1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka hamsini ya uhusiano wa kibalozi

Mtullya 12 Mei 2015

Ujerumani na Israel zinauadhimisha mwaka wa 50 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi baina yao. Na kwa ajili ya maadhimisho hayo, Rais wa Israel Reuven Rivlin anafanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1FOX9
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na mpenzi wake Daniela Schadt akiwa pamoja na rais wa Israel Reuven Rivlin na mkewe Nechama Rivlin.
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na mpenzi wake Daniela Schadt akiwa pamoja na rais wa Israel Reuven Rivlin na mkewe Nechama Rivlin.Picha: Reuters/H. Hanschke

Rais wa Israel Rivlin aliewasili jana nchini Ujerumani leo amekutana na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Viongozi hao wamezungumzia juu ya uhusiano baina ya nchi zao na juu ya mgogoro wa mashariki ya kati.

Baadae leo Rais wa Israel Rivlin atakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwenye hafla ya kuadimisha mwaka wa 50 tokea Ujerumani na Israel ziuanzishe uhusiano wa kibalozi baina yao.

Hapo awali marais wa Israel Rivlin na wa Ujerumani Joachim Gauck katika nyakati tofauti za mahojiano ya magezti walitanabahisha juu ya kuongoeza kwa hisia za chuki dhidi ya wayahudi barani Ulaya. Marais hao wametoa mwito wa kujitokeza na kupambana na chuki hizo.

Rais Rivlin amesema: "Harakati dhidi ya ubaguzi,chuki dhidi ya wayahudi na dhidi ya itikadi kali zinahitaji tuwe macho na imara.Tunapaswa kukumbuka kwamba demokrasia peke yake haitupi kinga dhidi ya itikadi kadi na ufashisti."

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na mwenzae wa Israel Reuven Rivlin
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na mwenzae wa Israel Reuven RivlinPicha: Reuters//Bundesregierung/Steffen Kugler

Miaka 50 iliyopita Rivlin alikuwa mpinzani mkali wa uhusiano wa kibalozi baina ya Israel na Ujerumani.Na wakati balozi wa kwanza wa Ujerumani alipowasili nchini Israel, Rivlin alikuwa miongoni mwa waandamanaji waliomtaka balozi huyo wa Ujerumani aondoke nchini Israel.

Uhusiano umeendelea kuwa mzuri baina ya Israel na Ujerumani

Hata hivyo katika kipindi cha miaka 50 iliyopita uhusiano baina ya Israel na Ujerumani umejengeka na kuwa madhubuti. Juu ya uhusiano huo Waziri wa mambo yanje wa Ujerumani Frank-Waltre Steinmeier amesema:

"Leo ziara baina ya viongozi wa Ujerumani na Israel zimekuwa jambo la kila siku.Wajumbe wa serikali za Israel na Ujerumani wanakutana kwa ajili ya mashauriano mara moja kila mwaka.Tunapanga miradi ya pamoja, tunajadiliana, tunacheka lakini pia mara nyingine tunatafautiana kama jinsi ilivyo ada ya marafiki wazuri."

Israel na Ujerumani zinaendelea kutafautiana juu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza wazi kabla ya kukutana na Rais wa Israel baadae leo, kwamba Ujerumani inaunga mkono suluhisho la kuundwa nchi mbili baina ya Israel na Wapalestina.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauk akimkaribisha ujerumani rais wa Israel Reuven Rivlin
Rais wa Ujerumani Joachim Gauk akimkaribisha ujerumani rais wa Israel Reuven RivlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Kansela Merkel amesisitiza kwamba suluhisho hilo ndilo litakaloleta amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati.

Rais wa Israel Reuven Rivlin ameanza ziara rasmi nchini Ujerumani siku tatu tu baada ya kufanyika maadhimisho ya mwaka wa 70 tokea majeshi ya fashisti Hitler yasalimu amri baada ya kuwaangamiza wayahudi milioni sita barani Ulaya wakati wa vikuu vya pili.

Rais Rivlin leo atazungumza na wenyeji wake Kansela Merkel na Waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinemeier pia juu ya serikali mpya iliyondwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Mwandishi:Mtullya abdu./dpa, ZA

Mhariri: Iddi Ssessanga