1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

30 wauwawa Adamawa

18 Novemba 2015

Zaidi ya watu 30 wameuwawa kufuatia bomu lililoripuliwa kaskazini mashariki eneo ambalo kundi la itikadi kali la Boko Haram linaendesha hujuma zake. Shambulio hilo limetokea mji wa Yola mapema Jumatano

https://p.dw.com/p/1H7dU
Mojawapo ya mashambulio ya kujitoa muhanga ya Boko HaramPicha: Reuters

Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Nigeria la Premium Times zimesema shambulio la bomu katika mji wa Yola mapema hii leo limesababisha umwagikaji mkubwa wa damu katika mji huo unaokaliwa na kiasi watu 330,000.Kishindo kikubwa cha mripuko kilisikika katika mji wote na kusababisha taharuki.Watu zaidi ya 30 wameuwawa na wengine 80 wamejeruhiwa imesema ripoti ya gazeti jingine la Daily Trust ambalo limebaini idadi kamili ya waliouwawa ni watu 32 likiwanukuu maofisa ambao hawakujatwa majina. Mwandishi wa Dw wa idhaa ya hausa Muntaqa Ahiwa aliyefika eneo la tukio alizungumza na mtu mmoja aliyeshuhudia kilichotokea na kumueleza haya.

''Tulikuwa tunarudi kutoka kwenye eneo la kuegesha pikipiki ndipo tuliposikia milio ya miripuko mikubwa.Tulipofika eneo la tukio tuliona maiti za wasichana wachuuzi wa chakula na maji na pia tuliona maiti ya mwanamke wa kiigbo lakini binti yake mdogo aliyekuwa nae hakuumia pahala popote.Wahanga wa shambulio hilo walionekana kuumia huku viungo vikionekana kutawanyika kila sehemu ya tukio hilo.Binafsi nilijionea takriban maiti 30 wakati baadhi ya wengine walioumia nadhani walifia njiani kabla ya kufikishwa hospitali.''

Polisi katika jimbo hilo la Adamawa imesema waliouwawa hadi sasa ni watu 31 na kwamba bado iko katika kuchunguza ikiwa bomu lililoripuko lilitegwa au liliripuliwa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga. Kundi la kigaidi la Boko Haram linalokutikana zaidi katika eneo hilo pamoja na maeneo yanayopakana na Cameroon,Niger na Chad limekuwa likihusika na mashambulio ya mabomu kama hayo.

Wanajeshi wa Nigeria wakilinda mpaka wake na Niger
Wanajeshi wa Nigeria wakilinda mpaka wake na NigerPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Boko Haram ni kundi linalopigania kuanzisha dola lake litakaloendeshwa kwa misingi ya kile inachokiamini na kukitafsiri kuwa Sharia ya dini ya kiislamu katika eneo hilo. Mashambulizi pamoja hujuma zinazofanywa na kundi hilo zimesababisha kuuwawa takriban watu 14,000 tangu mwaka 2009.

Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita serikali ya Chad iliweka sheria ya hatari katika eneo zima la mto Chad ikisema eneo hilo limegeuka kuwa kituo cha mikutano ya wanamgambo wa Boko Haram. Katika mojawapo ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na kundi hilo katika nchi hiyo kiasi watu 41 waliuwawa baada ya mshambuliaji wa kujiwa muhanga kushambulia soko la kila wiki katika mji wa Baga Sola mnamo mwezi Oktoba.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpa/ap

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman