1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 30 baadaye, Museveni ataka muhula wa tano

16 Februari 2016

Rais Yoweri Museveni aliwahi kusema kuwa viongozi wanaokaa sana madarakani ndiyo walikuwa chimbuko la matatizo ya Afrika, lakini miaka 30 baadae, Museveni anatazamia kuingia muongo wa nne madarakani nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/1Hw5X
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: picture alliance/Kyodo

"Wale wanaosema, 'aende,' wanahitaji kufahamu kuwa huu siyo wakati sahihi," Museveni alisema wakati wa mmoja ya mikutano yake ya kampeni hivi karibuni kuelekea uchaguzi mkuu wa Februari 18 ambao wengi wanataraji atashinda. "Mzee huyu ameiokoa nchi hii, vipi unamtaka aondoke? Ninaweza kuondoka kwenye shamba la migomba niliopanda na ambayo imeshaanza kuzaa matunda?"

Museveni alifanikiwa kubadilisha katiba mwaka 2005, na kuondoa ukomo wa mihula miwili. Viongozi wengine wa Afrika wamefuata nyayo zake, wakibadili au kurekebisha sheria ili kusalia madarakani, wa karibuni zaidi wakiwa marais wa Burundi Pierre Nkurunziza na wa Rwanda Paul Kagame.

Kwa sasa, Museveni hana nia ya kukabidhishi madaraka kwa mtu yeyote, akipinga ukosoaji wa mataifa wahisani ya magharibi kuhusiana na kukithiri kwa rushwa na hatua za kutoa madaraka makubwa kudhibiti mashirika ya kiraia na yale yasiyo ya kiserikali.

Museveni amektaa miito ya kumtaka aondoke madarakani.
Museveni amektaa miito ya kumtaka aondoke madarakani.Picha: Said Michael

Wakati akiwania kuingia muongo wake wa nne madarakani, Museveni anaednelea kuwa mmoja wa viongozi wajanja na ving'ang'anizi zaidi barani Afrika, sambamba na wengine mifano ya Jose Eduardo dos Santos wa Angola na Teodoro Obiang wa Guinea ya Ikweta (wote wako madarakani tangu 1979), Robert Mugabe wa Zimbabwe (tangu 1989) na Paul Biya wa Cameron (tangu 1982).

Kwa sehemu kubwa, Uganda imekuwa na amani wakati wa utawala wa Museveni. Uasi wa kaskazini, unaoongozwa na kichaa wa miujiza Joseph Kony na kundi lake la Lord's Resistance Army (LRA), ulifurushwa nje ya nchi hiyo muongo mmoja uliyopita na mkono wake imara umezuwia machafuko ya kutumia silaha na ugaidi.

Hali ya uchumi iliboreka na Uganda ilishuhudia ukuaji wa asilimia 7 katika miaka ya 1990 na 2000, ukisukumwa na uwekezaji wa umma katika miundombinu na kufufuka kwa kilimo. Pia aliendesha kampeni yenye ufanisi dhidi ya maradhi ya ukimwi na maambukizi yake.

Lakini ukuaji wa uchumi ulishuka hadi chini ya asilimia 5 mwaka uliyopita, wakati karibu asilimia 20 ya wakaazi milioni 38 wa nchi hiyo bado wanaishi katika hali ya umaskini kulingana na takwimu za benki ya dunia.

Wapigakura pia wanataka wanasiasa washughulikie rushwa, hali mbaya ya hospitali za umma, na viwango vikubwa vya utoro mashuleni. Kuna miito pia ya kubadili uchumi wa taifa hilo unaotegemea zaidi kilimo kuuwezesha kuwaajiri maelfu ya vijana wanaomaliza masomo kila mwaka.

Polisi wakilizingira gari la Besigye kumzuwia aisendelea ka kampeni mjini Kampala.
Polisi wakilizingira gari la Besigye kumzuwia aisendelea ka kampeni mjini Kampala.Picha: Ole Tangen

Wapinzani wakuu wa Museveni

Mpinzani mkuu wa Museveni miongoni mwa wagombea saba wa upinzani ni Kizza Besigye mwenye umri wa miaka 59, daktari wake wa zamani, ambaye pia ni kanali mstaafu wa jeshi na mgombea mara tatu wa nafasi hiyo ya urais.

