1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Ryadh

Oummilkheir28 Machi 2007

"Msingi wa ufumbuzi wa mzozo kati ya Palastina na Israel ni kuyahama Israel maeneo ya waarabu-"anasema katibu mkuu wa Umoja wa mataifa

https://p.dw.com/p/CHHH
Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarab Amr Musa
Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarab Amr MusaPicha: AP

Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu wameanza mkutano wao wa siku mbili hii leo mjini Ryadh kuzungumzia tena mpango wa amani pamoja na Israel-mpango walioupendekeza miaka mitano iliyopita –unaoangaliwa kama fursa bora,kama si ya mwisho ya kuutatua mzozo kati ya Israel na waarabu.

Viongozi takriban wote wa kiarabu,isipokua Muamar Ghaddafi wa Libya,wanahudhuria mkutano huo wa Ryadh .Lengo la mkutano huo ni kushadidia mpango wa amani uliokubaliwa mwaka 2002 mjini Bayrouth.

Akifungua mkutano huo mfalme Abdallah wa Saud Arabia amehimiza umoja na hali ya kuaminiana kati ya waarabu.Amekosoa vikali kile alichokiita kujiingiza Marekani “kinyume na sheria” nchini Irak pamoja na kuwepo vikosi vya kigeni nchini humo.Kuhusu Palastina mfalme Abdallah ametoa mwito wa kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya serikali ya umoja wa taifa iliyoundwa na Hamas na Fatah.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa jumuia za kimataifa walioalikwa mkutanoni mjini Riyadh.

Katika hotuba yake ya ufunguzi katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amelitaja eneo la mashariki ya kati kua ni eneo tete na la hatari kuliko wakati wowote ule mwengine. ”Katika ulimwengu wa kiarabu kidonda ambacho bado kinatona,hata baada ya kupita miaka 40 ni kule kukaliwa ardhi za waarabu na kukataliwa madai ya haki ya wapalastina ya kuwa na dola lao” amesema katibu mkuu huyo wa Umoja wa mataifa.

Amesisitiza tunanukuu:” msingi wa ufumbuzi unakutikana katika kuyahama Israel maeneo inayoyakalia tangu mwaka 1967 na kuundwa dola la Palastina jirani na Israel.”Mwisho wa kumnukuu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon.

Kabla ya hapo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa alizitembelea nchi kadhaa za mashariki ya kati,ikiwa ni pamoja na Israel ambako alitoa mwito wa kuzinagtiwa mpango wa amani ulioshauriwa na Saud Arabia katika mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mwaka 2002 mjini Bayrouth.

Mpango huo wa amani uliokubaliwa wakati ule na viongozi wa nchi za kiarabu ulikataliwa na Israel na kupuuzwa na Marekani pia.Israel inapinga vifungu vitatu vya mpango huo:kwabnza kuhusu kurejea nyuma hadi mipaka ya kabla ya vita vya mwaka 1967,kuwakabidhi wapalastina eneo la mashariki la Jerusalem na haki ya kurejea wakimbizi wa kipalastina katika maskani yao ya kabla ya vita vya mwaka 1948.

Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Amr Musa amewasihi viongozi wa Israel waukubali mpango huu kama msingi wa majadiliano badala ya kujaribu kuufanyia marekebisho.

“Tumefikia njia panda,ama tunafuata njia ya amani ya kweli au tunaingia katika njia ya mitihani” ameongeza kusema mwanasiasa huyo wa kutoka Misri.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Palastina Siad Abu Amr alisema hapo awali:

“Mpango wa amani wa nchi za kiarabu unaungwa mkono na kila mmoja na jumuia ya kimataifa pia sasa imeanza kuuzingatia.Hata waisrael wameanza kuzungumzia mema yaliyomo kuhusu mpango huo wa amani wan chi za kiarabu.Nnahisi ikiwa pande zinazohusika zimedhamiria kweli kufikia amani,basi mpango ni huu,mpango wa maana unaoweza kuleta amani,usalama, na utulivu kwa wote katika eneo hili.”

Rais wa utawala wa ndani wa palastina Mahmoud Abbas ameutaja mpango huo wa amani kua fursa ya mwisho kwa Israel kuishi katika “bahari ya amani”.

Wafuasi wa Hamas wamewaahidi viongozi wa Saud Arabia hawataupinga mpango huo wa amani,lakini wamewasihi viongozi wa kiarabu kwa upande wao wasiregeze kamba katika suala la haki ya kurejea nyumbani wakimbizi wa kipalastina waliofukuzwa tangu mwaka 1948.

Kikako cha ufunguzi kimeshamalizika na viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu wanatazamiwa kujadiliana kwa siri jioni ya leo kabla ya kukutana kwa karamu ya chakula cha usiku pamoja na mfalme Abdallah leo usiku.