1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpalestina apondwa na gari la muisraeli-kusudi ?

3 Desemba 2009

Netanyahu kuonana leo na viongozi wa walowezi.

https://p.dw.com/p/KpUQ
Benjamin Netanyahu na George Mitchell (mpatanishi)Picha: AP

Wakati waziri-mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepangwa kuonana leo na viongozi wa walowezi wa kiyahudi waliokasirishwa na mpango wake wa kusimamisha kwa muda ujenzi wa majumba mapya ya walowezi hao huko Ukingo wa magharibi,kisa cha mpalestina cha kuponmdwa na gari kusudi tena na tena na muisraeli aliekasirika kwa chomwa kisu mkewe kimegonga vichwa vya habari mjini Jeruselem.

Kituo cha TV cha Israel cha kibiashara Channel 2, kilionesha jana picha za gari la Mercedes-Benz likimponda tena na tena ,mpalestina aliejeruhiwa baada ya kupigwa risasi na mwanajeshi wa Israel,dakika chache tu kabla. Awali, mpalestina huyo , aliwachoma kisu waisraeli 2 kabla kupigwa risasi na mwanajeshi wa Israel. Aliemponda kwa gari hilo, ni mume wa mmoja kati ya waisraeli hao 2 waliopigwa kisu.

Motokaa hiyo, inaoneshwa ikirudi nyuma na halafu kurejea mbele huku ikimponda mpalasetina huyo tena na tena kabla kuzuwiliwa dereva huyo na polisi.

Kwa muujibu wa kituo hicho cha TV ,dereva wa gari hilo, ni mume wa mwanamke aliepigwa kisu alhamisi ya wiki iliopita na mpalestina huyo alieshika kisu na shoka mkononi nje ya maskani ya wayahudi ya Kiryat Arba,karibu na Hebron, Ukingo wa magharibi.

Mpalestina anaonekana baadae akibururwa kutolewa chini ya mvungu wa gari hilo akiwa katika hali ya kuzimia. Alipelekwa hospitali ya Jeruselem ,ambako bado ni taabani.Polisi wa Israel, wamemtia nguvuni dereva wa gari hilo la Mercedes na kumweka kizuizini nyumbani mwake.Mshtaki wa serikali anapanga kumfungulia mashtaka kwa jaribio la kuua.

Jazba juu ya maskani za wayahudi zikiwa zimepanda tangu kwa walowezi hata kwa wapalestina, waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel, anatazamiwa kukutana leo na viongozi wa walowezi hao kuzungumzia uamuzi wa Baraza lake la mawaziri wa hivi karibuni kuzuwia kwa muda tu, ujenzi wa majumba mapya huko Ukingo wa magharibi.Hii ni kwa muujibu wa taarifa kutoka afisi ya waziri mkuu huyo.

"Waziri mkuu amewaalika viongozi wa maskani za Judea na samaria (Ukingo wa magharibi) kusikiliza manun'guniko yao na kuwaelezea uamuzi uliopitishwa."

-afisa wa afisi ya waziri mkuu huyo aliarifu.

Waziri mkuu Netanyahu alitangaza wiki iliopita , kuwa serikali yake inasimamisha ujenzi wa majumba mapya kwa kipindi cha miezi 10 huko Ukingo wa magharibi ikiwa ni njia ya kuwashawishi wapalestina kurudi katika meza ya mazungumzo.

Uamuzi huo lakini, umeukasirisha Uongozi wa waplaestina ambao unadai Israel , isimamishe moja kwa moja shughuli zake za ujenzi tangu Ukingo wa magharibi hata Jeruselem ya Mashariki kabla hawakurejea mezani kwa mazungumzo.

Netanyahu alikwisha jaribu kuwapoza moyo walowezi alipowaambia wiki hii kuwa, kusimamisha ujenzi huko ni kwa muda tu na kwamba, serikali yake itaruhusu tena ujenzi mara tu kipindi hicho cha miezi 10 kikimalizika.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman