutokana na changamoto kuanzia janga la UVIKO-19 hadi vita vya miaka miwili katika jimbo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, zinaendelea kuwatia wasiwasi wengi wanaohofia mustakabali wa maisha yao. 

Kama ilivyo kwa wazazi wengi nchini Ethiopia, Samson Berhane anaonekana akitazama bila ya kuamini bei za maziwa ya watoto na bidhaa nyingine za watoto zinazopanda kwa kasi kutokana na mfumuko mkubwa wa bei nchini humo.

Anasema "Kila kitu ninachonunua kimepanda bei.. bei ya maziwa ya unga ya watoto imeongezeka kwa dola kama 5 hivi." Samson mwenye binti wa miezi tisa alikuwa akizungumza na shirika la habari la Reuters.

Mfumuko wa bei kwa mwaka umepindukia asilimia 30 nchini Ethiopia, hii ikiwa ni kulingana na takwimu rasmi zilizozingatia taarifa ya kiuchumi iliyoachpishwa na taasisi ya Trading Economics, na kuyajumuisha mataifa ya Afrika ambayo gharama za maisha zinaongezeka kwa kasi, kuanzia Ghana hadi Zimbabwe.

Ingawa kasi ya mfumuko huo wa bei nchini Ethiopia inapungua katika miezi ya hivi karibuni, bado umeshuhudiwa kuwa juu mno katika miaka ya karibuni.

Hali hiyo imechochewa na ukame, changamoto zilizotokana na janga la UVIKO-19 na miaka miwili ya mzozo katika jimbo la Tigray, kaskazini mwa taifa hilo, uliomalizika mwezi Novemba mwaka uliopita.

Familia sharti zipangilie upya bajeti walau kila mwezi

Upungufu wa "teff" ambayo ni aina ya nafaka inayotumiwa kwa kiasi kikubwa katika vyakula nchini humo umechangia kupanda kwa bei katika miezi ya karibuni, na kusababisha wakazi kupanga upya bajeti zao za vyakula na hasa wale wenye kipato cha chini.

Samson anasema uamuzi wa serikali wa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani katika bidhaa za msingi iliouchukua mwezi Septemba mwaka 2021, ikiwa ni miongoni mwa mfululizo wa hatua zilizolenga kupambana na athari za mfumuko wa bei, kwa kiasi kikubwa imeleta afueni japo kidogo sana.

Nafuu ni kwa familia zenye kipato kidogo na hasa kwa kuwa taifa hilo la pili kwa wingi wa watu barani Afrika kwa muda mrefu limeshuhudia uhaba wa fedha za kigeni, huku wengi wakiyageukia masoko yasiyo rasmi badala ya viwango rasmi vilivyoorodheshwa kwenye mabenki hali inayochochea changamoto iliyopo.

Baada ya kipindi cha zaidi ya muongo mmoja wa ukuaji mzuri, uchumi wa Ethiopia umeendelea kukua taratibu katika kipidi cha karibuni.

Uchumi ulitarajiwa kukua kwa angalau asilimia 7.5 mwaka 2023, tofauti na matarajio ya asilimia 6.3 ya mwaka uliopita, alisema Waziri Mkuu Abiy Ahmed mwezi Novemba.

Daniel anayeishi katika mji mkuu, Addis Ababa na watoto wake watatu amesema kupungua kwa kasi ya ukuaji, kumeathiri pia biashara yake ya duka la vifaa vya magari na kuifanya familia yake kupunguza matumizi.

Amesema ameacha kabisa kuwapeleka watoto wake kwenye maeneo ya kustarehe na kuongeza kwamba hata nyama hivi sasa hailiki nyumbani kwake, na badala yake wanakula mboga za majani na kunde.

Kitoweo mfano wa nyama imegeuka anasa nchini Ethiopia

Na tangu Mimi Tadesse mama mwenye watoto wawili alipoondolewa kazini alipokuwa muhasibu karibu miezi minne iliyopita, yeye pia kaacha kabisa kununua nyama, kula nje na hata kuwanunulia nguo mabinti zake.

Anasema kila mwisho wa mwezi wao hukutana tu na taarifa za kuongezeka kwa bei za nauli za usafiri wa umma, kutokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta na chakula kikuu kwa sasa ni Injera, ambacho ni maarufu sana nchini humo.

Anasema, hata bora kwake, kwa sababu anazijua familia nyingi zinazokula mara moja kwa siku.

Na huko Tigray, mtumishi mmoja wa serikali Fisseha Hagos amesema anahofia afya ya watoto wake wawili ambao hawakupata mlo kamili wakati ya vita vya miaka miwili kwenye jimbo hilo vilivyosababisha kupanda kwa bei za vyakula. Amesema wanahofia pia mustakabali wa ukuaji wa watoto wao.

Lakini Daniel, kama mfanyabiashara mdogo anaona kitu pekee kitakachosaidia ni kwa serikali kuwapiga marufuku wamiliki wa nyumba kuongeza kodi.