1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Brexit wa Theresa May wapata pigo jingine

Daniel Gakuba
19 Machi 2019

Mpango wa waziri mkuu wa Uingereza kuhusu Brexit umepata pigo jipya, baada ya spika wa bunge la nchi hiyo kutangaza kwamba hauwezi kupigiwa tena kura bungeni, isipokuwa pale utakapokuwa umefanyiwa marekebisho makubwa.

https://p.dw.com/p/3FHgx
Großbritannien Debatte zum Brexit im Unterhaus in London | John Bercow, Speaker
John Bercow, Spika wa Bunge la UingerezaPicha: picture-alliance/empics/House of Commons

 

Katika tangazo la kushtukiza jana jioni, Spika wa bunge la Uingereza John Bercow alisema wabunge hawawezi kuupigia kura mpango ule ule wa Brexit walioukataa awali katika msimu huu huu wa Bunge. Akitumia kigezo cha mwaka  1604, Spika huyo alisema itakuwa kinyume cha sheria kwa serikali kuwasilisha tena mpango uliokwishapingwa na wabunge.

Tangazo hilo la Spika Bercow limekuja wakati serikali ya Theresa May ikihangaika kuwashawishi wabunge kuukubali mpango huo wa Brexit ambao tayari wamekwishaubwaga mara mbili, ikitarajia kuwa ungepigiwa kura tena wiki hii.

Kuiwajibisha serikali

Bercow alitoa ufafanuzi kuhusu tangazo lake, akisema hataki lichukuliwe kama kauli ya mwisho kwenye mpango wa Brexit, bali kama sharti ambalo serikali inalazimika kulitimiza, ili yeye aweze kuandaa kura ya tatu bungeni kuamua juu ya mpango huo.

Waziri wa Brexit Steve Barclay akijibu tangazo la spika amesema hiyo inamaanisha kwamba yumkini hakutakuwa na upigaji kura wiki hii bungeni, na hiyo, ameongeza, inamaanisha kuwa Uingereza itachelewa kidogo kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

''Ni uamuzi muhimu, ambao bila shaka unahitaji kutazamwa kwa makini. Tutautafakari kwa kina na tutachukua uamuzi ipasavyo.'' Amesema Barclay.

Großbritanien | Theresa May spricht im Unterhaus | Brexit | London
Theresa May, waziri mkuu wa UingerezaPicha: Reuters/UK Parliament/J. Taylor

Chanzo kutoka katika serikali ya Bi Theresa May kimeliambia shirika la habari la AFP, kwamba hatua ya spika Bercow ni ishara kwamba anataka kuchelewesha Brexit kwa muda mrefu, ambapo bunge litachukua udhibiti wa mchakato mzima likinuia kufikia makubaliano laini na Umoja wa Ulaya.

Kiunzi kingine katika njia ya May kuelekea Brexit

Waziri Mkuu May alitazamia mpango wake ungeshinda kura ya tatu bungeni hapo kesho Jumatano, kabla ya kusafiri kwenda Brussels ambako ataomba kucheleweshwa kwa tarehe ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, hadi Juni 30 mwaka huu. Wabunge wengi wa chama cha Conservative ambao awali walipinga mpango wa Theresa May, walikuwa wameashiria kuukubali mara hii, kwa masharti mepesi.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama  wa Umoja wa Ulaya hapo jana walikubaliana na dhana ya kuipa Uingereza muda zaidi, ila walitilia shaka nia ya ucheleweshaji huo.

Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya amewaambia waandishi wa habari kuwa umoja huo unaweza kuridhia ombi la Uingereza kutaka muda zaidi wa mchakato wa Brexit, mradi ombi hilo liwasilishwe muda wowote kabla ya tarehe 29 Machi, na si baada ya saa tano usiku saa ya London.

Mwansheria mkuu wa Uingereza Robert Buckland amemkosoa vikali Spika wa bunge, akisema ameitumbukiza Uingereza katika mgogoro wa kikatiba.

afpe, rtre