1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Majeshi ya Uganda kushirikiana na Somalia

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLV

Majeshi ya Somalia na kikosi cha kulinga amani cha Umoja wa Afrika wanapanga kushirikiana ili kurejesha usalama na ustawi mjini Mogadishu.Hayo ni kwa mujibu wa serikali siku moja baada ya mashambulio ya makombora kusikika mjini humo katika kipindi cha majuma kadhaa.

Yapata watu watano wamepoteza maisha yao katika mapigano kati ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji wakati majeshi 370 ya Uganda yalipowasili mjini humo.Majeshi hayo yalishambuliwa kwa makombora mjini Mogadishu.Kwa upande wao serikali ya Somalia ina imani kuwa majeshi hayo ya kulinda amani ambayo bado yako katika uwanja wa ndege wa Mogadishu yataweza kuingia mtaani na kutekeleza majukumu yao.

Majeshi ya Somalia yakishirikiana na Ethiopia yamekuwa yakipambana na wanamgambo tangu kuwafurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu kutoka maeneo ya kusini na katikati mwa nchi hiyo mwezi Januari.

Hapo jana Wapiganaji waliojihami kwa silaha nzito walishambulia makao makuu ya zamani ya wizara ya ulinzi yanayotumika kama ngome ya majeshi ya Ethiopia.Shambulio hilo lilisababisha ulipizaji kisasi huku watu wawili wakipoteza maisha yao katika hospitali ya Medina na idadi kamili ya waliokufa kufikia watu watano na wengine 20 kujeruhiwa.

Majeshi zaidi ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani yanatarajiwa mjini humo katika kipindi cha siku chache zijazo huku vifaa vyao vikiwasili katika bandari ya Mogadishu.Ujumbe wa Umoja wa Afrika AU ni juhudi za kwanza za kimataifa za kudumisha amani nchini Somalia tangu ujumbe wa Marekani ulioungwa mkono na Umoja wa mataifa kutofanikiwa katika miaka ya 90.Kikosi hicho cha Umoja wa Afrika kinakabiliwa na uhaba wa pesa na vifaa.