1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa kwanza Ujerumani wakaazi wake wazuiwa kutoka nje

Sekione Kitojo
20 Machi 2020

Mitaa haina watu na maeneo ya watu kukutana katika viwanja vya  wazi pia nayo yako tupu katika mji mdogo wa Mitterteich jimboni la Bavaria nchini Ujerumani, mji wa kwanza nchini humo kufungwa kabisa.

https://p.dw.com/p/3ZlUf
Deutschland Bayern, Mitterteich | Coronavirus | Ausgangssperre
Eneo la karibu na kanisa katika mji wa Mitterteich liko tupu, mahali ambapo watu wengi hukusanyika katika hali ya kawaidaPicha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Wakaazi  wake  wametakiwa  kubakia nyumbani kutokana  na  hali  inayozidi  kuwa  mbaya  ya  kusambaa kwa  virusi  vya  Corona. 

Wakaazi 6,500  wa  mji huo wamekatazwa  kutoka  majumbani mwao  bila  sababu  maalum, hali  ambayo  inaonekana  kuwa  ndio kitu  kinachokaribia  kutokea  kwa  nchi  nzima  ambako  watu  wengi wamekaidi  hatua  za  kubakia  nyumbani. Wakaazi  wa  mji  huo  wa Mitterteich, ulioko  katika  wilaya  ya  Tirschenreuth kusini  mwa jimbo  la  Bavaria , waliamka  leo wakishuhudia  aina  nyingine  ya maisha.

Coronavirus in München - menschenleerer Platz
Migahawa imefungwa , ama kufunguliwa kwa nyakati na huduma maalum jimboni BavariaPicha: Imago Images/Zuma/S. Babbar

Kwa mujibu  wa  mkuu  wa   wilaya  hiyo  Wolfgang Lippert , wakaazi wanaweza  kutoka  tu  majumbani  mwao  iwapo  wanakwenda  kazini , kumuona  daktari  ama  wanakwenda  kununua  mahitaji yao.

Lakini  pia  inaonekana  wakaazi  hao  wanaikubali  hali  hiyo. "Ni vizuri  kwamba  huu  ni  mji  wa  kwanza  kuwekewa  amri  hiyo  ya kutotembea  ovyo, na  ni  vizuri  kwamba inafanyika kwa  msisitizo mkubwa,"  mkaazi  wa  eneo  hilo Sandra Wedlich  amesema.

Hatua  hizo zimechukuliwa  baada  ya  mji  huo  wa  Mitterteich kujitokeza  kuwa  eneo  la  hatari  la  virusi  vya  Corona,  kwa  kuwa na  watu  karibu  40  ambao  wameambukizwa  virusi  hivyo  katika wilaya  ya  Tirschenreuth. Maafisa  wanaamini  kuwa  mengi  ya maambukizi  yanahusishwa  na  sherehe  za  hivi  karibuni  za unywaji  bia.

Symbolbild Schule zu Hause in der Corona-Krise
Watu wengi wametakiwa kufanyakazi majumbani mwaoPicha: picture-alliance/dpa/U. Perrey

Jimbo  la  Bavaria  ni  moja  kati  ya  majimbo  yaliyoathirika  kwa kiasi  kikubwa  nchini  Ujerumani, kwa  mujibu  wa  tarakimu  rasmi kutoka  katika  taasisi  ya  kupambana  na magonjwa  ya kuambukiza  ya  Robert Koch. Lakini  maambukizi  yanasambaa haraka  kwingineko, na  kusababisha  kansela  Angela  Merkel  kutoa wito kwa  wananchi  katika  hotuba  yake  kupitia  televisheni  siku ya  Jumatano  jioni  kuwa wapunguze mikusanyiko ya  kijamii.

Ujerumani  imeripoti  ongezeko  la  siku  moja  la  zaidi ya maambukizi 2,800  kufikia  jana, na  kufanya  idadi jumla  ya  watu walioambukizwa  virusi  vya  Corona  kufikia  10,000.

Waziri  wa  ulinzi  wa  Ujerumani  Annegret Kramp-Karrenbauer amesema  ikiwa  hali  itakuwa  mbaya  zaidi , basi  jeshi  litatumika katika  kupambana  na  virusi  hivyo  kutokana  na  kuwa  na  nyenzo stahili.

Deutschland Corona-Krise | Annegret Kramp-Karrenbauer
Annegret Kramp-Karrenbauer waziri wa ulinzi wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Sohn

"Wote tunatambua  kuwa  mapambano  dhidi  ya  virusi  vya  corona ni  ya  muda  mrefu. Mwishoni, tutatokeza  katika  barabara ndefu ambayo  itatupatia  njia  ya  kuwa  na vifaa. Hilo litakuwa  jukumu mahsusi la  jeshi  la  Ujerumani. Ndio sababu  bado  hatujachukua hatua  kama ilivyo kwa  huduma  nyingine  za  jamii kwa  wakati  huu. Hata  hivyo  tunajitayarisha  kwa  vifaa  na  ikitokea  kwamba huduma  za  kijamii zinafikia ukomo, jeshi  la  Ujerumani  na  vifaa vyake litakuwa  tayari."

Mipaka  imefungwa  nchini  Ujerumani  kuzuwia  janga  hili, wakati nchi  nzima  maduka  yamefungwa, migahawa imelazimika kufanyakazi  kwa  muda  maalum  na  watu  wametakiwa  kufanyakazi kutokea  nyumbani.