1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Uingereza wa Brexit waibua wasiwasi Umoja wa Ulaya

Lilian Mtono
7 Septemba 2020

Mkuu wa mazungumzo ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya ama Brexit Michel Barnier amesema masharti ya Brexit yaliyofikiwa kabla ya Uingereza kujitoa rasmi kwenye umoja huo ni lazima yaheshimiwe.

https://p.dw.com/p/3i6MQ
EU-Verhandlungsführer Michel Barnier
Picha: imago images/Le Pictorium/N. Landemard

Barnier ametoa matamshi hayo kufuatia ripoti kwamba London huenda ikaliomba bunge kukivunja kifungu muhimu cha makubaliano ya mazungumzo hayo.

Michel Barnier amenukuliwa na kituo cha redio cha nchini Ufaransa cha Inter Radio akisema kila kitu kilichosainiwa ni lazima kiheshimiwe. Alikuwa akijibu ripoti iliyochapichwa na gazeti la Financial Times kwamba waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alitaka kuyabadilisha makubaliano yaliyofikiwa kuhusiana na Ireland ya Kaskazini na msaada wa serikali.

Amesema, makubaliano kuhusiana na mustakabali wa Brexit hayakuwa mepesi, ingawa alikataa kuzungumzia zaidi kuhusiana na mpango huo wa Uingereza wa kukiuka baadhi ya vipengele vya makubaliano ya kujiondoa. Barnier amesisitiza kwamba wangependelea utulivu hadi mchakato huo utakapokamilika.

Hatua hiyo inaonekana pigo kubwa kwenye mazungumzo ya kibiashara ya baada ya Brexit yanayotarajiwa kurejea kesho Jumanne. Kulingana na gazeti hilo la Financial Times, muswada kuhusu soko la ndani ambao ulikuwa tayari kuchapishwa huenda ukavunja vifungu vya makubaliano ya Brexit.

Barnier, amesema iwapo hatua hiyo ya Uingereza itatekelezwa, ni wazi itahujumu makubaliano na kusababisha mgongano Ireland Kaskazini. Aliongeza kwamba makubaliano kuhusu Ireland Kaskazini yalikuwa muhimu katika kuhakikisha hakutakuwa na ofisi za forodha za mpaka kati ya Ireland na Ireland Kaskazini. Amekiri kwamba ana wasiwasi mkubwa.

Boris Johnson amesema nchi yake kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano  itakuwa ni matokeo mazuri kwa Uingereza.
Boris Johnson amesema nchi yake kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano itakuwa ni matokeo mazuri kwa Uingereza.Picha: Reuters/10 Downing Street/A. Parsons

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson hii leo amesema kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano kuhusiana na mustakabali wa kibiashara itakuwa ni matokeo mazuri kwa Uingereza, huku akionya kwamba serikali ya mjini London itaachana na mazungumzo hayo na Brussels, hadi pale makubaliano yatapofikiwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Johnson, anatarajiwa kusisitiza hii leo kwamba makuabaliano yoyote kuhusiana na mustakabali wa kibiashara yanatakiwa kuhitimishwa ifikapo Oktoba 15, hii ikiwa ni kulingana na ofisi yake ya Downing Street.

Amesema na hapa namnukuu, "iwapo hatutakubaliana hadi utakapofikia wakati huo, basi sioni iwapo tutafikia makubaliano ya kibiashara kati yetu na kwa pamoja ni lazima tukubaliane hilo na kusonga mbele”.

Johnson amesema iwapo hakutafikiwa makubaliano hayo, Uingereza itaanza kufanya biashara na Umoja wa Ulaya chini ya sheria za Shirika la kimataifa la biashara, WTO, kama Australia.

Waziri mkuu huyo pia amesema, wanataka kuliweka wazi hilo kwamba kama walivyosema kuanzia mwanzo kwamba hiyo itakuwa na matokeo mazuri kwa Uingereza.

Uingereza ilijiondoa rasmi kwenye Umoja wa Ulaya Januari mwaka huu na kuingia kwenye kipindi cha mpito hadi mwishoni mwa mwaka. Na katika kipindi hicho, bado ni mwanachama wa ushuru wa forodha na soko huria la Umoja wa Ulaya.