1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgonjwa wa Corona Ujerumani yuko mahututi

Grace Kabogo
26 Februari 2020

Maafisa kwenye eneo la magharibi mwa Ujerumani wamesema mwanaume ambaye ameambukizwa virusi vya Corona yuko katika hali mbaya na amehamishiwa kwenye hospitali maalum ya mjini Duesseldorf.

https://p.dw.com/p/3YRvY
Deutschland Uniklinik Düsseldorf | Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gamabrini

Wizara ya afya katika jimbo la North Rhine-Westphalia imesema leo kuwa mwanaume huyo alilazwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu akiwa anaumwa homa ya mapafu kwenye hospitali moja ya mji wa Erkelenz mji ulio karibu na mpaka na Uholanzi. Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 47 aligundulika kuwa na virusi vya Corona na aliwekwa katika karantini kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi, kabla ya kuhamishiwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Duesseldorf.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mke wa mgonjwa huyo pia anatibiwa kama mgonjwa mwenye dalili ya virusi vya Corona na kwamba afya yake imetengamaa. Hata hivyo, vipimo kuhusu afya yake kubaini iwapo ameambukizwa virusi hivyo ama la, bado vinachunguzwa.

Mgonjwa kwenye jimbo la Baden-Württenmberg

Maafisa wa Ujerumani wamesema mwanaume mwingine kwenye jimbo la Baden-Württenmberg pia ameambukizwa virusi vya Corona na kuifanya idadi ya watu walioathirika virusi hivyo nchini Ujerumani kufikia 18, baada ya wiki mbili kutokuripotiwa kisa chochote.

Stephan Pusch, mkuu wa wilaya ya Heinsberg katika jimbo la North Rhine-Westphalia ambako mgonjwa huyo aligundulika amesema usafiri wa umma hautaathirika, ingawa shule pamoja na chekechea katika wilaya hiyo zitaendelea kufungwa. Pusch amewasihi wananchi ambao wanahisi dalili za kuumwa kubakia majumbani na kuwasiliana na madaktari kwa njia ya simu.

Aidha, Ufaransa imetangaza kifo cha kwanza cha raia wa nchi hiyo kutokana na virusi vya Corona.

Italien: Menschen mit Anti-Coronavirus-Masken in Rom
Baadhi ya wananchi wa Italia wakiwa wamefunika nyuso zao kujikinga na virusi vya CoronaPicha: picture-alliance/M. Nardone

Wakati huo huo, idadi ya watu waliokufa kwa virusi vya Corona nchini China ambako virusi hivyo vimeanzia, ni zaidi ya 2,700. Shirika la Afya Duniani, WHO limesema zaidi ya watu 80,000 wameambukizwa virusi hivyo duniani. WHO imesema kipindi ambacho mtu anaambukizwa virusi vya Corona hadi muda dalili zinapojitokeza kinachukua hadi siku 14.

Visa vyaongezeka Italia

Italia imeripoti kuongezeka kwa visa vipya vya virusi vya Corona, ambapo watu 322 wameambukizwa na 11 wamekufa kutokana na virusi hivyo. Waziri wa Afya wa Italia, Roberto Speranza amesema virusi hivyo havitambui mipaka ya kiutawala, majimbo, wala miji na ametoa wito wa kushirikiana kwa sababu hakuna nchi itakayoweza kukabiliana yenyewe na virusi vya Corona.

''Kutokana na hili niliiomba Ulaya kuandaa mkutano wa mawaziri wa afya kutoka kwenye nchi zinazopakana na Italia, mkutano umefanyika tena ndani ya saa chache. Mawaziri hao wametuonesha ushirikiano mkubwa. Ninaamini kwamba suala hili ni zuri na muhimu katika kuushinda ugonjwa huu,'' alifafanua Speranza.

Mataifa sita ya Ulaya yametangaza visa vya virusi vya Corona kwa watu ambao hivi karibuni wamerejea kutoka kaskazini mwa Italia, ambako virusi hivyo vya COVID-19 viliripuka wiki iliyopita. Nchi hizo ni pamoja na Uswisi, Austria na Croatia, ambazo zimetangaza visa hivyo kwa mara ya kwanza pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Uhispania ambazo tayari ziliripoti kuhusu wagonjwa wa Corona.

(AP,DPA, DW https://bit.ly/2w2JAki)