1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 23 ya muungano magazetini

3 Oktoba 2013

Miaka 23 ya muungano wa Ujerumani, na Vuta ni kuvute kati ya wademocrats na warepublicans nchini Marekani ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/19tFc
Rais wa shirikisho Joachim Gauk(kushoto) na mpenzi wake Daniela Schadt,wakihudhuria misa ya muungano pamoja na spika wa bunge Norbert Lammert,kansela Angela Merkel,waziri mkuu wa jimbo la Baden-Württemberg Winfried Kretschmann na mkewe, na rais wa korti kuu ya katiba Andreas Voßkuhle na mkewePicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie na Octoba tatu, siku kuu ya muungano wa Ujerumani. Miaka 23 imekamilika tangu ukuta wa Berlin ulipoporomoka na sehemu mbili za Ujerumani-Jamhuri ya kidemokrasia ya Ujerumani-au GDR na shirikisho la jamhuri ya Ujerumani au Ujerumani magharibi ya zamani zilipoungana. Suala wahariri wengi wa magazeti ya Ujerumani wanalojiuliza ni jee muungano umekamilika? Suala hilo hilo amejiuliza mhariri wa Gazeti la "Märkische Orderzeitung" anaesema:"Kipi kinakosekenana kuufikia muungano wa kweli? Kwanza ni kuleta usawa katika suala la malipo ya uzeeni na mishahara. Hakuna sababu inayohalalisha kuwepo pengo la mishahara miaka 24 baada ya ukuta wa Berlin kuporomoka. Na kuna suala ambalo pia ni muhimu na linalotishia kuwatenganisha kwa muda mrefu zaidi wakaazi wa mashariki na wale wa magharibi:Suala hilo linahusiana na kumiliki mali.Sehemu kubwa ya majumba na makampuni yanamilikiwa na wajerumani magharibi au wageni. Wajerumani mashariki hawakuwa na uwezo wa kununua milki hizo si kabla na wala si baada ya ukuta kuporomoka.La muhimu zaidi lakini ni madhara ya kisaikolojia.

Symbolbild Wiedervereinigung deutsche Einheit Westdeutsche Ostdeutsche Händedruck
Nembo ya muungano.Picha hiyo ya watu wanaopeana mikono inamaanisha" wanakuwa pamoja walio wamoja"Picha: imago/bonn-sequenz

Mustakbal wa Muungano unakutikana majimboni

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung linazungumzia pengo jengine lililoko. Gazeti linaandika:"Bado idadi ya wasiokuwa na kazi ni kubwa sehemu ya mashariki kuliko katika sehemu ya magharibi,lakini wakati huo huo idadi hiyo ni ndogo katika jimbo la mashariki la Thüringen ikilinagnishwa na idadi ya wasiokuwa na kazi katika jimbo la magharibi la Nord Rhine Westphalia.Ndo kusema walioondolewa patupu na muungano wanakutikana huko?Hasha.Shirikisho la neema la jamhuri ya Ujerumani ya zamani haliko tena.Sio kwasababu ya gharama za muungano,bali kutokana na kishindo jumla cha mashindano.Hiyo ndio maana tofauti za kimkoa zinazokutikana katika kila pembe ya Ujerumani ndizo zitakazoamua hali ya siku za mbele na sio tena mgawanyiko kati ya mashariki na magharibi.

Symbolbild USA Haushaltsstreit Schließung
Kitambulisho cha mvutano wa bajeti nchini MarekaniPicha: Reuters

Shughuli za serikali zasita Marekani

Mvutano kati ya wafuasi wa chama cha Republican na wale wa Democrat nchini Marekani umezidi makali kwa namna ambayo baadhi ya shughuli za serikali zimelazimika kufungwa na watumishi kulazimishwa kuchukua likizo bila ya malipo. Gazeti la "Volksstimmen" linaandika:"Kile ambacho miaka ya nyuma kiliweza chupu chupu kuepukwa,kimejiri hivi sasa:Shughuli za serikali ya Marekani zimesita.Rais Barack Obama ambaye kawaida daima huwa tayari kufikia maridhiano,safari hii amevinjari,hataki asilani kuona mpango wake wa kufanyiwa mageuzi sekta ya afya-au "Obamacare" kama unavyoitwa,unameguliwa na warepublican.Anachokipigania Obama hapo sio tuu huduma za afya kwa kila mmarekani,bali pia yeye mwenyewe kuingia katika madaftari ya historia ya Marekani.Nafasi yake lakini katika madaftari ya historia tokea hapo iko kutokana na kuwa rais wa kwanza wa Marekani ambae ni mweusi.Bima ya afya ambayo kabla ya hapo ilimtoa kijasho Bill Clinton ikifanikiwa,basi Barack Obama atajivunia pia sifa ya kuwa mwanamageuzi.Kwa hivyo kusitishwa shughuli za serikali kwa muda usiojulikana,si hasara ikilinganishwa na umuhimu wa mageuzi katika sekta ya afya anahisi rais Obama."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo