1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa bunge kuhusu bajeti

Oumilkher Hamidou27 Novemba 2008

Ukaidi wa kansela Merkel na uamuzi wa China kuakhirisha mkutano wa kilele pamoja na Umoja wa Ulaya vyakosolewa

https://p.dw.com/p/G35Z
Kansela Merkel ahutubia bungeniPicha: AP



 Uamuzi wa China wa kutoshiriki katika mkutano wa kilele pamoja na umoja wa ulaya,mjadala wa bunge la shirikisho kuhusu mswaada wa bajeti ya mwaka 2009 na miradi tofauti ya kupalilia ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani na katika nchi za umoja wa Ulaya kwa jumla, ndizo mada zilizoshughulikiwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.


Tuanze na juhudi za kuimarisha uchumi.Gazeti la FRANKFURTER  RUNDSCHAU linaandika:



Kansela Angela Merkel na waziri wa fedha Peer Steinbrück watafanya yale yale waliyoyatetea bungeni wiki hii.Watawasilisha mpango wa kuinua uchumi wenye thamani ya dazeni ya mabilioni.Pingamizi za kawaida dhidi ya sera za kuinua ukuaji wa kiuchumi zinatafsiriwa kama maneno matupu tuu yaliyoshawishiwa kinadharia.Kinachoshauriwa na Merkel na Steinbrück hakihusiani lakini hata kidogo na mkakati wa kusawazisha mzozo.Kwanza waliwasilisha mpango ambao haujasaidia kitu.Baadae wakapinga mpango ulioshauriwa na wataalam na kukataa kurekebisha msimamo wao.Hatimae wameashiria uwezekano wa kuungama ifikapo january mwakani na kuwajibika zaidi.Kwanini Merkel na Steinbrück wanawafaanya watu wawe katika hali ya kutojua nini kitatokea?Vurumai yote hii ya nini?Linajiuliza Frankfurter Rundschau.


Gazeti la DIE  WELT linaandika:


"Katika mjadala wa jana bungeni kuhusu bajeti,kansela Angela Merkel ameshikilia hawana azma ya kuteremsha haraka kodi ya mapato.Sio FDP peke yao waliolalamika.CSU pia wamejipatia uwanja unaowatenganisha kinaga ubaga na kansela.Karata hizi zimeanzia mjini Bruxelles:Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,José Manuel Barroso anapigania pawepo mpango wa kuhimiza ukuaji wa kiuchumi wenye thhamani ya yuro bilioni 200-Mpango huo utabidi ugharimiwe kwa sehemu kubwa na nchi wanachama,kwa kupunguza kodi za mapato na ruzuku nyenginezo za mishahara.Merkel anajitokeza zaidi kama mwenyekiti wa chama cha CDU kuliko mkuu wa serikali,anapofanya ukaidi na kuendelea kusema kodi ya mapato itateremshwa baada ya uchaguzi mkuu mwakani.Vipi ahadi za uchaguzi za kuwapunguzia mzigo wananchi, zinaweza kuaminika,ikiwa serikali kuu ya muungano inayoongozwa na kansela wa kutoka chama cha CDU haizungumzii chochote kuhusu mpango huo?



Ni maoni ya gazeti la Die Welt.Sasa tunaumulika uamuzi wa jamahuri ya umma wa China wa kutoshiriki katika mkutano wa kilele pamoja na Umoja wa Ulaya.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:



Mapambano ya China dhidi ya Dalai Lama yanachukua sura nyengine kabisa.Kwamba matamshi makali yanatolewa kila wakati ambapo kiongozi huyo wa kidini wa Tibet anapo pokelewa katika sehemu yoyote ile ya dunia ni jambo moja,lakini ni jambo jengine kabisa,kuzuwia mkutano wa kilele usifanyike katika wakati huu ambapo mzozo wa fedha na uchumi unausumbua ulimwengu mzima-eti kwasababu hivi karibuni wanasiasa wa Ulaya wanapanga kukutana na Dalai Lama kwa mazungumzo.Mkutano huo wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Jamhuri ya China ungewavutia pia wachina bilioni moja nukta 3 ambao viongozi wa mjini Beijing wanapenda kuwataja.