1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mipango mipya kuzuwia "Brexit" kuwasilishwa

Iddi2 Februari 2016

Umoja wa Ulaya utazindua mipango ya mabadiliko, ukiwemo mfumo wa "kadi nyekundu" ambao utaruhusu mabunge ya kitaifa kuzuwia sheria zilizotungwa na umoja huo, katika juhudi za kuepusha Uingereza kujitoa katika umoja huo.

https://p.dw.com/p/1HnS1
Brexit Symbolbild EU Flagge Union Jack Europäische Union
Picha: picture-alliance/dpa/R.Peters

Pande zote mbili zimeleezea kupigwa hatua kufuatia mazungumzo kati ya rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mwishoni mwa wiki. Rais wa Umoja wa Ulaya Tusk, ambaye yuko makini kuepusha kile kinachoitwa "Brexit", yaani kujitoa kwa Uingereza, alionya hata hivyo kuwa kulikuwa na masuala muhimu ya kutatua.

Makubaliano bado yana safari ndefu kufikiwa, wakati ambapo Cameron anahitaji kuwashawishi viongozi wenzake 27 katika Umoja wa Ulaya kuunga mkono mapendekezo yake ya mabadiliko, katika mkutano wa kilele utakaofanyika mjini Brussels kati ya Februari 18 na 19. Ikiwa atapata makubaliano, atapiga kampeni kwa Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya, wakati itakapopigwa kura ya maoni kuamua kujitoa au kubakia, ambayo huenda ifanyika mwezi Juni.

Jaribio la Uingereza kuufanyia mabadiliko uanachama wake katika Umoja wa Ulaya limeibua sintofahamu, likija wakati jumuiya hiyo ikipambana na mmiminiko mkubwa zaidi wa wahamiaji tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia, na madhara ya mgogoro wa madeni wa Umoja wa Ulaya. Tusk, waziri mkuu wa zamani wa Poland, alitarajiwa kuituma mipango hiyo kwa viongozi wakuu wa mataifa ya Umoja wa Ulaya mapema Jumanne, kabla ya kuyatoa kwa umma.

Donald Tusk (kushoto) na David Cameron mjini Brussels.
Donald Tusk (kushoto) na David Cameron mjini Brussels.Picha: Getty Images/AFP/E. Vidal

Hatua muhimu zimepigwa

Duru kutoka ofisi ya waziri mkuu wa Cameron katika mtaa wa Downing zilisema "hatua zimepigwa," na kuongeza kuwa kipindi cha majadiliano magumu kitaanza na mataifa yote wanachama kwa lengo kupata uungwaji mkono wa mapendekezo hayo yenye shauku kubwa.

Muswada wa mipango ya Tusk umejumlisha mfumo uliyoitwa "kadi nyekundu", ambao utaruhusu kundi la asilimia 55 ya mabunge ya kitaifa ya Umoja wa Ulaya kusitisha au kubadili sheria za Umoja wa Ulaya, suala ambalo lilikuwa moja ya malengo ya Cameron, kilisema chanzo kutoka ofisi yake.

Mfumo wa sasa wa "kadi ya njano" wa Umoja wa Ulaya -- ukitumia neno kutoka mchezo wa kandanda -- unayaruhusu tu mabunge kuomba maelezo kutoka Brussels. London ilionya huko nyuma kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya makubaliano ya mkutano wowote wa kilele kuwezekana kupatikana juu ya maeneo manne ya kisera ambayo Cameron anataka yafanyiwe mabadiliko.

Matakwa hayo yanajumlisha kuyalinda mataifa kama Uingereza ambayo siyo sehemu ya muungano wa safaru ya pamoja, kuhakikisha ushindani mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya, na kujitoa kwenye lengo la ushirikiano wa karibu zaidi. Lakini mabadiliko yenye utata zaidi yanahusu kuzuwia mafao kwa wafanyakazi wa Umoja wa Ulaya walioko nchini Uingereza, suala ambalo limeyaudhi hasa mataifa ya Ulaya ya Kati.

Ofisi ya Cemeron imesifu kile ilichokiita ishara za uhakika kutoka kwa Umoja wa Ulaya kuhusu makubaliano ya kile kinachoitwa "uzuwiaji wa mafao" ambao utaiwezesha London kuwatenga wahamiaji kutoka Umoja wa Ulaya katika mafao kama vile nyongeza ya mapato kwa wafanyakazi wenye kipato cha chini, ikiwa inaweza kuonyesha kwamba mfumo wake wa ustawi unakabiliw ana kitisho.

Picha ikionyesha taswira ya mjadala mkubwa juu ya hatma ya Uingereza katika EU.
Picha ikionyesha taswira ya mjadala mkubwa juu ya hatma ya Uingereza katika EU.Picha: picture-alliance/empics

Ufaransa yachora 'msitari mwekundu'

Ufaransa wakati huo huo, imeweka kile ilichokiita msitari mwekundu kwa kuionya Uingereza kuwa itazuwia pendekezo la ulinzi kwa mataifa yasiyo wanachama wa kanda ya sarafu ya euro ikiwa litakwenda mbali. Ingawa Cameron ameweka tarahe ya ya mwisho ya kufanyika kwa kura ya maoni mwishoni mwa mwaka 2017, na anasisitiza kuwa hana haraka ya kufikiwa kwa makualiano, duru zinasema yuko makini kufanikisha kura hiyo kufikia mwezi Juni. Magazeti ya Uingereza yaliripoti Jumatatu usiku kuwa huenda kura hiyo ikafanyika Juni 23.

Hilo litaepusha mlipuko mpya katika mgogoro wa wahamiaji wa Ulaya katika majira ya kiangazi mwaka huu, na kabla wapinzani wa Umoja wa Ulaya nchini Uingereza, na hasa katika chama cha Wahafidhina cha Cameron hawajachachama zaidi. Mkutano ujao wa kilele wa Umoja wa Ulaya utafanyika mwezi Machi, lakini hiyo inaweza kuwa imechelewa kwa maandalizi wa kura ya maoni mwezi Juni, ambapo tarehe nyingine inayowezekana katika kalenda ya uchaguzi ya Uingereza ni Septemba baada ya mapunziko ya kiangazi.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha mgawanyiko mkubwa juu ya iwapo Waingereza watapiga kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Hiyo itakuwa kura ya kwanza kabisaa ya umma juu ya uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya tangu mwaka 1975, miaka miwili baada ya nchi hiyo kujiunga na jumuiya ya kiuchumi ya Ulaya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri. Saumu Yusuf