1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michafuko inazidi nchini Iran

28 Desemba 2009

<p>Iran inajitayarisha kwa maandamano mengine, hivi leo, baada ya watu 8 kuuwawa jana katika machafuko mabaya kabisa tangu uchaguzi wa Juni uliogubikwa na utata, uliomrejesha madarakani Rais Mahmoud Ahmedinejad.

https://p.dw.com/p/LFUn
Michafuko IranPicha: AP
Televisheni ya kitaifa PRESS TV pia iliripoti zaidi ya watu 300 wamekamatwa kufuatia machafuko hayo nchini Iran.

Machafuko katika mji wa Tehran na miji mingine, nchini Iran yalifanyika wakati wa maadhimisho ya sherehe za siku ya Ashura- siku kubwa inayoadhimishwa na wafuasi wa dhehebu la Washia.

Kulingana na Televisheni ya kitaifa, PRESS TV watu wanane waliuawa- katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji ambao wamekuwa wakichukua fursa ya sherehe au maadhimisho yeyote sherehe nchini Iran, kuendeleza pingamizi zao dhidi ya serikali.

Hata hivyo mtandao wa upinzani, ulikuwa na ripoti tofauti ukidai zaidi ya watu 15 waliuawa katika machafuko hayo, wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji.

Ripoti kutoka kwa maaafisa wa serikali pia zinasema watu 300 wamekamatwa kufuatia ghasia hizo, ambazo huenda pia zikaendelea hivi leo. Mehdi Karroubi ambaye ni mmoja wa viongozi wa upinzani alishtumu umwagikaji huo wa damu uliofanyika katika siku muhimu ya Ashura, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa heshima ya Imam Hussein.

Karroubi aliukosoa utawala wa kiislamu nchini Iran, akisema hata Shah aliheshimu siku ya Ashura. Mtandao mmoja wa upinzani pia ulisema miongoni mwa waliokamatwa ni Ebrahim Yazid, kiongozi wa chama cha Freedom Movement. Yazid, ambaye alikuwa waziri wa mambo  ya nchi za nje katika serikali ya kwanza nchini Iran, baada ya kutimuliwa kwa Shah, anasemekana hana uhusiano na upinzani nchini Iran, lakini aliunga mkono maandamano ya jana dhidi ya rais Ahmedinejad.

Pia miongoni mwa wale waliouawa inasemekana na binamu ya kiongozi wa upinzani Mir Hossein Moussavi. Ali Moussavi mwenye umri wa miaka 20 anasemekana aliuawa katika  kati kati mwa mji wa Tehran, pale vijana walipokabiliana na polisi.

Polisi nchini Iran wanasema wameanzisha uchunguzi, kufuatia mauaji hayo. Televisheni hiyo ya kitaifa ilitoa taarifa ikisema polisi wamekana kuhusika na mauaji hayo ya watu wanane. Kituo hicho cha Televisheni pia kiliripoti maafisa wengi wa polisi na wale wa kundi la Basij walijeruhiwa katika machafuko ya jana.

Ikulu ya Marekani imelaani matukio hayo ya jana nchini Iran. Katika taarifa Ikulu hiyo ilisema inashtumu kwa dhati jinsi utawala nchini Iran unatumia nguvu kukandamiza haki za raia wake- haki za kujieleza. Taarifa hiyo iliendelea kusema Marekani ipo katika upande wa waandamanaji.

Utata kufuatia uchaguzi wa Juni umeitumbikiza Iran katika mvutano mkubwa wa kisiasa, ambao haujawahi kutokea tangu yale mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Mwandishi : Munira Muhammad/ RTRE

Mhariri:Othman Miraji