1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano ya vita vya Irak magazetini

Eickenfonder, Susanne20 Machi 2008

Wahariri wa magazeti wanakosoa sera za Marekani nchini Irak

https://p.dw.com/p/DRiT
Maandamano ya Chicago dhidi ya vita vya IrakPicha: AP



Miaka mitano ya vita nchini Iraq ndio mada iliyohanikiza magazetini hii leo.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na hotuba ya jana ya rais George Bush aliyetetea kisa cha kuvamiwa Iraq kwa kusema lilikua jambo la lazma.Bush amekiri hata hivyo vita vinadumu muda mrefu zaidi kuliko ilivyokadiriwa ,ni vikali zaidi na vimegharimu fedha nyingi zaidi hadi sasa- dala bilioni 500.


Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani yanapindukia hoja hizo.Kwa mfano gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linalohisi:


"Imedhihirika kwamba vita vya kimambo leo havina maana yoyote.Ama nchi inakaliwa moja kwa moja au vita vinaendeshwa kwa kutilia maanani kanuni zake ipasavyo;yaani kuwepo askari kanzu,vikosi maalum na kuachana na sheria za vita.Au  watu wanatanguliza mbele juhudi za amani,kupitia diplomasia na msaada wa kigeni.....Ujinga wa serikali ya Bush umepelekea kufanyika kosa kubwa ambalo halistahiki kurudiwa.Kishindo kikubwa kilichotokana na vitisho vya kiigaidi vya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam si hoja hata kidogo."


Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika:


"Demokrasia imechafuliwa na kupagazwa sifa ya "chombo cha wavamizi jabari wenye majivuno".Maadili ya maana,yamegubikwa na madai ya makusudi ya nadharia za kidini-kwa mfano humsikii yeyote anaezungumzia suala la haki ya wakinamama.Makamo wa rais wa Marekani Dick Cheney hajakosea aliposema:kazi haijakamilika.Lakini ni kazi nyengine,na sio ile anayoifikiria.Inahusu ujenzi wa amani.Lakini sera za Marekani hadi sasa zimekua zikikorofisha jambo hilo."


Mhariri wa gazeti la NEUEN DEUTSCHLAND ameandika:


"Pale rais George W. Bush,akiwa ndani ya manuari ya kijeshi katika Ghuba,siku 41 tuu baada ya vita kuanza nchini Irak,alipotoa tangazo lake,alitaka kuutanabahisha ulimwengu mzima:vita vilivyoanza March 20 mwaka 2003,ili kumng'owa madarakani muimla wa Iraki,vimemalizika kwa muda mfupi kupita kiasi.Lakini ukweli wa mambo haujakawia kuisuta picha hiyo ya udanganyifu.Pengine ni kweli kwamba wairak wengi tuu walishusha pumzi Sadam Hussein alipong'olewa madarakani-lakini visa vya matumizi ya nguvu,watu kudhalilishwa,maajivuno ya kibaguzi na kujitajirisha bila ya aibu wamarekani,yote hayo yakichanganyika na hali ya kutokuwepo mpangilio,yameigeuza Irak kua jahanam ya vita na vitisho."


Gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG la mjini Gera linaandika:


"Kulikua na wakati ambapo nchini Marekani liliibuka vuguvugu la wanaharakati waliohaninikiza kutaka vita vikome haraka.Wakati huo umeshapita lakini.Kampeni za uchaguzi zilizogubikwa na madai ya kutaka vita vikome kama wengi wa wafuasi wa chama cha Democrats walivyokua wakitarajia,hazikushuhudiwa.Na hali hiyo itasalia vivyo hivyo kwa wakati wote ambapo matumizi ya nguvu nchini Irak hayatakiithiri, yatasalia kama yalivyo wakati huu tulionao ambao hakuna anaeshutuka."


Hatimae gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER linatathmini hali ya mambo kama ifuatavyo:


"Katika jamii ya Marekani, vita vya Irak,miaka mitano baadae ,vimegeuka sehemu ya maisha yao ya kawaida.Wanahisi aa,ndio  vimeshatokea tena,watafanya nini.Lakini kuna wengine wanaosononeka ndani kwa ndani,hawapendi hata kuzungumzia,mfano wa maradhi hatari,ambayo unayazungumzia tuu kama huna budi.