1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wikiendi: David Rudisha kukosa mashindano ya Moscow

Mohamed Abdulrahman19 Julai 2013

Zambia, Zimbabwe kumenyana fainali ya Cosafa Jumamosi hii, timu za Ujerumani kujipima nguvu huko mjini Monchengladbach. David Rudhisha kukosa mashindano ya Moscow na timu za Ulaya zaanza kujianda na msimu wa ligi.

https://p.dw.com/p/19ApQ
epa03353379 David Lekuta Rudisha of Kenya celebrates winning the men's 800m final at the London 2012 Olympic Games Athletics, Track and Field events at the Olympic Stadium, London, Britain, 09 August 2012. At right is Nijel Amos of Botswana who placed second. EPA/BERND THISSEN +++(c) dpa - Bildfunk+++
London 2012 - LeichtathletikPicha: picture-alliance/dpa

Msukosuko klabu bingwa Afrika

Mashindano ya ligi ya vilabu bingwa vya Afrika yamekumbwa na msukosuko mwishoni mwa juma hili huku mechi moja ikifutwa na nyengine ikiwa haijulikani itachezwa lini. Mkasa huo ni  wa kundi B, pambano kati ya  Coton Sport ya Cameroon na Sewe ya Cote dÍvoire. Pambano hilo sasa limeahirishwa kwa wiki moja pakisubiriwa matokeo ya mazungumzo baina ya chama cha kandanda cha Cameroon na  Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA, kuhusu hatua yake ya  kupiga marufuku shughuli zote za kandanda katika taifa hilo la Afrika magharibi.

Mchuano wa Coton na Sewe ulikuwa ufanyike Jumamosi hii huko Garoua, lakini  Shirikisho la soka barani Afrika CAF limesema huenda  sasa zitamenyana Julai 27 ikitarajiwa kwamba FIFA itaondoa  amri yake ya kuisimamisaha Cameroon. Shirikisho hilo la soka  la kimataifa liliipiga marufuku Cameroon Julai 4 kwa sababu serikali imeingilia uchaguzi wa chama cha kandanda  cha nchi hiyo. FIFA sasa inataka iundwe kamati kuchunguza hali ndani ya chama hicho na kuandaa uchaguzi mpya.

Mashabiki wa timu ya zamalek wakifanya fuzo mwaka 2011.
Mashabiki wa timu ya zamalek wakifanya fuzo mwaka 2011.Picha: picture alliance /dpa

Zamalek, Al Ahli kucheza bila mashabiki

Pambano jengine baina ya  mahasimu wawili huko Misri  Zamalek na Al Ahli lililopangwa kufanyika siku ya Jumapili nalo limo hatarini. Mazungumzo yamekuwa yakifanyika kati ya chama cha soka cha Misri na  na Shirikisho la kandanda  barani Afrika CAF  ambalo lilitaka  tarehe ya mchezo huo wa Kundi A la ligi ya  vilabu bingwa barani humo kibiashara ibadilishwe kwa sababu za kibiashara .

Taarifa moja kwenye mtandao  iliotolewa na Al Ahlli ilisema litachezwa Jumanne au Jumatano , lakini taarifa ya Zamalek imesema ni Jumatatu au Alhamisi ijayo. Kutokana na hofu ya ukosefu wa usalama, mchezo huo utafanyika katika mji wa bandari ya  sham wa El Gouna  bila ya mashabiki uwanjani. Pia wakati wa kukutana miamba hiyo, utabadilishwa kwa sababu uwanja huo hauna  taa za kutosha kuhudumia pambano hilo wakati wa usiku.

Zambia vs Zimbabwe fainali Cosafa
 

Fainali ya  kombe la mataifa la Shirikisho la soka la kusini mwa Afrika Cosafa inachezwa jumamosi hii, ikiwa ni kati ya  Zambia mwenyeji wa mashindano  na  Zimbabwe mchezo utakaofanyika. Zambia iliibwaga Afrika kusini katika pambano la nusu fainali Jumatano kwa mikwaju  ya penalty mabao 5-3, baada ya  kumaliza  muda wa kawaida na nyongeza zikiwa bila kwa bila. Zimbabwe  mabingwa watetezi wa kombe hilo nayo ikaiadhibu Lesotho mabao 2-1  katika nusu fainali nyengine. Pambano hili lla fainali kati ya Zambia na Zimbabwe katika uwanja wa  Levy Mwanawasa mjini Ndola, ni sawa na marudio ya ile ya  2009.

