1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele juu ya amani ya Libya kufanyika Berlin

Amina Mjahid
16 Januari 2020

Jumuiya ya Ulaya inatarajia kuwa mkutano wa kutafuta amani ya Libya utakaofanyika wiki hii mjini Berlin, utaendeleza mchakato wa kisiasa kuelekea kusitisha mapigano katika nchi ya Libya inayokabiliwa na mzozo.

https://p.dw.com/p/3WHui
Bildkombo Haftar und as-Sarradsch

Ujerumani imeandaa mkutano wa kilele siku ya Jumapili kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, ambao unasimamia mashauriano juu ya kusaka suluhisho la amani juu ya mzozo wa Libya.

Waziri mkuu wa Libya anayetambuliwa kimataifa, Fayez al-Serraj, na kiongozi wa waasi Khalifa Haftar wamealikwa kwenye mkutano huo. Uingereza, Ufaransa, China, Falme za Kiarabu na Uturuki, na maafisa wakuu kutoka nchi kadhaa za Kiafrika na Kiarabu pia watahudhuria mkutano huo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema kuwa bado haikujulikana ikiwa viongozi hao wawili wa Libya kama wata hudhuria.

Jumuiya ya Ulaya itawakilishwa katika mazungumzo hayo ya Berlin na Rais wa Halmashauri ya Ulaya Charles Michel na mkuu wa sera za nje Josep Borrell, pamoja. Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa Jumapili.