1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mapigano mapya yazuka

10 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBaY

Yapata watu wane wameuawa hii leo nchini Somalia baada ya mapigano makali kuzuka mjini Mogadishu kati ya wapiganaji na jeshi la serikali linaloungwa mkono na jeshi la Ethiopia.

Kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP mjini humo mapigano hayo ni mabaya zaidi kutokea tangu mwezi Aprili wakati serikali ya muda ya Somalia ilipofurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu walioteka sehemu kadhaa za nchi.

Mapigano hayo yalianza katika eneo la kusini mwa Mogadishu wakati wa usiku na kudumu kwa muda wa saa moja.

Mapigano mabaya zaidi yalitokea katika kituo cha polisi cha Holwadag wakati wanamgambo waliposhambulia kwa makombora.

Mapigano mengine yameripotiwa karibu na kituo cha jeshi la Ethiopia mkoani Ali Kamin ambako mwili wa mtu mmoja ulipatikana.Zaidi ya wawakilishi alfu 1 wa koo za kisomali wanakutana mjini Mogadishu tangu Julai 15 katika mkutano wa maridhiano ya kitaifa unaofadhiliwa na serikali.Kundi la wapiganaji wanasusia kikao hicho na kupanga mkutano wao wenyewe mjini Asmara nchini Eritrea.Mkutano huo utafanyika mwezi ujao.