Ulaya nao wajipima nguvu

Barani  Ulaya Timu kadhaa zinaendelea kujinoa kwa michuano ya kujipima nguvu kabla ya  msimu wa ligi kuanza. Hapa Ujerumani mwishoni mwa Juma hili kunafanyika mashindano madogo ya timu nne ambazo ni mabingwa wa Bundesliaga na ligi ya vilabu bingwa vya ulaya na Champions league Bayern Munich, makamu bingwa  wa ligi kuu ya Ujerumani na  Champions league  Borussia Dortmund, Wenyeji Borussia Monchengladbach na  Hamburg.
Pindi ni Dortmund na  Bayern zitakazochuana katika fainali Jumapili ya kesho, basi itakuwa ni marudio ya  pambano la mwezi Mei la champions league ambapo Bayern waliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Dortmund hata hivyo inakabiliwa na matatizo  kwani mshambuliaji wake aliyesajiliwa karibuni Henrikh Mkitaryan atakuwa nje ya chaki kwa muda wa wiki nne kutokana na maumivu ya kisigino. Lakini Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 24 na mchezaji wa kimataifa wa Armenia aliyesajili na Dortmund kwa kitita cha euro milioni 25 anatarajiwa kuwemo katika  kikosi cha Dortmund kwa pambano la nyumbani dhidi ya Eintracht Braunschweig Agosti 18.

Chelsea yakiri kumuwinda Wayne Rooney

Wayne Rooney.
Wayne Rooney.Picha: picture-alliance/dpa

Huko Uingereza  harakati za usajili wa ligi kuu Premier League zinaendelea. Wiki hii kilabu ya  Chelsea ilithibitisha kwamba imetuma pendekezo la maandishi kwa mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney kwa nia ya kumsajili kwa kiwango cha fedha ambacho hakikutajwa, lakini wakati huo huo ikakanusha ikisema hakuna mchezaji aliyependekezwa kwa kitita kikubwa.  Akizungumza na waandishi habari mjini Bangkok-Thailand ambako Chelsea ilikuwa ziarani kwa mechi za kujipima nguvu kabla ya msimu wa ligi kuanza, Kocha wa timu hiyo Jose Morinho ambaye yumo mbioni kutafuta mshambuliaji mpya, alithibitisha kwamba kuna harakati zinazoendelea kumsajili Rooney na  yaliosemwa yameshasemwa na hana la kuongeza bali wanasubiri.

Awali Morinho aliungama kwamba ana mhusudu sana  Rooney. Hata hivyo Kocha wa Manchester united David Moyes amekuwa akirudi kusema mara kwa mara kwamba  Rooney ambaye ametaka aruhusiwe kuihama  kilabu  hiyo bingwa ya  England, hatouzwa. Alisema Wayne ni mchezaji wa Manu na ataendelea kuwa hivyo.

Wakati huo huo jitihada za  mabingwa wa England  Manchester United kutaka kumsajili, mchezaji wa kiungo wa Barcelona Cesc (the es) Fabregas zinaelekea zimegonga mwamba. Mchezaji huyo amesema hana nia yoyote ya kuihama klabu hiyo na kurejea tena England- Uingereza .

Majeraha yamuondoa David Rudisha Moscow

Mwanariadha kutoka Kenya na bingwa wa dunia wa  mbio za mita 800 David Rudisha  hatoshiriki katika mashindano ya  riadha ya ubingwa wa dunia mjini Moscow mwezi ujao. Rudisha alitangaza Jumanne kwamba anaendelea kupata nafuu ya goti lakini  maendeleo yake ni ya taratibu, kwa hiyo kutokana na  muda uliosalia hadi mashindano hayo hafikirii atakuwa amepona kikamilifu. Hayo pia yalielezwa na  kocha wa  mwanariadha huyo Colm O´Connell, ambaye alisikitishwa kwake  akisema  matumaini ya taifa  la Kenya yalikuwa makubwa.  Pamoja na hayo  O´Connell alisema kukosekana kwa Rudisha  mwenye umri wa miaka 24, katika mashindano hayo ya Moscow kutatoa nafasi kwa wanariadha wengine. Akizungumzia hilo Makamu mwenyekiti wa chama cha wanariadha nchini Kenya David Okeyo alisema wamechagua wawakilishi wenye uwezo katika mbio za mita 800 na wana uhakika hawatawangusha.

epa03353379 David Lekuta Rudisha of Kenya celebrates winning the men's 800m final at the London 2012 Olympic Games Athletics, Track and Field events at the Olympic Stadium, London, Britain, 09 August 2012. At right is Nijel Amos of Botswana who placed second. EPA/BERND THISSEN +++(c) dpa - Bildfunk+++
London 2012 - LeichtathletikPicha: picture-alliance/dpa

