1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Lisbon,unaozifanyia marekebisho taasisi za umoja wa ulaya waanza kutumika tangu leo

Oumilkher Hamidou1 Desemba 2009

Umoja wa Ulaya wajipatia rais na waziri wa mambo ya nchi za nje-marekebisho yanayorahisisha shughuli za umoja huo katika daraja ya ndani na ya kimataifa

https://p.dw.com/p/Kmch
Rais na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya,kutoka kushoto;Herman van Rompuy na Catherine AshtonPicha: AP Graphics/DW

Mkataba wa Lisbon umeanza kufanya kazi kuanzia leo,kwa kukabidhiwa wadhifa wake rais wa kwanza wa Umoja wa Ulaya,Herman van Rompuy wa kutoka Ubeligiji na waziri wa mambo ya nchi za nje,bibi Catherine Ashton wa kutoka Uingereza.

Mkataba huo uliolengwa kurahisisha shughuli za Umoja wa Ulaya na muongozo wake ulimwenguni,"utaupatia madaraka ya kutosha kuweza kukabiliana na changamoto za siku za mbele na kujibu matakwa ya wananchi." amesema hayo mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,José Manuel Barroso.

La kwanza jipya lililotokana na mkataba huo wa Lisbon ni kubuniwa wadhifa wa kudumu wa rais wa baraza la ulaya(taasisi inayowaleta pamoja viongozi wa taifa na serikali ).Wadhifa huo amekabidhiwa Herman Van Rompuy wa kutoka Ubeligiji kwa muda wa miaka miwili na nusu.Hadi wakati huu wadhifa huo ulikua wa zamu kati ya nchi wanachama na kwa muda wa miezi sita.

Muengereza Catherine Ashton kwa upande wake ameteuliwa kushika wadhifa wa muakilishi mkuu anaeshughulikia siasa ya nje na usalama.Anashika nafasi iliyoachwa na Javier Solana baada ya kuongoza diplomasia ya Umoja wa Ulaya kwa miaka 10.Kinyume na Javier Solana lakini,mwanasiasa huyo wa kutoka Uengereza atasimamia taasisi yenye nguvu ya siasa ya nje itakayokua na watumishi maelfu kadhaa.

Sherehe fupi itakayoandaliwa na serikali ya Ureno,Sweeden ambayo ndio mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya na halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya,imepangwa kufanyika baadae leo usiku mjini Lisbonn,mji mkuu wa Ureno,kuadhimisha kuanza kufanya kazi mkataba huo mpya wa Umoja wa ulaya.

Mkataba huo umelengwa kurahisisha utaratibu wa kupitisha maamuzi na kupunguza nguvu za kura ya turufu katika Umoja wa ulaya wenye wanachama 27 na pengine 30 baadae pale mataifa ya balkan na Island yatakapojiunga na umoja huo.Unaimarisha pia madaraka ya bunge la Ulaya na mabunge ya kitaifa yatakayokua yakishauriwa mara kwa mara pamoja na kushadidiwa haki za kimsingi za Ulaya.

Abgeordnete im Europaparlament in Straßburg
Wabunge wa Ulaya mjini StrassburgPicha: picture-alliance/ dpa

Mbunge wa Ulaya kutoka chama cha SPD nchini Ujerumani Jo Leinen anasema:

""Bunge la ulaya ndio mshindi mmojawapo wa mkataba mpya wa mageuzi.Tutakua na haki sawa na serikali na baraza la mawaziri taasisi ambazo hadi wakati huu zilikua na nguvu kupita kiasi katika Umoja wa ulaya.Inamaanisha:Sheria zitakazopitishwa Brussels,zitaweza tuu kufanya kazi ikiwa bunge litaziidhinisha.Ikiwa baraza la umma litazikubali."

Umoja wa Ulaya kupitia mkataba mpya wa Lisbon utakua ukizungumza kwa sauti moja katika majukwaa ya kimataifa.

Miongoni mwa mepya yanayotokana na mkataba wa Lisbon ni pamoja na haki ya wananchi wa ulaya kuamua na haki ya nchi kujitoa katika umoja huo.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman