1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kujadili utoaji misaada ya kiutu

21 Mei 2016

Viongozi wa dunia pamoja na mashirika muhimu yasiyokuwa ya kiserikali NGOs wanakusanyika mjini Istanbul Jumatantu(23.05.2016) kwa mkutano wenye lengo la kujadili jinsi ya kushughulikia utoaji wa misaada ya kiutu.

https://p.dw.com/p/1IsAs
Türkei Edirne Flüchtlinge
Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki wamejipanga kupata chakulaPicha: picture-alliance/AA/B. Ozkan

Mkutano huo unasimamiwa na Umoja wa Mataifa na utaangalia jinsi ya kubadilisha hatua zinazochukuliwa na dunia katika mizozo licha ya kwamba kuna shaka mazungumzo hayo yataleta athari ndogo.

Türkei Syrische Flüchtlinge
Wakimbizi wa Syria nchini UturukiPicha: DW/A.L. Miller

Kukiwa na takriban watu wanaokadiriwa kufikia milioni 60 ambao wamekimbia makaazi yao duniani kote na mizozo na mabadiliko ya tabia nchi yakitishia kuleta kitisho zaidi, kuna makubaliano miongoni mwa serikali na mashirika ya kutoa misaada kwamba mfumo wa sasa wa utoaji misaada ya kiutu unahitajika kwa haraka sana kufanyiwa mabadiliko.

Lakini washiriki wa mkutano huo wa kilele watahitaji kuondoa shaka zilizojikita kuhusiana na uwezo wa mkutano huo kufikia malengo yake, na sio kuwa kama kijiwe kingine cha kimataifa cha kuzungumzia masuala ya ambayo hayapatiwi ufumbuzi.

Syrien Jordanien Grenze Flüchtlinge warten
Wakimbizi wa Syria katika mpaka kati ya Syria na LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Adayleh

MSF yajitoa

Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limejitoa katika mkutano huo, likihofia kuwa mkutano huo utakuwa hauna maana , kwasababu ya kukosa kuchukuliwa hatua na viongozi wa dunia.

Uchaguzi wa mji wa Istanbul ni ishara , kwa kuwa Uturuki yenyewe inawahifadhi kiasi ya wakimbizi milioni 2.7 kati ya wakimbizi wanaokadiriwa kufikia milioni 4.84 ambao wamekimbia mzozo nchini Syria.

Iwapo wajumbe watatoka nje kidogo ya vizuwizi vya usalama vinavyotengani eneo la fahari la mkutano huo , wataona nyuso zenye fadhaa za wakimbizi wa Syria wakiomba na kuuza bidhaa zenye thamani ya chini katika mitaa mingi ya Istanbul.

Afghanistan Ärzte ohne Grenzen Krankenhaus in Kundus
Hospitali inayoendeshwa na shirika la madaktari wasio na mipaka nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/AP Photo/N. Rahim

Lakini viongozi 60 duniani wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ikiwa ni pamoja na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan , kansela wa Ujerumani Angel Merkel na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon , washiriki wanamatumaini mkutano huo huenda ukawa mwanzo wa kufanya mabadiliko.

Matarajio

"Matarajio ya mkutano huwo taratibu yamepungua. Bado tuna hisia kwamba kuna hali ya nia njema katika mkutano huwo wa Istanbul. Pia tuna mawazo ya wastani kwa kile kinachoweza kufikiwa, " amesema Rob Williams, mtendaji mkuu wa asasi ya mtoto wa vita, ambayo inasaidia na kuwalinda watoto duniani kote walioathirika na mizozo.

Idadi ya watu duniani ambao wanatambua kwa dhati vipi mfumo wa utoaji misaada umeshindwa ni ndogo mno," ameliambia shirika la habari la AFP katika mahojiano ya simu.

Guinea MSF Ärzte ohne Grenzen Einsatz gegen Ebola
Madaktari wasio na mipaka wakitoa msaada wa matibabu kwa wagonjwa wa Ebola GuineaPicha: Amandine Colin/Ärzte ohne Grenzen

"Iwapo idadi hiyo ya watu itaongezeka wakati wa mkutano huo itakuwa bora zaidi. Lakini nafikiri tumo katika siku za mwanzo mwanzo kwa dunia kuwa wakweli."

Amesema mfumo wa sasa wa utoaji misaada ya kiutu "imeshindwa kuwasaidia watoto kwa kiwango kikubwa" na mkutano huwo unapaswa kuwa na makubaliano dhabiti kutoa adhabu kwa makosa ya kivita , kuimarisha elimu kwa watoto na kulinda hali yao katika makambi.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid