1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatishia kufunga njia inayotumiwa kusafirisha mafuta

9 Mei 2019

Iran inasema inaacha utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake kwenye mkataba wa kusitisha utengezaji silaha za nyuklia. Marekani imetuma meli za kivita kwenye eneo hilo. Je, tunaelekea kwenye vita vya tatu vya Ghuba?

https://p.dw.com/p/3IETw
Iran | Präsident Hassan Rohani
Picha: picture-alliance/abaca/Parspix

Mwezi uliopita, Marekani iliweka vikwazo vikali zaidi kwa kufungia mafuta ya Iran kununuliwa na taifa lolote, matokeo yake ni Iran kupata ugumu wa kuuza mafuta kama ilivyokuwa kabla ya vikwazo. Marekani ilianza kwa kuliorodhesha miongoni mwa makundi ya kigaidi Jeshi la Mapinduzi la Iran, IRGC. Ni kutokana na matukio haya mawili, ambapo rais wa Iran Hassan Rouhani na mkuu wa jeshi la IRGC wametishia kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz, unaoiunganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman.

Swali ni je kufunga njia hii kunamaanisha nini? Maana yake ni kwamba Mlango Bahari wa Hormuz ndio njia kuu inayopita asilimia 30 ya meli za mafuta ghafi za ulimwengu mzima, kwa hivyo ulimwengu mzima utaathirika lau utafungwa. Upana wa njia hii ni kilomita 40 ambapo meli mbili kubwa za mafuta zinaweza kupita, kwa hivyo kuifunga ni jambo rahisi kwa kutumia mabomu machache tu ya chini ya maji.

Kuna uwezakno Marekani ikaongeza idadi ya uwepo wa majeshi yake katika Ghuba ya Uajemi. Kikosi cha Wanamaji kimepelekwa katika eneo hilo pamoja na mabomu aina ya B-52. Lengo ni Marekani kuweza kuchukua hatua za mara moja iwapo Iran itaamua kushambulia.

Iran 2010 Bau Atomkraftwerk in Bushehr
Wafanyakazi wakishughulika katika kiwanda cha Nyuklia nchini IranPicha: Getty Images/IIPA

Lakini Iran inayo njia nyangine kando na hiyo ambapo ni kutaka baadhi ya sehemu za mkataba huo kufutwa ili kuiruhusu kuwa na madini zaidi ya uranium na hivyo uwezo wa kuwa na nyuklia. Mkataba huo wa mwaka 2015 unafahamika kama Mpango Mkakati wa Maelewano ya Pamoja yaani JCPOA, ambao licha ya Marekani kujitoa, Iran na mataifa mengine ya Ulaya wamejitolea kuutekeleza.

Sasa je, kuna vita? Kwa sasa hakuna vita, madamu Iran haitafanya jambo lolote hatari pasi kujali madhara yake. Marekani inapanga kuanzisha mashambulizi makubwa baada ya silaha na vikosi vyake kuwa tayari ila kiuhakika wanaweza kuchukua uamuzi wa haraka iwapo Iran itaamua kuufunga Mlango Bahari wa  Hormuz ama kuvishambulia vikosi vya jeshi la Marekani katika kanda hiyo.

Marekani katikati ya mataifa ya Shia na Sunni

Wakati huo huo, Marekani haina nia ya kuanzisha vita vyengine kwa kuzingatia kampeni za Rais Donald Trumph alipoahidi kwamba hatokuwa mwepesi wa kuanzisha vita kama walivyokuwa watangulizi wake. Kwa hivyo, licha ya vitisho kuendelea pande zote mbili hakuna uwezekano wa vita vya tatu vya Ghuba.

Iran 2010 Bau Atomkraftwerk in Bushehr
Kiwanda cha nyuklia cha Bushehr, kusini mwa IranPicha: Getty Images/IIPA

Mashirika ya kijasusi ya Marekani, ambayo mara nyingi taarifa zake haziwi sahihi, yanaripoti kwamba Iran inapanga kuvishambilia vikosi vya jeshi la Marekani vilivyoko Syria na Iraq. Vile vile, kulingana na kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, Iran imepeleka maroketi ya masafa mafupi Iraq kupitia meli za kibiashara ikiwanukuu viongozi wa daraja la juu wa Iran.

Inachokitaka Marekani kutoka kwa marafiki zake wa kikanda ni kuaminiwa na ulinzi ambapo hili linadhihirika na ziara ya kushtukizia nchini Iraq ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Mike Pomeo. Iraq, sawa na Iran, ni mataifa yaliyo na Mashia wengi na ni mataifa yaliyo na uhusiano wa karibu, lakini Iraq haina budi kupiga goti kwa Marekani ambayo ndio imewezesha kuwa na serikali. Kiupande mwengine Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu ambayo ni Sunni ni marafiki na Marekani ila wana uhasama na Iran.

(DW)