1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Pakistan yaionya Taliban dhidi ya kuhifadhi magaidi

15 Julai 2023

Mkuu wa jeshi la Pakistan Jenerali Asim Munir ameuonya utawala wa Taliban dhidi ya kuhifadhi makundi ya wanamgambo ambayo yanapanga mashambulizi kwenye mipaka ya nchi hizo kutokea Afghanistan.

https://p.dw.com/p/4TwRM
Polisi wa Pakistan kwenye mafunzo ya kupambana na ugaidi
Polisi wa Pakistan kwenye mafunzo ya kupambana na ugaidiPicha: Fayaz Aziz/REUTERS

Jenerali Munir amesema jeshi lake litajibu vikali iwapo Taliban itashindwa kuwafichua wanamgambo hao.

Onyo hilo limetokea baada ya mashambulizi mawili wiki hii kusababisha vifo vya wanajeshi 12 wa Pakistan katika mkoa wa kusini magharibi wa Baluchistan, unaopakana na Afghanistan.

Utawala wa Taliban mjini Kabul haukujibu mara moja juu ya onyo hilo la mkuu wa jeshi la Paskitan.

Soma zaidi: Wakuu wa siasa, jeshi wajadili kitisho cha ugaidi Pakistan

Jenerali Munir amesema anatarajia utawala wa Taliban kutekeleza ahadi waliyotoa mnamo mwaka 2020 kufuatia mkataba na Marekani kwamba itazuia makundi ya kigaidi kutumia ardhi ya Afghanistan kupanga au kufanya mashambulizi.

Ameongeza kuwa Pakistan ina wasiwasi mkubwa ya kile alichokiita "maeneo salama na uhuru wa kufanya watakavyo" unaodaiwa kutolewa na Taliban kwa kundi la wanamgambo la Tehrik-e Taliban Pakistan TTP, linalojulikana zaidi kama Taliban ya Pakistan.