1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

291110 Afrika EU Entwicklungshilfe

30 Novemba 2010

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika unamalizika leo mjini Tripoli Libya. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji imewasilisha mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano na bara la Afrika

https://p.dw.com/p/QLhO
Kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi, kulia, akisalimiana na rais wa baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy mjini Tripoli, Libya, Jumatatu Novemba 29, 2010.Picha: AP

Kwa Umoja wa Ulaya malengo ya maendeleo ya milenia yamepewa kipaumbele kikubwa na ndio kitovu cha ushirikiano wake na Afrika. Ushirikiano katika misaada ya maendeleo unatakiwa kuelekezwa katika sekta ya afya na elimu, pamoja na ujenzi wa miundombinu. Lengo la Umoja wa Ulaya ni kujenga mazingira yatakayofanikisha uwekezaji, biashara na kuunda nafasi mpya za ajira pamoja na washirika wake barani Afrika. Hizo ndizo mada ambazo zilipaswa kujadiliwa kwenye mkutano wa siku mbili kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika ulioanza jana (29.11.10) mjini Tripoli Libya, alisema Andris Pielbags, kamishna wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya.

"Ningesema mkutano huu wa kilele utatuwama zaidi juu ya uwekezaji. Hiyo ndiyo tofauti kubwa iliyopo kulinganisha na mkutano uliopita uliofanyika mjini Lisbon, Ureno. Mkutano wa Lisbon ulikuwa wa kisiasa."

Mazingira yamebadilika

Tangu mkutano wa pili kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mnamo mwaka 2007 mjini Lisbon, Ureno mazingira ya kimataifa yamebadilika. Kwa mtizamo wa makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika unatakiwa kuundwa upya. Hususan baada ya mzozo wa kimataifa wa kiuchumi mnamo mwaka 2008, uliozorotesha ukuaji wa kiuchumi barani Afrika. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la fedha la kimataifa, IMF, uchumi wa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ulikua kwa asilimia 2,5 mwaka jana 2009. Kiwango hicho kiko chini kwa pointi nne asilimia ikilinganishwa na ukuaji wa kiuchumi wa wastani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. (2004 - 2008)

Kwa upande mwingine jukumu la uongozi la bara la Ulaya katika bara la Afrika ambalo limekuwepo tangu jadi, sasa linakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa dola kuu mpya. Hususan China ambayo imejitanua kwa kujihusisha zaidi katika ujenzi wa barabara, madaraja na reli barani Afrika. Swali linalojitokeza ni, je Umoja wa Ulaya una kipi cha kutoa?

Andris Pielbags, kamishna wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya, amesema, "Nadhani barani Afrika hakuhitajiki tu miundombinu. Utawala bora, vita dhidi ya rushwa, haki za binadamu na demokrasia pia ni muhimu. Nadhani mfumo wa Ulaya ni imara kupitia demokrasia, haki za binadamu na uchumi wa masoko ya fedha."

Kwa maoni yake Elise Ford, mkuu wa ofisi ya shirika la Oxfam katika Umoja wa Ulaya, amesema umoja huo lazima uwe na msimamo imara kuhusiana na ahadi na kanuni zake.

"Kanuni ambazo zimewekwa na Umoja wa Ulaya kuhusu Afrika, zitasikilizwa kama umoja huo utazizingatia. Naamini huu ndio ufunguo wa kuhakikisha msaada unakuwa na manufaa zaidi. Kwani ni wazi kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuamuru unavyotaka barani Afrika kama ilivyokuwa hapo zamani."

Lengo mojawapo la mkutano uliopita kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mnamo mwaka 2007 mjini Lisbon lilikuwa kusaini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi. Azma ya mkataba huo ni kuifanya biashara iwe huru kati ya pande hizo mbili na kwa mujibu wa sheria za shirika la biashara la kimataifa, WTO. Kwani mkataba wa awali wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, eneo la Karibik na Pacifik, haukuzingatia tena sheria na shirika la WTO.

Misaada ya maendeleo yapewa kipaumbele

Kwa kuwa mazungumzo kuhusu mkataba wa kiuchumi hayajapiga hatua, Umoja wa Ulaya unajishughulisha zaidi za misaada ya maendeleo. Takriban asilimia 56 ya misaada yote ya maendeleo ulimwenguni inatoka katika Umoja wa Ulaya na nchi wanachama. Mwaka jana 2009 umoja huo ulitoa Euro bilioni 49 kama msaada wa maendeleo na unataka sasa kuhakikisha msaada wake unatumika vizuri.

Mjadala kuhusu msaada wa maendeleo bila shaka utakamilika baada ya mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na bara la Afrika unaofika kikomo hii leo mjini Tripoli, Libya.

Mwandishi:Correia da Silva , Guilherme (DW Portugiesisch)/Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraji