1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadhi ya mwanadamu haina mjadala

11 Februari 2016

Jumuiya kuu ya wafanyakazi nchini Ujerumani,DGB inawataka watu washikamane katika kuwasaidia wakimbizi na kupinga ubaguzi unaofanywa dhidi ya wakimbizi hao nchini Ujerumani na barani Ulaya kote

https://p.dw.com/p/1Htrb
Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya wafanyakazi nchini Ujerumani,Reiner Hoffmann
Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya wafanyakazi nchini Ujerumani,Reiner HoffmannPicha: picture-alliance/dpa

Changamoto kubwa na ambazo siyo za kawaida zinaikabili, Ujerumani wakimbizi na wahamiaji.

Na kutokana na hali hiyo, makanisa,jumuiya za waislamu,wayahudi, jumuiya za wafanyakazi na za waajiri zimeunda mfungamano wa "dunia wazi" ili kuzikabili changamoto hizo. Reiner Hoffmann ambae ni Mwenyekiti wa jumuiya kuu ya wafanyakazi nchini Ujerumani DGB ametoa mwito wa mshikamano.

Kwa kuutoa mwito huo jumuiya kuu ya wafanyakazi ya Ujerumani inatoa ishara ya wazi na muhimu sana. Ni kweli kwamba changamoto ni kubwa. Lakini upo uhakika kwamba, kwa pamoja itawezekana kuzimudu changamoto hizo.

Juhudi kubwa zitahitajika kutoka pande zote, pia kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji wenyewe. Yatakayofanyika lazima yafuate masharti na taratibu, kama jinsi inavyofafanuliwa katika mwito.

Hakuna kitakachofanikishwa bila ya uekezaji, elimu, miundo mbinu na watendaji. Jumuiya kuu ya wafanyakazi ya nchini Ujerumani ina msimamo thabiti wa kisiasa dhidi ya wale wanaoeneza chuki na ubaguzi.

Inapasa kuukomesha mwenendo uliojitokeza katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya ambako mwelekeo wa siasa za mrengo mkali zimechochea mashambulio zaidi ya 900 kwenye makaazi ya wakimbizi.Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulio hayo, hata moja tu siyo haki.

Moyo wa ukarimu unahitajika

Inapasa kuwatilia maanani wote waliojizatiti na kushikamana na kuwapokea wakimbizi nchini Ujerumani na katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.Pongezi kwa maalfu ya watu wanaowasaidia wakimbizi,miongoni mwao polisi,mashuleni ,makazini , viwandani na katika sehemu nyingine za jamii.

Wakimbizi mjini Berlin
Wakimbizi mjini BerlinPicha: DW/B. Gräßler

Kwa mwito huu jumuiya kuu ya wafanyakazi ya Ujerumani inadhamiria kujenga mshikamano dhidi ya wale wenye itikadi kali wanaowapinga wakimbizi. Inapasa kuwakabili watu hao mitaani, makazini na kwenye mtandao.

Mfungamano huu wa "dunia wazi" umeanzishwa kwa sababu, ni katika sehemu za kijamii, ambako mchakato wa utangamano unafanyika- ofisini, madukani,viwandani na kwenye sehemu zingine za kazi. Ni kwenye sehmu hizo ambako watu wenye nasaba mbalimbali wanakutana. Watu wanaokutana kila siku na kufanya kazi kwa pamoja ,wanajuana na kutangamana vizuri. Hakuna anaemwona mwenzake kuwa ni mgeni.

Wanachama wa jumuiya ya wafanyakazi, pamoja na viongozi pia watajizatiti katika juhudi za kuwaingiza wakimbizi na wahiamiaji katika jamii. Washirika wetu katika mfungamano huu watajiwekea malengo yao juu ya kuutekeleza mwito wetu. Hata hivyo tutushirikiana katika kuijenga misingi ya pamoja.

Washirika 10 katika mfungamano wa "dunia wazi " watahakikisha kwamba, mfungano huu unajengeka na kuwa wazi kwa wote na siyo kwa watu fulani tu. Na kwa ajili hiyo, katika wiki zijazo tutajaribu kuyajumuisha mashirika, asasi na watu mashuhuri ili wajiunge na harakati za kusimama pamoja na wakimbizi.

Mwandishi: Hoffmann Reiner

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri: Abdul-Rahman.