1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu maji waingia siku ya pili mjini Stockholm

6 Septemba 2010

Hali inayoongezeka ya uchafuaji wa maji pamoja na kupungua kwa ubora wa maji duniani ni mada muhimu wakati wataalamu 2,500 kutoka duniani kote wanapoanza mkutano wao wa 20 wa wiki ya maji duniani mjini Stockholm

https://p.dw.com/p/P5AO
Nembo ya wiki ya maji mjini Stockholm

Kutokana na mabadiliko ya ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi, maji yanazidi kuchotwa, kutumika, na kurejewa tena kutumika, kusafishwa kwa madawa, na kumwagwa ovyo, watayarishaji wa mkutano huo wanaonya, katika utangulizi wa mkutano wa mwaka huu.

Ukuaji wa miji, kilimo, viwanda na mabadiliko ya hali ya hewa yanaongeza mbinyo katika ubora na upatikanaji wa maji, wameongeza watayarishaji wa mkutano huo katika taarifa yao. Mkutano huo, ambao ulianza rasmi jana Jumapili na unapangwa kuendelea hadi Septemba 11, unawajumuisha wataalamu kutoka karibu mataifa 130 duniani ili kujadili juu ya mada inayojulikana kama, "changamoto ya ubora wa maji, uzuwiaji, matumizi ya busara na kupunguza matumizi.

Hali si nzuri, kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya maji mjini Stockholm, ambayo ndiyo inayotayarisha mkutano huo kila mwaka. Uchafuaji wa maji unaongezeka duniani, taasisi hiyo imesema , na kudokeza kuwa kila siku, karibu tani milioni mbili za uchafu wa kinyesi cha binadamu unaingia katika mito, maziwa na bahari. Na katika nchi zinazoendelea , asilimia 70 ya uchafu wa viwandani unatupwa moja kwa moja katika maji bila ya kusafishwa, na kusababisha uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji yanayotumiwa na binadamu.

Ujoto duniani unalifanya tatizo hilo kuwa kubwa zaidi, kwa mujibu wa mkurugenzi wa wiki ya maji duniani, Jens Bergren.

Mabadiliko ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa yanahusika na maji na yanahusishwa na uchafuzi wa maji, ameeleza mkurugenzi huyo, akidokeza kuwa ongezeko la ujoto duniani linabadilisha mpangilio wa majira na kusababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya maeneo pamoja na ukame katika maeneo mengine.

Wasserknappheit in Afrika
Mwanamke wa Afrika Kusini akitoka kuchota maji ambayo si safi kwa kunywaPicha: AP

Hili ni tatizo kubwa kutokana na jinsi maji yanavyoweza kuchanganyika na vitu vinavyochafua. Iwapo kutakuwa na maji mengi, yanatoa zaidi nje vitu vinavyochafua, na kuvisambaza kote, lakini iwapo kunakuwa na ukame, maji yanakuwa pungufu katika mito na maziwa na kushindwa kuyeyusha vitu vinavyochafua na husababisha athari zaidi. Kwa njia zote kuna hali ya uchafuzi, amelamamika Bergren.

Ongezeko la uchafuzi kwa upande mwingine, linasababisha kuzuka kwa changamoto kadha na kuchangia katika upunguaji wa maji safi duniani, na kuathiri afya za watu, uhai anuai ardhini pamoja na majini. Shirika la umoja wa mataifa la chakula na kilimo, FAO, linakadiria kuwa katika muda wa miaka 15 ijayo, watu bilioni 1.8 watakuwa wanaishi katika nchi au maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji, na kwamba wakaazi karibu theluthi mbili duniani wanaweza kukabiliwa na uhaba huo.

Lakini pamoja na kuwa tatizo hilo ni kubwa , Bergren anasisitiza kuwa tatizo la uchafuzi na uhaba wa maji linaweza kutatuliwa. Hakuna kwa kweli uhaba halisi wa maji duniani, amesema, na kusisitiza kuwa, kwa kweli maji yapo ya kutosha. Kwa mujibu wa Bergren, tatizo ni jinsi maji hayo yanavyotumika, hilo ndilo tatizo kubwa, na hilo linawezekana kubadilishwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / AFPE

Mhariri: Josephat Charo