1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya Iraq wafanyika Paris

2 Juni 2015

Nchi wanachama wa muungano wa kijeshi dhidi ya kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu,IS zinakutana mjini Paris nchini Ufaransa kuijadili hali ya mambo nchini Iraq na Syria.

https://p.dw.com/p/1FaXd
Waziri wa nje wa Ujerumani akiwasili katika mkutano wa Paris dhidi ya IS
Waziri wa nje wa Ujerumani akiwasili katika mkutano wa Paris dhidi ya ISPicha: picture-alliance/dpa/J. Büttner

Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi amesema kusonga mbele kwa wapiganaji wa dola la Kiislamu kunaonyesha kushindwa kwa jumuiya ya Kimataifa,mtazamo ambao unazidi kuongeza mashaka kuhusu hali ya Iraq kabla ya mkutano kamili unaofanyika baadae leo ukiwakutanisha mawaziri kiasi ya 20 kutoka muungano wa kijeshi dhidi ya IS.

Mkutano huo wa leo umeongezwa uzito na tukio la shambulizi la bomu lililofanywa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga dhidi ya kituo cha polisi wa Iraq ambapo kiasi watu 37 waliuwawa na kuipunguza kasi operesheni ya kuukomboa mji wa Ramadi ulioko karibu na mji mkuu Baghadad.

Mkutano wa mjini Paris unatarajiwa kulijadili zaidi suala la mpango wa Iraq wa kuukomboa mji huo wa Ramadi kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani huku waziri mkuu wa Iraq al Abadi akitazamiwa kuweka wazi jinsi serikali yake ilivyopanga kuukomboa mji huo na ni kitu gani kinachoweza kufanywa na washirika kusaidia katika operesheni hiyo.

Na saa chache kabla ya mkutano wa Paris kuanza waziri mkuu huyo alisisitiza kwamba kundi la dola la Kiislamu sio tu ni tatizo la Iraq na Syria kwakuwa limeyadhibiti maeneo mengi ya nchi hizo lakini ni tatizo la ulimwengu kwa ujumla.

Abadi amesema wimbi la wapiganaji wa kigeni limeongezeka kuliko ilivyokuwa awali na hilo ni tatizo kwa ulimwengu kwa ujumla ambalo linabidi lichukuliwe hatua kutatuliwa. Kwa mujibu wa bwana Abadi kwasasa katika kila wapiganaji 10 wa IS kiasi 6 ndio wa Iraq na waliosalia ni wapiganaji kutoka mataifa ya kigeni na kutoka na mtazamo huo waziri mkuu huyo ameongeza kusema kundi hilo linaunda kizazi kipya cha wapiganaji ambao wamejitolewa na wako tayari kufa lakini sio washambuliaji wa kujitoa muhanga.

Halikadhalika Jumuiya ya Kimataifa imetakiwa ieleze ni kwanini magaidi wengi wanatokea Saudi Arabia,nchi za Ghuba,Misri,Syria na Uturuki pamoja na nchi za Ulaya?Pamoja na hayo waziri mkuu wa Iraq amekiri kwamba nchi yake inashindwa katika ujasusi ingawa inajaribu kwa hali zote pamoja na kwamba kundi la IS linauwezo wa Kimataifa.

Wapiganaji wa IS wameuteka mji wa Ramadi
Wapiganaji wa IS wameuteka mji wa RamadiPicha: picture-alliance/abaca/Balkis Press

Iraq imesema inahitaji haraka silaha na zana za kijeshi kupambana na IS na kuongeza kwamba mikataba mingi inayohusu silaha ilikuwa wameifunga na Urusi au Iran nchi ambazo zimewekewa vikwazo na nchi za Magharibi.Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wanasema lengo kubwa la mkutano wa baadae leo ni kumuunga mkono Abadi katika wakati huu ambapo anakabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa la kumtaka awajumuishe wasunni katika mapambano hayo dhidi ya IS.

Wakati huohuo ndani ya Iraq kwenyewe hali ya mambo haina dalili ya kuimarika.Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejiripua ndani ya gari lililokuwa limesheni mabomu katika kituo cha polisi na kuua kiasi watu 37 na zaidi ya 30 wamajeruhiwa katika mkoa wa Salaheddin:

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssessanga