1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mlipuko watokea kwenye kambi ya kijeshi

28 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEq

Magari mawili yanaripotiwa kulipuka jana usiku katika mashambulizi yaliyotokea kwenye kambi ya majeshi ya Ethiopia mjini Mogadishu na kusababisha vifo vya mtu anayeshukiwa kuwa mlipuaji wa kujitolea muhanga vilevile dereva mmoja wa taxi. Kulingana na afisa mmoja wa jeshi la Ethiopia aliyethibitisha tukio hilo majeshi yake yalimzuia mlipuaji huyo wa kujitolea muhanga.

Shambulio hilo lilitokea katika eneo la Darmole nje ya mji wa Mogadishu. Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo dereva wa taxi aliyepoteza maisha yake hakuhusika na shambulio hilo lila alikuwa karibu na gari lililolipuka.

Majeshi ya serikali ya Somalia yalifunga sehemu ya barabara hiyo inayoelekea eneo la kaskazini la Puntland ili kufanya ukaguzi zaidi kufuatia shambulio hilo.

Makubaliano ya kusitisha vita yalifikiwa Ijumaa wiki iliyopita baada ya mashambulizi makali kutokea kwa kipindi cha wiki moja tangu majeshi ya Somalia yakishirikiana na ya Ethiopia kuwafurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu Disemba mwaka jana.

Hapo jana Ukoo wa Hawiye ulio na ushawishi mkubwa mjini Mogadishu uliiagiza serikali kuwaachia huru vbaadhi ya wapiganaji wake siku moja baada ya kuwaachia majeshi 18 ya serikali waliotekwa wiki jana katika mapigano.