1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Beijing kufunikwa na ukungu mzito

Admin.WagnerD8 Desemba 2015

China imetoa "tahadhari ya juu" kutokana na wingu la ukungu mzito linalotarajiwa kuufunika mji wa Beijing kwa takriban siku tatu kutokana na kiwango cha juu cha kuchafuka kwa hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/1HJ6o
China Smog in Peking
Uwanja wa Tiananmen ukionekana kufunikwa na ukunguPicha: picture-alliance/dpa/Jhphoto

Mawaziri kutoka nchi mbali mbali duniani wamezindua msukumo wa siku tano mjini Paris jana kutoa jibu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni "wito wa kihistoria" wa kupata makubaliano yatakayomnusuru binadamu dhidi ya maafa ya mabadiliko ya tabia nchi.

Mazungumzo ya Umoja wa Mataifa mjini Paris ya mabadiliko ya tabia nchi yanayohusisha nchi 195 yameelezwa kuwa ni fursa ya mwisho kuepusha madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi duniani , ikiwa ni pamoja na maafa kama ukame uliokithiri, mafuriko na vimbunga, pamoja na kupanda kwa maji ya bahari hali inayoweza kuvimeza visiwa pamoja na maeneo ya pwani yanayokaliwa na watu wengi.

Peking Autobahn Autos Stau China Smog
Magari mengi mjini Beijing husababisha uchafuzi wa hali ya hewaPicha: picture-alliance/dpa/S.Jun

"Fursa ya kupaaza sauti ya wito huo haipatikana kwa kila mtu ama kila siku," mkuu wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi wa Umoja wa Mataifa Christian Figueres aliwaambia waandishi habari katika mji mkuu wa Ufaransa Paris jana.

Matumaini yakufikia makubaliano

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia amewaonya wajumbe wa majadiliano , kwamba muda unakwenda mbio kuelekea maafa makubwa ya hali ya hewa", na amewataka kuweka kando mivutano yao na maridhiano yasiyo na tija ambayo yamedhoofisha kampeni za hapo kabla za Umoja wa Mataifa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

China Smog in Peking
Ukungu uliotanda mjini Beijing tarehe 08 Desemba 2015.Picha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Hata hivyo watayarishaji wa mazungumzo hayo mjini Paris wameonesha matumaini kwamba wanaweza kufikia makubaliano ifikapo mwishoni mwa juma, hata kama kuna ishara ndogo juu ya vipi tofauti kuhusu za upatikanaji wa fedha unaweza kutatuliwa.

Nchini China wingu zito la hewa yenye unyevunyevu ambayo inatarajiwa kuugubika mji wa Beijing kwa takriban siku tatu umesababisha serikali kutoa tahadhari ya juu leo wakati wakaazi wengi wamepuuzia tahadhari ya kupunguza muda wao wa kuwapo nje ya majumba yao.

Ukaguzi zaidi wa mazingira Beijing

Ilipofika mapema asubuhi leo(08.12.2015), mamia kwa maelfu ya watu , ikiwa ni pamoja na watoto, walikuwa wamejazana katika uwanja wa Tiananmen kuangalia sherehe za kupandishwa bendera. Redio ya taifa imesema baadhi ya watu wamepuuzia pia marufuku ya kutumia magari ambayo yana namba tasa za usajili.

Smog in Peking
Mkaazi wa jiji la Bejing akitumia kinga maalum dhidi ya ukungu mjini humoPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Waziri wa mazingira Chen Jining ameitisha kikao maalum jana usiku kuhimiza ukaguzi zaidi mjini Bejing pamoja na maeneo yake ya karibu ikiwa ni pamoja na Tianjian wakati akiongeza idadi ya vikundi vya ukaguzi wa mazingira hadi 12, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya serikali.

Watafiti wa China wamegundua kwamba uchafuzi wa mazingira kuwa ni chanzo kikuu cha ghasia nchini humo. Shirika la ulinzi wa mazingira la Greenpeace limesema , tahadhari ya kiwango cha juu, iliyotolewa ni ishara njema ya mwelekeo tofauti kutoka serikali ya mjini Beijing.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Yusuf Saumu