1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

23 Oktoba 2009

Kombe la dunia 2010-n'gombe kutolewa mhanga ?

https://p.dw.com/p/KDzA
Uwanja wa dimba A.KusiniPicha: AP

-Ujerumani yakanusha kuwashauri wachezaji wake wa taifa kwa Kombe lijalo la dunia kuvaa vizbao vya kinga ya risasi watakapokwenda mwakani Afrika Kusini.

Je, FIFA itaruhusu kuchinjwa n'gombe katika kila kiwanja kati ya 10 vitakavyochezewa Kombe la dunia kama mila za kienyeji huko zinavyodai ?

Kombe la COSAFA la Kusini mwa Afrika, linaendelea huko Zimbabwe.

Matumaini ya timu ya taifa ya Comoro "Coelacanthe" kusonga mbele katika kinyan'ganyiro hiki yalizimwa kati ya wiki na Swaziland.Swaziland, iliikandika Comoro mabao 3:0 mjini Bulawayo.

Kabla changamotro hiyo,Comoro ikiongozwa na kocha wao Mohammed Shamte ikiongoza kundi lao kufuatia kutoka sare baop 1:1 na Botswana.Comoro baadae ikawalaza jirani zao visiwa vya Ceyschelles mabao 2:1.Comoro sasa iko nafasi ya 3 ya kundi lake mbele ya Ceyschelles.

KOMBE LA DUNIA 2010 :

Taarifa kutoka Frankfurt,makao makuu ya Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) zinakanusha taarifa kuwa wachezaji wa timu ya taifa wameshauriwa kuvaa vizbao vya kinga ya risasi-bullet-proof vests-watakapokwenda Afrika kusini kwa Kombe la dunia hapo mwakani.

Taarifa hizo kutoka mkuu wa kampuni moja la usalama la kibinafsi, imezusha msasngao na mtafaruku huko Afrika kusini hapo juzi alhamisi,lakini Shirikisho la kabumbu la Ujerumani (DFB) limesema taarifa hizo hazina msingi.

Mkuu wa usalama wa shirikisho hilo Bw.Helmut Spahn,amefunga safari ya Afrika kusini na ujumbe mdogo mwishoni mwa wiki hii, ili kuangalia hali ilivyo pale timu ya Ujerumani itakapopiga kambi yake karibu na jiji la Pretoria.

Stenger alisema kwamba, katika maswali ya usalama, shirikisho la dimba la Ujerumani DFB halitajichukulia hatua pekee,bali hatua zote za ulinzi zitachukuliwa kwa ushirikiano na FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni pamoja na serikali ya Afrika Kusini.

Gazeti la kila wiki la michezo la Ujerumani -SPORT BILD- lilimnukulu Günther Schnelle wa kampuni la usalama BAYSECUR kusema kwamba, nyendo za wachezaji wa Ujerumani nje ya mipaka ya Hoteli watakayofikia zisiwe nyingi sana kutokana na wasi wasi wa uhalifu nchini Afrika Kusini.

BAYSECUR ni mojawapo ya makampuni ya usalama linalotazamia kuajiriwa na DFB -Shirikisho la dimba la Ujerumani, kukilinda kikosi cha Ujerumani kati ya Juni 11-hadi finali ya Kombe la dunia, Julai 11,mwakani.

Mkasa mwengine uliogonga vichwa vya habari kuelekea Kombe la dunia 2010 ni ule wa kutolewa mhanga n'gombe ili kuvizindua viwanja 10 vitakavyochezewa Kombe la Dunia 2010 huko Afrika kusini kwa muujibu wa mila za kienyeji : Je, FIFA,itakubaliana na mhanga huo ?

Taarifa kutoka Johannesberg , zinasema ikiwa viongozi wa kienyeji wataachiwa kuwa na usemi,n'gombe watatolewa mhanga kwa kuchinjwa katika viwanja vyote 10 kabla dimba kuanza. Shirika linalowakilisha falme za kienyeji linadai kwamba, ngombe wachinjwe katika kila kimoja kati ya viwanja 10 kulingana na itikadi za kale .

"Hii ni muhimu ili kuvibariki viwanja hivyo.Kuchinja kinyama katika kila kiwanja ni kama kuvichangamsha viwanja."Alisema Mkiva, muimbaji nyimbo za sifa kwa mzee MANDELA:

LAKINI WAKATI NI MILA NA DESTURI ZA BAADHI YA MAKABILA YA AFRIKA KUSINI KUCHINJA KINYAMA KAMA MHANGA AMA KATIKA SHEHERE ZA KUZALIWA MTOTO,HARUSI AU SHEREHE NYENGINEZO AU KUMKUMBUKA JAMAA ALIAGA DUNIA, HAKUNA DESTURI YA KUMWAYA DAMU KATIKA VIWANJA VYA MPIRA:

Mkiva amesema kwamba, shirika lake limeomba mkutano na Kamati ya maandalio ya kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini kuzungumzia swali hilo.Afrika kusini, imejenga viwanja 5 vipya na imevitengeza vitano vyengine kwa ajili ya Kombe la dunia .

Viwanja vyote hivyo, vinatarajiwa kukamilisha ujenzi Desemba mwaka huu.

Alipoulizwa maoni yake juu ya kuchinjwa n'gombe hao viwanjani,Delia Fischer,msemaji wa Kamati ya Maandalio ya Kombe la dunia ya FIFA 2010, aliliambia gazeti la CITIZEN, kuwa FIFA, itabidi kwanza kukichunguza kisa hicho.

Je, Bafana Bafana, wataka kuroga uwanjani kabla ya firimbi kulia Juni 11,2010 kwa kombe la kwanza la dunia barani Afrika ?.Lakini sio kila bara lina mila zake ?

Muandishi: Ramadhan Ali