Mashindano ya riadha  ya ubingwa wa dunia yamepata pigo jengine kutokana na  kujiondoa kwa bingwa wa dunia wa mbio za mita 100 Yohan blake wa jamaica kwa sababu ya majeraha. Mwanariadha huyo alishinda ubingwa huo  katika michezo ya 2011 ya Daegu licha ya kumaliza nafasi ya pili, alipotunukiwa medali ya dhahabu kutokana na  Usain Bolt pia kutoka Jamaica  kuchomoka kabla ya  wakati. Blake mwenye umri wa miaka 23 aliumia Aprili  mwaka huu na  hali hiyo ilimsababisha pia kuyakosa mashindano ya majaribio nyumbani, Jamaica.

Kutoshiriki kwake mjini Moscow mwezi ujao sio tu kutainyima Jamaica nafasi ya  kumuona akitetea ubingwa wake, lakini pia Kisiwa hicho kitawakosa baadhi ya wanariadha wake ambao wamekumbwa na kashfa ya  utumiaji wa madawa yaliopigwa marufuku yenye kuimarisha nguvu za misuli. Itakumbukwa Jumapili iliopita bingwa wa zamani  wa dunia  wa mbio za mita 100 Asafa Powell na mshindi wa medali ya dhahabu ya olimpik Sherone Simpson walisem wamegunduliwa baada ya uchunguzi  kutumia  aina fulani ya dawa zilizopigwa marufuku. Kashfa hiyo pia imemkumba mwanariadha wa Marekani Tyson Gay.

Katika ringi ya  ubondia, Mji mkuu wa Qatar-Doha utakuwa mwenyeji wa mashindano ya ndondi ya  ubingwa wa dunia, baada ya kulishinda jiji la Bangkok nchini Thailand katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka ujao 2014. Mbali na ndondi Qatar pia itakuwa mwenyeji wa Kombe la  kandanda la dunia 2022 na  mashindano ya ubingwa wa dunia wa mpira wa mikono-handball 2015 na  ya mbio za baiskeli barabarani 2016. Uamuzi wa Jumatano wiki hii wa kuipa nafasi Qatar kuwa mwenyeji wa  mashindano ya  ndondi ya ubingawa wa dunia  2015 ulichukuliwa katika mkutano wa  kamati tendaji ya  Chama cha kimataifa mabondia wa ridhaa  mjini Jeju Korea kusini.

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani, Wolfgang Niersbach .
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani, Wolfgang Niersbach .Picha: dapd

Kandanda na ushoga Ujerumani

Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB limewasilisha kijigazeti  kwa njia ya mtandao na kufungua mjadala kuhusu suala la Kandanda na ushoga, kwa lengo la kuwasaidia mashoga waweze kujitokeza hadharani na kujieleza jinsi walivyo. Maelezo yaliomo ni pamoja na taarifa, ufafanuzi wa  maneno na anuwani za  mawasiliano kuhusiana na  suala hilo ambalo limekuwa ni mwiko.

Rais wa Shirikisho la kandanda la Ujerumani Wolfgang Niersbach alisema katikati ya juma kwamba kila mchezaji kandanda awe shoga wa kiume au wakike anaweza kutegemea msaada wa DFB. Waziri wa sheria  wa Ujerumani Sabine Leutheusser Schnarrenberger, amependekeza kwamba kocha wa timu ya taifa  Joachim loew na baadhi ya  wachezaji washriki katika tamasha la  kila mwaka kutetea haki za mashoga linalojulikana kama Christopher Street Day, akiongeza kwamba Shirikisho la kandanda  kuwa na nafasi yake katika  tamasha hilo 2014  litakuwa jambo zuri kabisa.

Mwaka 2011 mlinda mlango wa timu ya soka ya  Ujerumani ya wanawake Nadine Angerer alijitokeza wazi  kuungama kwamba anafanya mapenzi na watu wa jinsi zote mbili akiwataka mashoga kujitokeza bila kujali athari za kuungama kwao. Huko Marekani mchezaji mkongwe wa  mpira wa vikapu Jason Collins alitangaza hadharani kupitia  jarida moja amaarufu la  michezo mwezi Mei mwaka huu kwamba yeye ni Shoga.  Suala la Ushoga  na haki za mashoga linaendelea kuwa kumzo na zingatio katika sekta mbali mbali za jamii takriban kote duniani na sasa  linajikita katika sekta ya michezo.
 

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Saumu Yusuf