1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mapigano mapya Mogadishu baada ya makubaliano kufikiwa

23 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGC

Mapigano mapya yanaripotiwa kuzuka mjini Mogadishu baada ya makubaliano ya muda ya kusitisha vita kufikiwa.Makubaliano hayo yalifikiwa kati ya majeshi ya Ethiopia na ukoo wa Hawiye.Yapata watu 24 wamepoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa wiki hii.Kulingana na wakazi wa eneo hilo hali ya wasiwasi imetanda kote mjini Mogadishu.Kikosi cha majeshi ya Uganda yako mjini humo kujaribu kulinda amani japo hakijaanza kushika doria kwenye barabara za miji.

Kulingana na msemaji wa jamii hiyo Ugas Abdi Dahir Mohammed ,jamii hiyo imekubaliana na jeshi la Ethiopia kusitisha vita baada ya mazungumzo.Makubaliano hayo aidha yanawahusisha majeshi ya serikali ya muda ya Somalia wanaotegemea ushirikiano wa jeshi la Ethiopia lilo na vifaa.

Hali inaripotiwa kuwa shwari hii leo mjini Mogadishu baada ya mapigano ya siku mbili yaliyosababisha vifo vya watu 24 na kujeruhi wengine kadhaa.

Maafisa wa kijeshi wa Ethiopia wanathibitisha kuwa mkutano kuhusu makubaliano hayo ulifanyika kwenye nyumba ya Abdi Hassan Qeybid,mbabe mmoja wa kivita.Hata hivyo hawakuthibitisha iwapo makubaliano ya kusitisha vita yamefikiwa.Hii ni mara ya kwanza kwa makubaliano ya aina hiyo kufikiwa kwa mujibu wa jamii hiyo ya Hawiye.

Somalia imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 91 baada ya Rais Siad Barre kungolewa madarakani.