1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya kumbukumbu ya uasi ulioshindwa wa Watibet dhidi ya utawala wa China.

Sekione Kitojo10 Machi 2009

Ulinzi mkali umewekwa hii leo katika jimbo la Tibet , wakati Watibet wakikumbuka miaka 50 ya uasi dhidi ya utawala wa China katika jimbo hilo.

https://p.dw.com/p/H95M
Dalai LamaPicha: picture-alliance / dpa

Katika maadhimisho ya siku ya Tibet tarehe 10 na 14 March raia nchini China wanakumbana na hatua kubwa za uimarishaji wa usalama katika jimbo hilo pamoja na maeneo yanayopakana na Tibet. March 10 siku ya Jumanne inatimia miaka 50 katika historia ya uasi uliofanywa na Watibet dhidi ya utawala wa China. Kiongozi wa kiroho wa jimbo la Tibet Dalai Lama alikimbilia nchini India mara baada ya uasi huo na kuishi uhamishoni hadi leo.

March 14 mwaka mmoja kabla, mji mkuu wa jimbo la Tibet wa Lhasa ulishuhudia ghasia kubwa ambapo vyombo vya usalama vilisambaratisha kwa nguvu maandamano katika mji huo. Mwaka mmoja baadaye China inahakikisha kuwa hali hiyo hairejei tena. Lakini mzozo huo kuhusiana na hali ya baadaye ya jimbo la Tibet pamoja na Dalai Lama bado unaendelea bila kupatiwa ufumbuzi. Waandishi wa kigeni tayari wamekwisha zuiwa kuingia katika jimbo la Tibet.


Ni eneo la Anjue , mahali pa kufanyia ibada kwa watawa, katikati ya mji wa Kangding.

Mishumaa kadha inayowaka inaangaza chumba ambacho kina sanamu ndogo ndogo za budha. Watawa wanasali na kufanya taamuli. Bendera kadha zenye rangi mbali mbali zinapepea katika kamba nyekundu. Ni picha ya Dalai Lama tu ambayo inakosekana, picha ya kiongozi huyo wa kiroho kwa Watibet imepigwa marufuku kutundikwa popote nchini China.

China imeweka ulinzi mkali katika eneo la milima la Tibet leo Jumanne katika kumbukumbu ya mwaka wa 50 tangu kushindwa kwa uasi dhidi ya utawala wa China hali iliyomlazimisha kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama kwenda kuishi uhamishoni nchini India.

Wananchi waishio katika mji wa Kangding ni theluthi mbili ya Watibet. Mji huo uko magharibi ya jimbo la Xichuan, lakini hapa ndio panaanzia kile kinachoitwa na Watibet wanaoishi uhamisho kuwa ni Tibet kuu.

Maandamano ya amani yakiongozwa na watawa mjini Lhasa katika kumbukumbu ya mwaka jana ilizusha siku nne baadaye ghasia za kuipinga China ambayo yalisambaa katika maeneo mengine ya magharibi ya China yaliyo na Watibet.

Kilometa chache upande wa magharibi kutoka Kangding yanaonekana malori katika barabara kuu inayoelekea Tibet. Ni barabara pekee inayoelekea upande wa magharibi , lakini katika siku hii polisi wanachunguza nani anaendesha magari hayo. Waandishi kutoka mataifa ya kigeni hawaruhusiwi .

Lakini sababu ni wazi. Katika mji wa Litang, kiasi cha kilometa 250 upande wa magharibi , Watibet kwa muda wa wiki kadha wamekuwa wakifanya maandamano. Katika jimbo lote la Tibet pamoja na maeneo mengine ya Tibet katika jimbo la Xichuan , Ganzu na Qinghai hali imekuwa ya wasi wasi. Pia katika mji wa Kangding polisi wanafanya doria. Jeshi pia limewekwa katika maeneo ya nje ya mji huo katika siku ya leo ya kumbukumbu hiyo. Maafisa wa polisi katika jimbo la Tibet pamoja na maeneo mengine yenye hali ya wasi wasi ya magharibi ya China wamewekwa katika hali ya tahadhari ya kutokea ghasia. Wakaazi na wafanyabiashara katika mji mkuu wa jimbo hilo Lhasa wameripoti kuona polisi zaidi wakifanya doria mitaani katika mji huo leo Jumanne.

Mtawa huyu kijana anacheka na anachezea simu yake ya mkono huku akiwa na wasi wasi, njia muhimu ya mawasiliano katika eneo hili la Watibet.

Mtawa mwingine anatuita katika kijiji chenye wakaazi karibu 800 kando ya mji wa Kangding.


Kwangu mimi Dalai Lama tumemuweka moyoni mwetu kabisa, kwangu mimi yeye ni mfalme. Ni kitu pekee ambacho ni muhimu na kwamba anaweza kurejea nchini China.


Ni maneno ya matumaini, lakini miaka 50 baada ya uasi uliotokea mjini Lhasa dhidi ya utawala wa China, mzozo wa hali ya baadaye ya Tibet na maeneo ya Tibet bado haujapatiwa jibu.