1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpambe wa Dick Cheney akutikana na hatia ya kusema uwongo mahakamani

Oummilkheir7 Machi 2007

Eti kweli rais G-W. Bush ataaamuru asemehewe "Scooter" Libby?kashfa ya kufichuliwa siri za ikulu ya Marekani

https://p.dw.com/p/CHIo
Lewis Scooter Libby baada ya hukmu kutangazwa
Lewis Scooter Libby baada ya hukmu kutangazwaPicha: AP

Mkuu wa zamani wa ofisi ya makamo wa rais wa Marekani Dick Cheney,Lewis Libby anakabiliwa na hatari ya kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 25 jela kutokana na makosa ya kusema uwongo mahakamani na kukorofisha shughuli za idara ya sheria.

Rais George W. Bush na wapili wake Dick Cheney wamesema wamehuzunishwa na uamuzi wa korti dhidi ya mpambe wa makamo wa rais,lakini ikulu ya Marekani imekwepa kutoa taarifa ndefu kuhusu kisa hicho kinachohusishwa moja kwa moja na malumbano kuhusu vita vya Irak.

Hata hivyo msemaji wa ikulu ya Marekani,Dana Perino,amezisuta hoja kwamba hukmu dhidi ya Lewis Libby inaathiri moja kwa moja hadhi ambayo tokea hapo imeanza kuchujuuka ya utawala wa Marekani na makamo wake wa rais.

Dick Cheney ametoa taarifa ya mistari sita tuu,akisifu kazi ya mkuu wa zamani wa ofisi yake.

Ikulu ya Marekani inahisi hatia dhidi ya Libby imekutikana katika wakati ambapo uhalalifu na chanzo halisi cha vita vya Irak vinazidi kuwekewa suala la kuuliza .Msemaji wa ikulu Dana Perino amezisuta hata hivyo dhana eti rais George W. Bush huenda akaamuru asemehewe Libby,licha ya shinikizo la wademocrats kumtaka asipitishe uamuzi kama huo.

Wakili wake,Theodor Wells anataka kesi isikilizwe upya la sivyo watakata rufaa anasema: “Tunaamini,sawa na tulivyosema alipofunguliwa mashtaka,Scoloter hana hatia-hana hatia hata kidogo-na hajafanya lolote baya.Tutaendeleza mapambano yetu mpaka tunadhihirisha hana hatia.”

Lewis “Scooter” Libby amekutikana na hatia hapo jana katika mashtaka manne kati ya matano dhidi yake ikiwa ni pamoja na kukorofisha shughuli za mahakama,kutoa ushahidi wa uwongo mahakamani.

Mahakama itakutana tena June tano ijayo kuamua adhabu gani anastahiki kupewa.Anakabiliwa na hatari ya kufungwa hadi miaka 25 jela.

Anaandamwa katika kesi iliyofunguliwa kutaka kujua nani alitoa habari ambazo ni za siri kupita kiasi,zinazowakashif miongoni mwa wengineo,wale wanaokosoa vita nchini Irak.

Dhana kwamba siri hizo zimefichuliwa na mtu anaefanyakazi ikulu,zilizusha kashfa kubwa katika wakati ambapo hoja zilizotolewa za kuingia vitani nchini Irak zinazidi kutiliwa shaka.

Wademocrats,wanaodhibiti wingi wa viti katika baraza la Congress ,na ambao wamesimama kidete dhidi ya siasa ya rais Bush kuelekea Irak,wanasema Libby ametolewa mhanga tuu.Wanadai mhusika halisi ndani ya utawala wa Marekani afichuliwe ili ajieleze kwa kampeni ya kuzambaza habari za uwongo ili kuwachafulia sifa zao wapinzani wa vita vya Irak.

Kisa hiki kimeanzia July mwaka 2003 pale balozi wa zamani wa Marekani Joseph Wilson alipoutuhumu utawala wa rais Bush kutia chunvi katika suala la Irak kumiliki silaha za kinuklea..Vyombo vya habari wakati ule,vikinukuu duru za siri za ikulu ya marekani,vililitaja jina lka mkewe balozi huyo,Valerie Plame kua ni mtumishi wa shirika la ujasusi la CIA-katika wakati ambapo kufichuliwa jina la mtumishi wa idara ya upelelezi ni kitendo cha uhalifu nchini humo.