1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshindi wa Ballon d'Or kujulikana Jumatatu

Sekione Kitojo
3 Desemba 2018

Mshindi wa kiatu cha dhahabu Ballon d'Or atajulikana usiku wa Jumatatu , na anayetarajiwa kushinda ni Luka Modric

https://p.dw.com/p/39NH4
Schweiz, Ballon d'Or 2015
Picha: Reuters/A. Wiegmann

Mshindi  wa  kiatu  cha  dhahabu  Ballon d'Or mwaka  2018 atapatikana  katika  sherhe  itakayofanyika  mjini  Paris leo Jumatatu usiku, ambapo Luka  Modric  wa  Croatia  pamoja  na wachezaji  kadhaa  wa  kikosi  kilichoibuka  mshindi  katika  kombe la  dunia  cha  Ufaransa  wakitaraji  hatimaye  kufikisha  mwisho miaka  10  ya  ushindi  wa  Cristiano Ronaldo  na  Lionel Messi.

Schweiz, Lionel Messi Nominierter für den Fußballer des Jahres 2015
Lionel Messi bingwa wa tuzo hiyo mara tano kutoka Barcelona ya UhispaniaPicha: Getty Images/P. Schmidli

Wachezaji  sita wa  kikosi  cha  Ufaransa  ni  miongoni  mwa wachezaji 30 walioteuliwa kwa  ajili  ya  tuzo  hiyo ambayo inatayarishwa  na  jarida  la  michezo  la  Ufaransa na  kupigiwa  kura na  waandishi  habari  180 duniani  kote.  Miongoni  mwao  ni pamoja  na  Kylian Mbappe, Antoine Griezmann , Raphael Varane, Hugo Lloris, Paul Pogba  na  N'Golo Kante.

CL- Auslosung | Krönung von Luka Modric zum Europas Fußballer des Jahres in Monaco
Luka Modric akikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya Picha: Getty Images/AFP/V. Vache

Na kwa  upande  wa  shirikisho  la  kandanda  barani  Ulaya, limeidhinisha  kuundwa  kwa  mashindano  ya  tatu  ya  UEFA  ya vilabu  jana  Jumapili, mashindano  ambayo  yatakuwa  katika mfumo  kama  Champions League  ya  sasa  pamoja  na  Ligi  ya Ulaya, Europa  League kuanzia  mwaka  2021.

Katika  mkutano  wao mjini  Dublin , kamati  kuu  ya  UEFA ilikamilisha  mipango ya kuanzisha mashindano  hayo, kwa  jina  la  UEL2 na  yatahusisha timu 32 katika  awamu  ya  makundi ,  katika  msimu  wa  2021 hadi 2024.

Fußballer Cristiano Ronaldo
Mshambuliaji wa Ureno na Juventus Turin Cristiano Ronaldo ambaye alishinda Ballon d'Or mara tanoPicha: picture-alliance/dpa/E. Leanza

Katika  bara  la  Afrika , klabu  ya  Morocco  ya  Raja  Casablanca imefikisha  mwisho  miaka  15  ya  kusubiri  kunyakua  taji  la  bara la  Afrika kwa  kushinda  kombe  la  CAF  la  shirikisho katika  jamhuri ya  kidemokrasi  ya  Congo  jana  Jumapili  licha  ya  kufungwa mabao 3-1  katika  mkondo  wa  pili  wa  fainali  dhidi  ya  V Club  ya Congo.  Raja  ambayo  ilishinda  mara  ya  mwisho  kombe  hilo mwaka  2003, iliishinda  V Club  kwa  mabao 3-0 katika  mchezo  wa mkondo  wa  kwanza  mjini  Casablanca Jumapili  iliyopita  na kufanikiwa  kulinyakua  kombe  hilo  kwa  jumla  ya  mabao 4-3 katika  michuano  ya  mikondo  miwili  ya  fainali.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / dpae / rtre / ape

Mhariri: Mohammed Khelef