1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mporomoko wa daraja waua 39 Italia, lawama zaanza

Iddi Ssessanga
15 Agosti 2018

Wafanyakazi wa uokozi nchini Italia wamepata miili zaidi ya watu kutoka kwenye vifusi vya daraja la barabara kuu lililoporomoka Jumanne katika mji wa Genoa, na kufanya idadi jumla ya waliofariki katika mkasa huo kuwa 39.

https://p.dw.com/p/33Dth
Italien Genua | Einsturz Autobahnbrücke Morandi
Picha: Reuters/S. Rellandini

Magari kadhaa pamoja na malori matatu yalitumbukia urefu wa mita 45 kutoka juu baada ya kuporomoka kwa daraja hilo la Morandi, wakati ambapo familia nyingi za Kitaliano zilikuwa barabrani kuelekea mapumziko makubwa ya msimu wa kiangazi siku ya Jumatano. Daraja hilo liliporomoka kufuatia dhoruba kali.

Mamlaka ya ulinzi wa kiraia ilithibitisha Jumatano kuwa watu 39 wamefariki na 15 wamejeruhiwa, ambapo waziri wa mambo ya ndani Matteo Salvini amesema watoto watatu ni miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo.

Wakitumia zana nzito nzito, wafanyakazi wa uokozi wamekuwa wakipanda juu ya vifusi wakiwa na mbwa wa kunusa kuanzia usiku wa Jumanne hadi Jumatatu kutafuta manusura au miili ya wahanga.

Wakati huo huo, wachunguzi walikuwa wanajaribu kubaini kilichosababisha kipande cha urefu wa mita 80 cha barabara kuu kuvunjika kwenye daraja hilo lenye urefu wa juu wa mita 45 katika mji wa bandanri Genoa ulioko kaskazini-magharibi mwa Italia.

Watafutana uchawi

Wanasiasa wa Italia kwa upande wao, walikuwa wanatafuta nani wa kumlaumu kwa tukio hilo baya lililosababisha maafa. "Kila ninapofikiria kuhusu watu waliokufa Genoa, nazidi kupatwa na hasira," ameandika waziri Salvini kwenye ukurasa wake wa Twitter, na kuongeza kuwa wanaohusika na janga hilo watatajwa na watalipa gharama kubwa.

Italien Giuseppe Conte bei der eingestürzten Brücke Morandi in Genua
Waziri mkuu wa Italia Giueseppe Conte akiwasili kuzuru eneo lilipoporomoka daraja la Morandi, katika mji wa bandari wa Genoa, Italia, Agosti 14, 2018.Picha: Reuters/M. Pinca

Hisia hizo zimetiliwa mkazo pia na naibu waziri mkuu ambaye pia ni waziri wa ajira Luigi Di Maio

"Tatizo la kuporomoka linatokana na ukweli kwamba tunapolipa gharama za kutumia barabara, tunadhani kwamba pesa hizo zittumika kuwekeza katika uboreshaji wa madaraja ya barabara kuu. Usipowekeza katika uboreshaji na kutoa tu faida kwa wanahisa, ndivyo madara haya yanavyoporomoka," alisema Di Maio.

"Tuko hapa kusema kwamba tutapitia upya mikataba na tuko tayari kulipisha faini za hadi euro milioni 150, kwa sababu mbali ya hayo, kampuni hiyo ya Autostrade kuwa inamilikiwa na kampuni ya kifedha yenye makao yake nchini Luxembourg, lakini pia hawalipi kodi nchini Italia."

Kampuni ya Autostrade imesisitiza kuwa daraja hilo la Moradi lilikuwa linakaguliwa kila baada ya miezi mitatu kwa kutumia vifa vya kisasa zaidi, na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake waziri Matteo Salvini alikosoa sheria za nidhani ya bajeti za Umoja wa Ulaya, akihoji kuwa zinadhibiti uwezo wa Italia kuwekeza katika uboreshaji wa usalama wa barabara zake na majengo ya umma. Alitishia kukiuka vidhibiti vya Umoja wa Ulaya "vinavyotuzuwia kutumia fedha kwenye usalama wa shule wanakoenda watoto wetu au barabara na majengo ya umma.

Umoja wa Ulaya hauna usemi wa moja kwa moja juu ya matumizi ya usalama wa barabarani nchini Italia, lakini katika miaka ya karibuni umekabiliana na serikali mtawalia za nchi hiyo kuhusiana na kushindwa kwao kupunguza deni kubwa la taifa.

Italien Genua | Einsturz Autobahnbrücke Morandi | Rettungsarbeiten
Baadhi ya magari yaliotumbukia katika mporomoko wa daraja la Morandi mjini Genoa.Picha: Reuters/Italian Firefighters Press Office

Daraja lililochoka

Daraja la Moradi lilizinduliwa mwaka 1967 na lilikuwa linajulikana kwa wenyeji kama Daraja la Brooklyn. Watalaamu kadhaa wamelieleza kuwa mradi imara wa kiuhandishi lakini wenye kasoro nyingi. Miaka miwili iliyopita, profesa wa uhandisi katika chuo kikuu cha Genoa, Antonio Brencich, aliliita daraja hilo "kushindwa kwa uhandisi" kuliko na "gharama kubwa za uendeelezwaji."

Siku ya Jumatano, Brencich aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa daraja hilo lilikuwa kama gari chakavu linalohitaji marekebisho enedelevu, na "unapohitaji kuitengeneza gari mara kwa mara, unapaswa kununua tu mpya."

Hata hivyo Brencich alithibitisha kuwa daraja hilo lilikuwa linasimamiwa kwa umakini mkubwa, na kuongeza kuwa chanzo cha janga hilo huenda kisijulikane kabisaa.

Mwendesha mshitaka mkuu wa Geneo Francesco Cozzi, aliiambia televisheni ya taifa ya RAI kwamba atachunguza "kwa nini, na kwa nini kwa wakati huo" lilivunjika daraja hilo, na kusema ilikuw ani haraka mno kuzungumzia tukio lisilozuwilika.

Massimo Mantellini, mwanablogi na mwandishi habari, alisema uharaka wa kutoa lawama ni jambo la "kipumbavu", na kuitaka serikali ichukuwe tahadhari zaidi. "Waziri Toninelli tayari ametathmini hali, kupima uwajibikaji na kuweka adhabu juu ya wakosaji. Kila kitu kinakuwa chepesi hivyo unapokuwa mpumbavu," aliandika katika ujumbe wa Twitter.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, ape

Mhariri: Mohammed Abdulrahman.