1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnyamar: Ndege za Umoja wa Mataifa zaruhusiwa kupeleka msada

Mwakideu, Alex8 Mei 2008

Kinyume na ripoti za awali Marekani haijaruhusiwa kufikisha misaada yake Mnyamar

https://p.dw.com/p/Dwmc
Wafanyikazi katika uwanja wa ndege mjini Yangon wapokea misaada ya Umoja wa MataifaPicha: AP

Kinyume na ilivyoarifiwa awali, ndege ya msaada ya Marekani haijaruhusiwa kuingia Miyanmar ambako mamilioni ya wananchi walioachwa bila makao kufuatia kimbunga cha Nargis wanahitaji maji chakula na huduma za afya.


Hata hivyo ndege ya Umoja wa Mataifa imetua mjini Yangun ikiwa na misaada ya vyakula.


Balozi wa Marekani nchini Thailand Eric John amesema huenda kulikuwa na mchanganyiko wa taarifa kutoka kwa serikali ya kijeshi ya Miyanmar au labda serikali hiyo iligeuza kauli yake baadaye.


Ubalozi huo uliripoti mapema leo kwamba serikali ya kijeshi ya Miyanmar imeruhusu ndege ya Marekani ya msaada itue nchini humo.


John ameambia wanahabari kwamba Marekani bado ina imani wafanyikazi wake wa misaada wataruhusiwa kuingia Miyanmar ambayo ilikuwa inajulikana kama Burma.


Nchi hiyo imekuwa ikiwakabidhi vibali vya visa wafanyikazi wa misaada wanaoingia kutoka nje licha ya kukumbwa na janga la kimbunga cha Nargis.


Watu takriban 23,000 wamefariki kulingana na hesabu rasmi ya serikali hiyo. Hata hivyo mjumbe mmoja wa Marekani anasema huenda watu laki moja wamefariki.


Waziri wa maswala ya nchi za nje nchini Marekani Condoleezza Rice amesema janga la Miyanmar halipaswi kuchanganywa na siasa "hili linapaswa kuwa swala rahisi. Sio swala la siasa. Ni swala la kibinaadamu,na linapaswa kuwa swala ambapo serikali ya Burma inataka kuwaona watu wake wakipokea msaada ambao unaletwa kwa ajili yao” Rice amesema.


Lakini ndege za misaada za Umoja wa Mataifa zimeanza kuruhusiwa kuingia Miyanmar.


Msemaji wa shirika la chakula duniani WFP Paul Risley amesema ndege ya kwanza imewasili Miyanmar ikiwa na misaada ya vyakula na ndege zingine tatu zinatarajiwa kuwasili kwa shughuli yiyo hiyo.


Kimbunga cha Nargis kilivuma katika miji ya pwani na vijiji vilivyoko katika maeneo ya ukuzaji mchele ya Irrawaddy delta kusini magharibi mwa Yangun.


Kimbunga hicho kilichovuma jumamosi kimetajwa kuwa dhoruba kali zaidi barani Asia tangu mwaka wa 1991 wakati watu 143 elfu walifariki katika nchi jirani ya Bangladesh.


Walioshuhudia wanasema vijiji vimeharibiwa na manusura wengine wanaishi juu ya miti kwani mafuriko yameenea katika sehemu kubwa ya jimbo la Irrawaddy delta.


Msemaji katika afisi ya misaada ya Umoja wa Mataifa OCHA Richard Horsey anasema kuna takriban watu milioni moja wanahitaji msaada katika jimbo hilo lakini imekuwa ngumu kuufikisha msaada huo "kwa jumla eneo lote la chini la Delta liko chini ya maji. Hayo yamedhihirika kutokana na picha mpya kabisa za satilaiti. Na hii inaonyesha kweli changamoto zinazokabili kikosi hiki kinapojaribu kufikisha misaada ya dharura kwa umma unaouhitaji" Horsey amesema.


Misaada imekuwa ikiingia kutoka kwa nchi zingine jirani barani Asia.


Tailand, Japan, India, China, Singapore na Indonesia zimekuwa zikiingiza misaada nchini humo.


Akionge kwa niaba ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa; Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia misaada ya dharura John Holmes amesema "kutokana na hasara iliyotokana na janga hili, Katibu mkuu anaiomba serikali ya Miyanmar iruhusu misaada ya kimataifa kwa kuongoza shughuli ya kuwasili kwa misaada hiyo na kufanya kila njia iingie nchini humo. Hii inaweza kuisaidia serikali hiyo kukabiliana na janga hili vizuri zaidi"


Hasara iliyotokea Miyanmar nchi ambayo ilikuwa ikisafirisha mchele kwa wingi zaidi duniani, inazua hofu zaidi kwa tatizo la upungufu wa nafaka hiyo ulimwenguni.