1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu umemalizika mjini Riyadh

Oummilkheir29 Machi 2007

Waarabu wawasihi waisrael wasiupuuze mkono wa amani waliowanyoshea

https://p.dw.com/p/CB50
Picha: AP

Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu waliokua wakikutana tangu jana mjini Riyadh wameyatolea mwito madola makuu yaunge mkono mpango wao wa amani ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa mashariki ya kati,chini ya misingi ya kubadilishana ardhi kwaajili ya amani.

Akihutubia sherehe za kuufunga mkutano huo wa kilele ulioanza jana,rais wa utawala wa andani wa Palastina Mahmoud Abbas ametahadharisha dhidi ya hatari ya kuzidi makali matumizi ya nguvu katika eneo hilo ikiwa Israel haitaupokea mkono wa amani waalionyoshewa na wapalastina.Rais Mahmoud Abbas ametoa mwito pia wa kuitishwa mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya mashariki ya kati.

“Tusiiache fursa hii kupita hivi hivi katika historia hii ndefu iliyojaa machungu“ Ameshadidia Mahmoud Abbas.

Maazimio yaliyopitishwa jana usiku na viongozi wa nchi za kiarabu,yakitanguliwa na lile linalohusiana na mpango wa amani pamoja na Israel yatatangazwa baadae hii leo wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saud Arabia,mwanamfalme Saoud el Faysal na katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Amr Mousa.

Katika taarifa ya mwisho iliyosomwa mwishoni mwa vikao vya leo,wajumbe mkutanoni wameunga mkono mpango wa“amani ya haki na jumla” kama mkakati wa kufuatwa na ulimwengu wa kiarabu unaoambatana na juhudi za amani za nchi za kiarabu chini ya misingi ya kubadilishana ardhi kwaajili ya amani.

Mpango wa amani wa nchi za kiarabu ulitajwa hapo awali na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon kua “mmojawapo wa mihimili ya utaratibu wa amani.”

Mpango huo wa amani ulioandaliwa miaka mitano iliyopita na aliyekua wakati ule mrithi wa kiti cha ufalme cha Saud Arabia, mfalme Abdallah unashauri kuanzishwa uhusiano wa kawaida pamoja na Israel kwa masharti dola hilo la kiyahudi linayahama maeneo yote inayoyakalia tangu mwaka 1967,kuundwa dola ya Palastina-Jerusalem Mashariki ukiwa mji mkuu na kupatikana ufumbuzi wa “haki na unaokubalika” kwa suala la wakimbizi wa kipalastina.

Israel imeshautia ila mpango huo.Ikiungwa mkono na mshirika wake mkubwa Marekani,Israel inasema inapendelea watu wajadiliane kabla ya masharti yoyote ya kufikia amani.

Mkutano wa kilele wa Riyadh umezungumzia pia suala la Irak.Katika hotuba yake rais Djalal Talibani ameahidi kuwapatia madaraka makubwa zaidi waumini wa madhehebu ya Sunni.Amewahimiza viongozi wa nchi za kiarabu wawasaidie kuuwavunja nguvu waasi na kuifutia Irak madeni yake.

Katika taarifa yao ya mwisho viongozi wa nchi za kiarabu wametahadharisha dhidi ya hatari ya itikadi kali ya kidini na kutoa mwito eneo la mashariki ya kati litakaswe na silaha za maangamizi.

Akifuata upepo huu mpya unaovuma mashariki ya kati, kansela Angela Merkel,ambae nchi yake ndio mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya anapanga kulitembelea eneo hilo kuanazia jumamosi ijayo.Baada ya Jordan ambako atakua na mazungumzo pamoja na mfalme Abdallah,kansela Merkel atakwenda pia Israel atakakokua na mazungumzo pamoja na waziri mkuu Ehud Olmert na baadae atakutana na rais mahmoud Abbas wa utawala wa ndani wa Palastina kabla ya kumalizia ziara yake nchini Libnan.