1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogherini atunukiwa tuzo ya demokrasia

12 Novemba 2016

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya demokrasia mjini Bonn kwa mchango wake kwa demokarasia na amani duniani kote tuzo ambayo inatajwa kutuma ujumbe muhimu kwa wakati muafaka.

https://p.dw.com/p/2Sbgf
Vertreterin der Europäischen Union für Außen- und Sicherheitspolitik Federica Mogherini mit DW Intendant Peter Limbourg, 11.11.2016
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini na Mkuu wa DW Peter Limbourg.Picha: DW

Hafla ya kutunukiwa kwa tuzo hiyo imefanyika katika ukumbi wa jiji wa mji mkuu wa zamani wa Ujerumani ya magharibi Bonn hapo Ijumaa. Akizungumza na washiriki waliohudhuria hafla hiyo mkuu wa wakfu eenye kutowa Tuzo hiyo ya Kimataifa ya Demokrasia Jürgen Müller amesema kwamba Federica Mogherini amepaza sauti ya Umoja wa Ulaya katika siasa za dunia.Amesema mtizamo wake ulikuwa wa hisia na wakati huo huo ulikuwa na uthabiti jambo ambalo limemsaidia katika kueneza maadili ya Umoja wa Ulaya duniani na katika nchi zilizo jirani na umoja huo.

Mchango wa Mogherini katika kufikiwa kwa makubalino ya nyuklia na Iran ulikuwa ni sababu muhimu kwa nini wakfu wao umeamua kumtunukia tuzo hiyo.Müller pia amesema ameivutia wakfu huo kwa hatua yake ya kuunga mkono kwa nguvu uimarishaji wa misingi ya demokrasia na utawala wa sheria wakati wa mijadala kuhusu mzozo wa Ukraine.

Akipongeza juhudi hizo za Mogherini mkuu wa bunge la Ulaya Martin Schulz amesema "wakati maisha yetu yanapozidi kuelezewa na majanga,vita,sera kali za mrengo wa kulia na mara nyingi na hata na uongo na chukin ya wazi kazi ya Bibi.Mogherini inakuwa ya kupigiwa mfano kwa sababu ya juhudi zake bila ya kuchoka za kulinda maadili yetu ya Ulaya ya amani,demokrasia,haki za binaadamu na siasa za vyama vingi duniani."

Schulz ameongeza kusema kwamba mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amefanikiwa kuzifanya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zizidi kukaribiana katika wakati ambao Ulaya haiwezi tena kujificha nyuma ya mgongo wa kaka yeke mkubwa Marekani.

Umoja Ulaya yenye kujiamini zaidi

Vertreterin der Europäischen Union für Außen- und Sicherheitspolitik Federica Mogherini mit DW Intendant Peter Limbourg, 11.11.2016
Federica Mogherini mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.Picha: DW

Akizungumza na DW baada ya kupokea tuzo hiyo Mogherini amelitaja suala la kuchaguliwa kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump katika uchaguzi wa hivi karibuni.Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na Marekani kwa kusema kwamba ni kwa maslahi ya pande zote mbili kuendelea kushirikiana.Hata hivyo amesema yumkini kipau mbele cha sera za kiongozi huyo kikapelekea Marekani kujitenga sana na baadhi ya maadili ya msingi ya Ulaya.

Pia amezungumzia ishara alizotowa Trump za kutaka kuimarisha uhusiano na Russia kwa kusema kwamba sera ya Umoja wa Ulaya kwa Ukraine haiamuliwi mjini Washingoton yaliko makao makuu ya serikali ya Marekani na kwamba umoja huo utaendelea kutambuwa hatua ya Russia kulinyakuwa jimbo la Crimea kuwa sio halali.Pia ameupongeza utawala wa Obama kwa kuwa nao mazunguzo yenye tija katika miaka iliopita.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya pia ametangaza mipango ya usalama na ulinzi ya Umoja wa Ulaya kwa kusema kwamba haihusu uundaji wa jeshi bali mfumo wa ulinzi na usalama wa Ulaya utakoafanya kazi.Atawasilisha mipango madhubiti kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wakati watakapokutana hapo Jumatatu.

Tuzo ya kimataifa ya demokrasia ilianzishwa mwaka 2009 na hutunukiwa watu au mashirika yanayochangia katika masuala ya haki za binaadamu na maadili ya kidemokrasia.Mogherini ni mtunukiwa wa tano wa tuzo hiyo ambapo wengine ni pamoja na Rais wa zamani wa Jamhuri ya Czech Vaclav Havel, mwanasheria wa haki za binaadamu wa Iran Shirin Ebadi na shirika la maripota wasiokuwa na mipaka.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/DW/

Mhariri : Isaac Gamba