1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka minne ya mzozo wa Darfur

Mohammed Abdul-Rahman3 Mei 2007

Kiongozi wa Rwanda atishia kuwaondoa wanajeshi wa nchi yake jimboni humo. Asema hakuna kinachofanyika kwa sababu ya ukosefu wa hatua za kivitendo na nyenzo.

https://p.dw.com/p/CHEu
Rais Paul Kagame wa Rwanda
Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: AP

Jumamosi tarehe 5 Mei itatimia miaka minne tangu uliporipuka mzozo wa jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur. Pia itakua ni mwaka mmoja tangu uliposainiwa mkataba wa kumaliza mgogoro huo katika mji mkuu wa Nigeria –Abuja-mkataba ambao hadi sasa umeshindwa kuzaa matunda. Wakati huo huo Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye nchi yake imechangia majeshi katika kikosi cha kulinda amani cha umoja awa Afrika huko darfur anasema kwamba wanajeshi wa umoja huo wameshindwa kuwajibika kwa sababu ya uhaba wa nyenzo kuweza kutimiza wajibu wao.

Katika mahojiano na Shirika la habari la Reuters, Kiongozi huyo wa Rwanda alielezea kuvunjwa moyo kwake na hali ya kuendelea kwa mgogoro huo wa miaka minne sasa wa Darfur na kusema ana utahadharisha ulimwengu kwamba huenda akalazimika kuwaondoa wanajeshi 2000 wa nchi yake sehemu ya kikosi cha wanajeshi 7000 wa kulinda amani cha umoja wa Afrika jimboni humo.

“Kuna haja gani ya wao kukaa tu juani badala ya kufanya wanachowajibika kufanya kuwasaidia watu wanaoathirika wa Darfur,” aliuliza Rais Kagame baada ya kutoa mhadhara wakati wa somo la historia katika chuo cha Baruch mjini New York. Pamoja na hayo hakutaja muda maalum wa kuondoka kwa majeshi ya Rwanda, isipokua aliutanabahisha ulimwengu kuwa hauna budi kuchukua hatua za kivitendo.

Mwaka uliopita, baraza la usalama la umoja wa mataifa,lilipitisha azimio la kutumwa wanajeshi wa pamoja wa umoja wa mataifa na umoja wa Afrika zaidi ya 20,000 huko Darfur, lakini Rais Omar Hassan al Bashir wa sudan amekubali paweko na watumishi wa polisi na jeshi 3,000 wa umoja wa mataifa kukisaidia kikosi cha umoja wa Afrika.

Rais Kagame anasema si Sudan pekee ya kulaumiwa, kwa ucheleweshaji wa zoezi hilo pamoja na nyenzo, bali kuna pande tatu- umoja wa mataifa, umoja wa Afrika na serikali ya Sudan Alisema hawana budi kukaa pamoja na kusaka suluhisho.

Nalo shirika la haki za binaadamu Human rights watch, limeitaaka serikali ya Sudan kuwakabidhi watu wawili muhimu katika tuhuma za kuhusika na mwaagaji damu huko Darfur, ambao wanatakiwa na mahakama ya jinai ya kimataifa. Mahakama hiyo imetoa waranti wa kukamatwa waziri wa nchi anayehusika na masuala ya binaadamu Ahmed Haroun na Kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed Ali Kosheib, wanaokabiliwa na mololongo wa mashitaka dhidi ya binaadamu na uhalifu wa kivita.

Hadi sasa serikali ya Sudan imekataa kuitikia wito wa mahakama hiyo-hali ambayo wadadadisi wanasema inazusha matatizo mengine katika usakaji wa suluhisho la mgogoro huo.