1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wafukuta mataifa ya Ghuba

Iddi Ssessanga
25 Mei 2017

Qatar imeingia katika mzozo na baadhi ya mataifa washirika katika kanda ya Ghuba, kuhusiana na kile ilichosema yalikuwa matamshi ya uzushi aliosingiziwa mfalme wake akikosoa sera ya kigeni ya Marekani.

https://p.dw.com/p/2dZi6
Golf Gipfel Saudi Arabien König Abdul Aziz
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani akihudhuria mkutano wa kilele kati ya rais wa Marekani na viongozi wa mataifa ya Kiislamu mjini Riyadh, Saudi Arabia.Picha: picture alliance/Saudi Royal Council

Kadhia hiyo imeonyesha  mchanganyiko usiodhahiri miongoni mwa mataifa washirika ya Ghuba, siku chache baada ya rais Donald Trump kuzuru mjini Riyadh na inaashiria uwezekano wa kufufuka kwa mzozo wa mwaka 2014 kati ya Qatar na majirani zake kuhusiana na madai kuwa nchi hiyo inawaunga mkono wanasiasa wa nadharia za Kiislamu.

Qatar na washirika wake wa Ghuba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu wametumia hifadhi zao kubwa za mafuta na gesi kushawishi matukio katika mataifa mengine ya Kiarabu, na mgogoro kati yao unaweza kubadilisha urari wa kisiasa nchini Libya, Misri, Syria, Iraq na Yemen.

Shirika rasmi la habari la Qatar liliripoti siku ya Jumanne kuwa Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, akiwa katika mahafali ya kijeshi alikosoa  mzozo mpya na Iran, na kuzungumzia juu ya kuyaelewa makundi ya Hezbollah na Hamas,akisema  kwamba hadhani rais Donald Trump atadumu muda mrefu madarakani.

Riad  Donald Trump Saudi Arabien
Trump akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mataifa ya Ghuba mjini Riyadh.Picha: Getty Images/M.Ngan

Doha ilikanusha vikali kwamba matamshi hayo yaliwahi kutolewa, lakini mataifa ya Ghuba yakiwemo mzalishaji nambari wa mafuta duniani Saudi Arabia yaliruhusu vyombo vya habari vya serikali kuyatangaza kwa siku nzima siku ya Jumatano huku vikinukuu shirika la habari la Qatar. Msemaji wa serikali alisema Amir hakutoa matamshi hayo wakati mahafali ya Waqatari waliohitimu mafunzo ya kijeshi.

Kampeni ya uhasama dhidi ya Qatar

Waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo Sheikh Mohammed al-Thani akasema Alhamisi kuwa Qatar imelengwa na kampeni ya uhasama, hususani katika vyombo vya habari vya nchini Marekani, na kueleza kwamba inashangaza kuwa katika muda wa wiki tano zilizopita, kulikuwepo na makala 13 za maoni zikijikita juu ya Qatar katika vvyombo vya habari vya Marekani, na kwamba siku ambapo shirika la habari la Qatar QNA lilipodukuliwa, mkutano kuhus Qatar uliitishwa bila wao kuhudhuria wakati waandishi wa makala hizo walikuwepo.

Alisema udukuzi huo ulifanyika jioni sawa ulipofanyika mkutano kuhusu Qatar. Udukuzi huo uliodumu kwa saa nne baada ya saa sita za usiku siku ya Jumanne, ulisababisha malalamiko katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati kutokana na maudhui ya hadith hizo, yakiwemo matamshi kuhusu mzozo na utawala wa Marekani, mgogoro kati ya Israel na Wapalestina na uhusiano na Iran.

Mamlaka nchini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zikaifungia tovuti kuu la televisheni ya Qatar ya Aljazeera, ambayo Riyadh na Abu Dhabi zimekuwa zikiiona mara nyingi kama inayozikosoa serikali zao. Aljazeeza inasema yenyewe ni kituo huru kinachotoa sauti kwa kila mmoja katika kanda hiyo.

Symbolbild - Al-Dschasira
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimefungia tovuti ya Aljazeera ambayo zinaiona kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali zake.Picha: picture-alliance/dpa/M. Ulmer

Kitisho kwa ushirika wa Ghuba

Mataifa hayo yote yalikataa madai ya Qatar kuhusu udukuzi. Kituo cha Al Arabiya cha Saudi kilitangaza ripoti yenye kichwa cha "ushahidi kuwa shirika la habari la Qatar halikudukuliwa," iliobainisha kwamba taarifa hiyo ilirushwa pia na televisheni ya taifa ya Qatar na kwenye kaunti ya Instagram ya shirika la QNA.

Mzozo huo ni mugumu hasa kwa mataifa hayo ya Ghuba ya Kiarabu baada ya viongozi wake kukutana na Trump mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kilele wa mataifa ya Kiislamu mjini Riyadh, uliolenga kuonyesha mshikamano dhidi ya makundi ya kisunni ya itikadi kali na hasimu wao wa Kishia katika kanda hiyo Iran.

Uhusiano kati ya Qatar na mataifa mengine ya Ghuba ulizorota kwa miezi nane mwaka 2014, kuhusiana na madai ya Qatar kuliunga mkono kundi la Udugu wa Kiislamu, ambalo itikadi yake ya kisiasa inapinga kanunu za utawala wa Kifalme.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, afpe

Mhariri: Saumu Yusuf