1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Trump kuhusu Mashariki ya Kati: Dunia yatoa maoni

Daniel Gakuba
29 Januari 2020

Baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutangaza mpango wake wa amani kati ya Israel na Wapalestina, wadau mbali mbali duniani wametoa kauli zao, wengi wakiutilia mashaka. Wapalestina wameukataa kata kata mpango huo.

https://p.dw.com/p/3Wxo7
Westjordanland Mahmud Abbas | Reaktion auf Friedensplan von Donald Trump & Benjamin Netanjahu
Kiongozi wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas (katikati) akizungumza baada ya mpango wa Trump kutangazwaPicha: Reuters/R. Sawafta

Jana jioni, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mpango wake wa amani kati ya Israel na Wapalestina, akisimama bega kwa bega na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington.

Trump alisema mpango huo, ambao wachambuzi wanasema unajikita tu katika maslahi ya Israel, unaweza kuwa fursa ya mwisho kwa Wapalestina. Pande mbali mbali duniani zimekuwa zikitoa maoni kuhusu mpango huo.

Kama ilivyotarajiwa, Israel iliukaribisha kwa shangwe mpango huo wa Rais Donald Trump, huku waziri wake mkuu Benjamin Netanyahu akisema unakidhi mahitaji ya nchi yake. Mdau mwingine muhimu katika mpango huo, mamlaka ya Wapalestina, umeupinga vikali mpango huo wa Rais Trump, ikisema ni hila yake na Netanyahu, ambayo haitapiga hatua yoyote mbele.

USA Israel Donald Trump und Ministerpräsident Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani Donald Trump wakipongezana baada ya mpango wa Trump kutangazwa mjini Washington.Picha: picture-alliance/Consolidated News Photos/CNP/J. Lott

Miongoni mwa misingi ya mpango huo, makazi ya walowezi wa kiyahudi katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kimabavu yatatambuliwa kama himaya ya Israel, na mji wote wa Jerusalem utatambuliwa kuwa makao makuu ya Israel. Makaazi hayo ya walowezi, na ukaliaji wa Israel wa Jerusalem Mashariki ni kinyume na sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Wapalestina wasema ni njama dhidi yao.

Kiongozi wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas, akizungumza mbele ya maafisa wa chama cha Ukombozi wa Palestina PLO mjini Ramallah jana usiku, alisema Jerusalem na haki za Wapestina haviuzwi wala kujadiliwa, na kuwataka Wapalestina kuungana kuupinga mpango wa Rais Trump.

''Katika wakati huu mgumu, nawageukia Wapalestina wote kuwataka wasimame pamoja, na kupinga njama dhidi ya Palestina ili kufikia malengo ya kitaifa.'' Amesema Abbas na kuongeza, '' Mkakati wetu wa kupigana utaendelea ili kumaliza ukaliaji haramu, na kufikia kuundwa kwa taifa la Palestina, mji wake mkuu ukiwa Jerusalem.''

Gazastreifen Gaza City | Protest gegen Friedensplan Trump & Netanjahu
Wapalestina katika Ukanda wa Gaza waliandamana kupinga mpango wa amani wa rais TrumpPicha: Imago Images/ZUMA Press

Jumuiya ya kimataifa pia imekuwa ikitoa kauli yake kuhusu mpango huo wa Trump kuhusu amani ya Mashariki ya Kati. Jordan imesema mpango pekee wenye tija ni ule unaozingatia mipaka ya mwaka 1967 kati ya Israel na Palestina, ikaongeza lakini kuwa itakaribisha juhudi zenye nia njema ya kutafuta amani.

Tija itatokana na mpango uliojadiliwa na kukubaliwa na wadau

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas, amesema njia pekee ya kupata suluhisho la kudumu kati ya Israel na Wapalestina, ni kupata mpango uliojadiliwa na kukubaliwa na pande hizo mbili.

Ufaransa pia imesema amani katika mashariki ya kati itatokana na mpango unaozingatia sheria za kimataifa na kuheshimu mipaka iliyopo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake, amesema umoja huo utaendelea kuheshimu maazimio yaliyopitishwa na sheria za kimataifa kuhusu amani ya mashariki ya kati.

Michelle Dunne ambaye alikuwa mshauri wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu mashariki ya kati, amesema azma ya mpango huu wa Trump ni kujaribu kuunusuru mustakabali wa kisiasa wa waziri mkuu Netanyahu, na kumpatia Trump uungwaji mkono wa wapenzi wa Israel nchini Marekani katika uchaguzi mkuu ujao.

afpe, rtre