1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michelle Obama ampigia debe Barack Obama

P.Martin26 Agosti 2008

Chama cha Demokratik nchini Marekani kimefungua mkutano wake wa taifa mjini Denver Colorado siku ya Jumatatu,huku wajumbe wakijitayarisha kumteua rasmi Barack Obama kugombea urais kwa tikti ya chama hicho.

https://p.dw.com/p/F4zQ
Michelle Obama, wife of Democratic presidential candidate, Sen. Barack Obama, D-Ill., speaks during the Democratic National Convention in Denver, Monday, Aug. 25, 2008. (AP Photo/Chris Carlson )
Michelle Obama,mke wa mgombea urais wa Demokratik akihotubia mkutano wa taifa wa chama cha Demokratik mjini Denver,Agosti 25,2008.Picha: AP

Siku ya mwanzo ya mkutano huo ilikamilishwa kwa hotuba ya Michelle Obama aliechukua fursa hiyo kuwaeleza wajumbe mkutanoni kwanini mume wake Barack Obama achaguliwe rais katika uchaguzi ujao.Hotuba hiyo ilituwama zaidi juu ya maisha yake na Barack Obama na hasa alieleza kule walikotokea.Amemsifu mume wake kama baba na mume muadilifu ambae siasa zake zinatokana na mila na tamaduni za Kimarekani. Akizungumza mbele ya zaidi ya wajumbe 4,000 waliokusanyika Denver kutoka kila pembe ya Marekani,Michelle Obama alieleza jinsi yeye na mume wake walivyokulia katika mazingira ya kawaida.Kwa hivyo amesema,yeye na Barack Obama wanaelewa vizuri shida zinazokabiliwa na umma katika maisha yao ya kila siku.Amesema,ni imani na jitahada za wazazi wao zilizowasaidia kufika pale walipo hii leo.Kwa hivyo anajua kuwa kila Mmarekani anaweza kutimiza ndoto yake.Akaongezea:

"Ninaamini kuwa kila mmoja wetu bila ya kujali umri,mazingira au kule tulikotokea-kila mmoja ana uwezo wa kutoa mchango wake katika maisha ya taifa hili."

Kwa kweli hotuba yake ilijaribu kuwaeleza wapiga kura zaidi kuhusu Barack Obama aliewasili katika uwanja wa kisiasa baada ya kuchaguliwa seneta miaka minne iliyopita tu.

Lakini mbali na hotuba hiyo ya kusisimua,mkutano wa chama cha Demokrat hiyo jana ulifikia kilele chake,pale Seneta Edward Kennedy mwenye miaka 74 alipojitokeza bila ya kutazamiwa.Kennedy anaeumwa saratani ya ubongo amesema,hakuna kilichoweza kumzuia kufika katika mkutano muhimu kama huo.Amesema,kuteuliwa kwa Obama kugombea urais ni ishara ya matumaini mapya kwa Marekani.Edward Kennedy ni seneta mwenye ushawishi mkubwa katika chama cha Demokratik.