1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yapigwa marufuku na CAF

12 Novemba 2014

Morocco imetupwa nje ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2015 na kunyimwa kibali cha kuwa mwenyeji baada ya kukataa kuandaa kwa tarehe zilizopangwa mapema mwakani kwa sababu ya hofu ya Ebola

https://p.dw.com/p/1Dlgx
Marokkanische Fußballnationalmannschaft
Picha: AFP/Getty Images/F. Senna

Shirika la Kandanda Afrika – CAF limesema katika mkutano wa dharura unaoadaliwa katika makao yake makuu mjini Cairo, kuwa dimba hilo la Januari na Ferbauri sasa litakuwa na nchi nyingine mwenyeji ikiwa imesalia miezi miwili pekee tamasha hilo likianza.

CAF haijatangaza nchi itakayopewa kibali cha kuwa mwenyeji mpya, lakini limesema limepokea “maombi kadhaa”. Taarifa ya CAF imesema maombi hayo yanatathminiwa kwa sasa, na kamati kuu itakamilisha hivi karibuni uteuzi wa nchi itakayofanikiwa. Hata hivyo haikutaja majina yoyote ya nchi zinazotaka kuandaa.

CAF-Präsident Issa Hayatou in Marokko
Waziri wa michezo wa Morocco Mohamed OuzzinePicha: picture-alliance/AP Photo/Abdeljalil Bounhar

Afrika Kusini, Misri, Sudan na Ghana zote zimeonesha kuwa haziko tayari kuchukua nafasi ya Morocco, mojawapo ya sababu ikiwa ni kitisho cha Ebola. Nigeria, Angola na Gabon pia zimetajwa kama wawaniaji wanaoweza kuchukua nafasi hiyo.

Morocco ilikataa kuandaa mashindano hayo mnamo tarehe zilizopangwa za Januari 17 hadi Februari 8 kwa sababu ya kitisho cha Ebola. Ugonjwa huo hatari umewauwa watu zaidi ya 5,000 katika eneo la Afrika Magharibi, na Morocco ilitaka dimba hilo liahirishwe hadi Januari 2016 kwa sababu ya kitisho cha mashabiki wanaosafiri kuambukizana virusi hivyo. CAF inatathmini adhabu itakayoipa Morocco, na pia italazimika kupanga upya droo ya mwisho ya kinyang'anyiro hicho. Mashindano hayo yanayoendelea kwa sasa huenda yakaathirika kama nchi inayocheza kwa sasa katika mechi za kufuzu itapewa nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki katika mashindano hayo kama mwenyeji mpya. Morocco imesema ilichukua hatua hiyo kutokana na ushauri kutoka kwa maafisa wa afya.

Wakati huo huo, maandalizi ya mashindano ya FIFA ya Klabu Bingwa Ulimwenguni nchini Morocco mnamo mwezi Desemba yanaendelea na FIFA imesema kufikia sasa hakuna kitisho cha Ebola ambacho kinaweza kusababisha dimba hilo lifutuliwe mbali au liahirishwe.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman