1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Motlanthe ala kiapo cha kuilinda katiba

Kalyango Siraj25 Septemba 2008

Ana kibarua kigumu cha kuziba mgawanyiko ndani ya chama

https://p.dw.com/p/FP1F
Rais mpya wa Afrika kusini President Kgalema Motlanthe akila kiapoPicha: AP

Bunge la Afrika Kusini limemchagua makamu rais wa chama tawala cha ANC,Kgalema Motlanthe, kama rais wa tatu wa nchi hiyo baada ya kumalizika mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Kgalema Petras Motlanthe amechaguliwa na bunge la Afrika kusini kuwa rais wa nchi hiyo hadi uchaguzi mkuu utakaofanyika aidha Mwezi Aprili au Mei hapo mwakani.

Katika kikao cha bunge, kilichofanyika mjini Cape Town,Motlanthe alikusanya kura 269 kati ya kura zote 360 zilizopigwa.Kura 51 ziliharibika na mpinzani wake Joe Seremane wa chma cha upinzani cha Democratic Alliance kupata kura 50 tu.

Na baada ya matokeo ya kura kutangazwa mwanasheria mkuu Pius Langa alimtangaza kama rais rasmi wa nchi hiyo.Nae akala kiapo kama kiongozi wa taifa cha kuilinda katiba ya nchi.

Ni machache yanayojulikana kumhusu Motlanthe. Miongoni mwa hayo ni kuwa alizaliwa Julai 19,1949 katika mtaa moja ulio karibu na jiji la Johannesburg.

Inasemekana alijihusisha katika shughuli za kisaisa katika ujana wake baada ya kuvutiwa na siasa za kiongozi wa alieleta muamko miongoni mwa wausi wa Afrika kusini Steve Biko.

Mwaka mmoja baada ya matukio ya Soweto ya mwaka wa 1976,alikamatwa na kuwekwa ndani kwa kipindi cha miaka 10.Akiwa gerezani alipata nafasi kukutana na vigogo wa ANC kama vile Nelson Mandela pamoja na Walter Sisulu.

Baada ya kuachiliwa huru aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama kitaifa cha wachimba migodi.Wakati Cyril Ramaphosa alipoachia ngazi kama katibu mkuu wa ANC mwaka wa 1997,Motlanthe akachukua nafasi hiyo mara moja.

Katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama cha ANC uliofanyika Disemba mwaka wa 2007 ambapo Zuma alimbwaga Mbeki kama kiongozi wa chama,Motlanthe alijitokeza kama daraja kati ya kambi mbili za Zuma na Mbeki ndani ya chama hicho.

Kutokana na mchango wake huo wafuasi wa Zuma wakamzawadia nafasi ya naibu rais wa chama.

Wapinzani wanamchukuliaje kiongozi huyo mpya.Bi Hellen Zille ni mkuu wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance.nasema kuwa katika kambi ya Zuma,Motlanthe ndie afadhali japo sio bora kuliko watu wote nchini humo.

Uvumi umekuwa ukitanda kuwa Motlanthe ndie angechukua hatamu baada ya Zuma,ambae anakabiliwa na madai ya rushwa,ikiwa hataweza kuchukua urais.

Lakini yeye Motlnthe amekuwa akikanusha madai hayo akisema angependelea kuwa mwalimu aidha wa timu ya soka ya taifa ya Bafabafana au mwalimu wa siasa wa vijana wa chama cha ANC.