1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Stoltenberg: Kuchelewa msaada wa Marekani kunaiumiza Kyiv

Bruce Amani
15 Februari 2024

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami - NATO Jens Stoltenberg amesema leo kuwa kucheleweshwa kuuidhinisha msaada mpya wa Marekani kwa ajili ya Ukraine tayari kunaviumiza vikosi vya Ukraine vinavyopambana na Urusi.

https://p.dw.com/p/4cQxZ
Stoltenberg akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Stoltenberg akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken.Picha: Alex Wong/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami - NATO Jens Stoltenberg amesema leo kuwa kucheleweshwa kuuidhinisha msaada mpya wa Marekani kwa ajili ya Ukraine tayari kunaviumiza vikosi vya Ukraine vinavyopambana na Urusi.

Stoltenberg amewaambia waandishi wa habari kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO mjini Brussels kuwa anatarajia uamuzi kufanywa hivi karibuni.

"Tunaona kwamba msaada wetu unaleta mabadiliko, kwenye uwanja wa vita kila siku. Ni jana tu, Waukraine waliweza kuizamisha manowari ya wanamaji ya Urusi.

Soma pia: Scholz: Uamuzi wa EU unapaswa kuwa ishara pia kwa Putin

Na hii inadhihirisha ustadi na umahiri wa vikosi vya jeshi la Ukraine pia katika kufanya mashambulio makubwa katika maeneo ya Urusi. Ili kuhakikisha kuwa Ukraine inapata silaha na vifaa wanavyohitaji, tunahitaji kuongeza uzalishaji."

Makamanda wa Ukraine na maafisa wa nchi za Magharibi wamesema askari wa Kyiv wanazidiwa na mbinu na silaha za Urusi kwenye uwanja wa mapambano na wanalazimika kutumia silaha chache walizo nazo zikiwemo mifumo ya ulinzi wa angani.

Mawaziri wa ulinzi wa NATO wanajadili leo msaada wa muda mrefu kwa Ukraine na kuendelea na mazungumzo ya kutumia asilimia 2 ya patojumla la ndani kwa bajeti ya ulinzi.