1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako wa bacar waendelea Nzouni

26 Machi 2008

Vikosi vya Comoro vikisaidiwa na vile vya Umoja wa Afrika vinaendelea na msako wa muasi M.Bacar Nzouni.

https://p.dw.com/p/DUp4

Siku moja baada ya kukivamia kisiwa cha Nzouani,vikosi vya jeshi la shirikisho la Comoro, vikishirikiana na vile vya Umoja wa Afrika, vonaendelea leo na safisha-safisha ya mabaki ya waasi na kumsaka kiongozi-muasi Mohammed Bacar kisiwani Nzouni.

Milio ya risasi ilisikika mapema asubuhi ya leo karibu na Ouani huku taarifa zikisema watu 3 walijeruhiwa leo na hivyo kufanya idadi ya raia waliojeruhiwa tangu kuanza opresheni hii hapo jana kufikia 8.Duru za serikali ya Comoro zinaarifu kwamba, idadi kubwa ya washirika wa Kanali Bacar wametiwa nguvuni.

►◄

"Vikosi vya muungano vimeingia Nzouani..... lakini huwezi kukidhibiti kisiwa kizima kwa muda wa saa 3"waziri wa ulinzi wa Comoro, Mohamed Bacar Dossar amenukuliwa kusema mjini Moroni.

Muandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa (AFP) amewaona wapiganaji wa kanali Bacar wakifunga utambi mwekundu-alama ya rangi ya bendera ya Nzouani katika bunduki zao.ilikua karibu na maskani ya kiongozi-muasi huko Barakani mapema hapo jana.

Majeshi ya Comoro na Umoja wa Afrika yanayojumuisha askari wa Tanzania na Sudan mwishoe yaliwatimua waasi katika vituo vyao na halafu kuliteka eneo hilo.

"naweza kuthibitisha kuwa kila kitu kimemalizika huko Barakani.Vikosi vyetu vimeingia katika Qasri ,wanajeshi wakalipekua qasri hilo,lakini Bacari hajakuwepo ."

Antoy Abdou kiongozi wa hadhi ya juu wa serikali ya Comoro alisema.

Qasri la Kanali Mohamed Bacar "Dar el Najah" huko Ouani,si mbali na mji mkuu Mutsamadu,lilikuwa tupu n a milango yake ilikuwa wazi haikufungwa.

vikundi vidogo vya wafuasi wa kanali Bacar, idadi yao ikikisiwa ni 400 kisiwani kote vilionesha upinzani kandoni mwa kituo chao cha usalama na katika ghala ya mafuta huko Amirosy si mbali na mji mkuu Mutsamadu.

Milio ya risasi ilisikika mapema hii leo karibu na Ouani huku mapambano yakiendelea.

Jumla ya raia 8 wamejeruhiwa-watatu hii leo.

Duru za serikali ya Comoro mjini Moroni, zinasema washirika wengi wa kanali Bacari wametiwa nguvuni.

Vikosi vya Comoro na vya Umoja wa Afrika vikijumuisha majeshi ya tanzania na Sudan, vilianza uvamizi wao uliosubiriwa kitambo mapema hapo jana katika mji mkuu wa nzouni-Mutsamadu na katika uwanja wa ndege na kukaribishwa mikono miwili na umati wa wakaazi wa mji huo.

Serikali ya shirikisho la visiwa vya Comoro ya rais Ahmed Abdullah Sambi imeahidi kuitisha uchaguzi haraka mara tu kanali Bacar ametimuliwa .Tangu kujitangazia uhuru hapo Julai, 1975,visiwa vya Comoro ambavyo asili ya jina lake "Qmara" au mwezi,havikujionea utulivu wa kisiasa.Vilijionea si chini ya majaribio 19 ya mapinduzi ya kijeshi.

Nzouni ni kisiwa cha pili kwa ukubwa baada ya Ngazija kikiwa na wakaazi 240,000 kikisafirisha n'gambo zao la ylang ylang.

Mayotte, kisiwa cha 4 cha Comoro kilibakia katika mamlaka ya Ufaransa pale rais Ahmed Abdullah alipotangaza uhuru.

juhudi za kukirejesha kisiwa hicho cha 4 katika shirikisho la Comoro hadi sasa zimeshindwa. Kila kisiwa -Ngazija-kikubwa kati ya vyote,Nzouani na Moheli-kidogo kabisa,kina kiongozi wake chini ya mfumo wa shirikisho .

Kanali Bacar, mwenye umri wa miaka 45 alichaguliwa rais wa kisiwa cha Nzouani 2002 na akachaguliwa tena Juni, 2007 katika uchaguzi wa kutatanisha uliotangazwa si halali na rais wa shirikisho Ahmed Sambi na pia haukutambuliwa na Umoja wa Afrika.

Kuanzia hapo kanali Bacar amekuwa akitawala nzouni kama kisiwa kilichojitenga na shirikisho la visiwa vya Comoro hadi jana.