1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo ya Olimpiki

Liongo, Aboubakary Jumaa20 Agosti 2008

Wakati michuano ya Olympic ikielekea ukingoni, Kenya na Ethiopea zimekuwa mwokozi wa bara la Afrika kwani mpaka sasa zimeweza kujinyakulia medali mbili za dhahabu kila mmoja

https://p.dw.com/p/F1U7
Kenenisa Bekele wa Ethiopia akishangilia baada ya kufuzu kwa fainali ya mbio za mita 10,000 katika michezo ya Olympic mjini BeijingPicha: AP

Hata hivyo lakini Kenya inaziada ya medali nne za fedha na ni majogo wa riadha kutoka katika nchi hizo ndiyo waliwika, na bado wanatarajiwa kuwika.


Kwa upande mwengine Kamati ya Kimataifa ya Olympic imesema kuwa michezo ya olimpik ya mwaka huu mpaka sasa imeweka rekodi ya kutizamwa na idadi kubwa zaidi ya watu.


Kwa kutumia teknolojia mpya ya mtandao wa internet watu wengi wamekuwa wakifuatilia michezo hiyo moja kwa moja kutoka huko Beijing, mbali ya wale wanaofuatilia kwa kutumia runinga.


Mfano kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya watu bilioni 1.2 walishuhudia sherehe za ufunguzi, huku watu milioni 40 nchini Marekani pekee wakishuhudia muogeleaji wao Michael Phelps akitwaa medali ya nane ya dhahabu.


Ama katika kandanda la wanaume, Brazil jana ilitimuliwa nje ya michuano hiyo na hasimu wake Argentina katika nusufainali kwa kutandikwa mabao 3-0, huku Nigeria wakiingia kwa kishindo fainali baada ya kuivuruga Ubelgiji kwa mabao 4-1.


Kwa Brazil hivi sasa kina dada wa timu ya soka ndiyo wanaotegemewa kuyaponya majeraha hayo itakapopambana na Marekani katika fainali.


Kuhusiana na jedwali ya medali katika michuano hiyo, huyu hapa mwenzangu alijiunga nasi hapa Deutsche Welle hivi punde kutoka Mombasa nchini Kenya Eric Ponda.


´´Akhsante Abou. Mpaka sasa China ndiyo inayoongoza kwa kuwa na medali 44 za dhahabu, 14 fedha na 19 shaba ikifuatiwa na Marekani yenye 26 dhahabu, 26 fedha na 27 shaba.


Uingereza ambayo ni muandaji wa michezo ijayo ya majira ya joto ya Olympic ya mwaka 2012 ni ya tatu ikiwa dhahabu 16 10 fedha na 10 shaba.


Ujerumani iko katika nafasi ya sita baada ya kunyakua medali 11 za dhahabu,8 fedha na 9 shaba´´