Besigye ambaye ni kipenzi cha Waganda wengi anatazamwa kama mpinzani anaeaminika zaidi kuliko mshirika wa muda mrefu wa Museveni Amama Mbabazi mwenye umri wa miaka 67, alietimuliwa katika nafasi ya waziri mkuu mwaka 2014 kutokana na malengo yake ya urais.

Mkereketwa huyo wa chama tawala cha National Resitance Movement NRM, anaesimama kama mgombea binafsi - huenda akapunguza kura za wafuasi wa chama hicho, wanasema wachambuzi. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Museveni huenda akapata ushindi wa moja kwa moja.

Lakini ikiwa hakutakuwa na mgombea aatakaepata zaidi ya asilimia 50 ya kura na uchaguzi ukaenda katika duru ya pili, wachache wana mashaka kwamba rais Museveni atashinda.

Mapambano ya vitisho

"Tunachoshughulika nacho siyo uchaguzi," alisema prefesa wa sheria Oloka Onyango kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, na kuongeza kuwa mapambano ya kisiasa yanafanyika kuptia vitisho kuliko kwenye sanduku la kupigia kura.

Wagombea wawili wakuu wa upinzani wamekamatwa kwa muda wakati wa kampeni za uchaguzi, ambao pia umeshuhudia ukandamizaji wa vyombo vya habari. "Wazuwia uhalifu wamekuwa wakiwashambulia wanachama wa upinzani na kuivuruga mkiutano ya upinzani," alisema Patrick Tumwine kutoka shirika la HURINET.

John Patrick Amama Mbabazi, waziri mkuu wa zamani na mgombea wa vuguvugu la "Go Forward."
John Patrick Amama Mbabazi, waziri mkuu wa zamani na mgombea wa vuguvugu la "Go Forward."Picha: DW/E. Lubega

Alilituhumu kundi hilo la wazuwia uhalifu kwa kushirikia katika vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha, mapigano katika mabaa na hata mauaji. Lakini kiongozi wa kundi hilo Blaise Kamugisha anakanusha tuhuma hizo: "Tunatoa tu taarifa kwa polisi na maafisa wa polisi wanaova sare hutupa ushauri wa kiufundi."

Besigye pia ana kikundi chake kinachomlinda, maarufu kama vijana wasio na ajira, wakati Mbabazi anaungwa mkono na vijana maskini. HURINET inaorodhesha makundi kama hayo 11 yanayofungamanishwa na vyama au wanasiasa.

Wanachama wa makundi hayo wakati mwingine hujitokeza kwenye mikutano ya kampeni wakiwa na fimbo na mapanga, kulingana na makundi ya haki za binaadamu, ambayo yanaripoti mashambulizi kadhaa dhidi ya wanasiasa au wafuasi wao kabla ya uchaguzi.

Hatari ya mauaji kutokea baada ya uchaguzi

Chaguzi zilizopita mwaka 2001, 2006 na 2011 zilikumbwa na madai ya wizi wa kura, vurugu, vitisho," lilisema shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch. " Ikiwa maadamano yataibuka baada ya uchaguzi, kuna hatari kubwa kwamba wandamanaji, na hata wapintanjia.Watakufa mikononi mwa vyombo vya usalama," limeonya shirika hilo la haki za binaadamu.

Mhadhiri wa historia Mwambutsya Ndebesa kutoka chuo kikuu cha Makerere anaona mfano wa hatari kutoka nchi jirani ya Burundi, ambako kundi la vijana wa chama tawala la Imbonerakure, linatuhumiwa kwa kuwauwa wapinzani wa serikali.

"Kuufanya uchaguzi kuwa wa kijeshi..kunachochea hasira za kisiasa kwa kiwango ambacho vurugu zinaelekea kutokea," alisema Ndebesa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe

Mhariri: Saumu Yusuf