1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshirika wa Trump ahukumiwa kifungo cha miezi 47 jela

Amina Mjahid
8 Machi 2019

Paul Manafort, amehukumiwa kifungo cha takriban miaka 4 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukwepa kulipa kodi na udanganyifu wa kibenki unaohusiana na kazi yake ya kuwashauri wanasiasa wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/3EfGE
USA Alexandria - Hohe Haftstrafe für Trumps Ex-Wahlkampfmanager Manafort
Picha: picture-alliance/AP/D. Verkouteren

Mwenyekiti wa zamani wa kampeni ya Rais Donald Trump wa Marekani, Paul Manafort, aliyekuwa amekaa katika kiti cha walemavu kutokana na kuumwa na goti, hakuonesha hisia zozote wakati aliposikia hukumu yake ya miezi 47 jela.

Licha ya kuwa hii ni hukumu kubwa zaidi kutokana na uchunguzi wa Mchunguzi Maalum Robert Mueller, lakini inatajwa pia kuwa ya afadhali kulingana na uzito wa hatia dhidi yake.

Miongozo ya hukumu kama hiyo inaonesha kwamba Manafort aliye na miaka 69 angepaswa kufungwa miaka 20 au hata kifungo cha maisha. Manafort alikuwa gerezani kuanzia mwezi Juni mwaka jana kwa hiyo kifungo chake kitapungua kwa miezi hiyo 9, lakini bado anakabiliwa na uwezekano wa kuongezewa hukumu kutokana na kukabiliwa na kesi nyengine tofauti katika Wilaya ya Columbia ambako amekiri makosa ya kufanya ushawishi kinyume cha sheria.

Akiwa mbele ya Jaji T.S. Ellis, mwenyekiti huyo wa zamani wa kampeni ya Rais Trump alisema kutamka kuwa anajisikia aibu na fadhaa pekee hakuwezi kuelezea anavyojisikia. Hata hivyo, Manafort hakuomba msamaha wa aina yoyote.

Wakili wa Manafort asema mteja wake amewajibika

USA Alexandria Rechtsanwalt Kevin Downing nach Manafort Urteil
Wakili wa Paul Manafort Kevin Downing akizungumza na waandishi habari katika jimbo la VirginiaPicha: Reuters/J. Young

Akizungumza na waandishi habari waliokuwa nje ya mahakama, wakili wa Manafort, Kevin Downing, alisema mteja wake amewajibika. "Kitu muhimu mulichokiona leo ni kile ambacho tumekuwa tukikisema kutoka siku ya mwanzo, hakuna ushahidi wa aina yoyote kuwa Paul Manafort alishirikiana na maafisa wowote wa serikali kutoka Urusi," alisema Kevin Downing.

Manafort aliongoza kampeni za urais za Trump wakati wa miezi muhimu ya kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2016, huku Urusi ikidaiwa kuuingilia uchaguzi huo kwa kwa kufanya udukuzi dhidi ya akaunti za barua pepe za wanachama wa Democrats.

Paul Manafort alikuwa miongoni mwa watu wa karibu wa Trump walioshitakiwa na kuanza kuchunguzwa na tume maalum ya Robert Mueller na hadi sasa amekuwa mshitakiwa wa cheo cha juu kabisa kutupwa jela. Hata hivyo, mashitaka haya yaliyomtia hatiani Manafort hayahusiani na kazi yake katika kampeni ya urais ya mwaka 2016, ambapo Mueller alikuwa akichunguza kuona iwapo kampeni ya Trump ilifungamanishwa na Urusi. 

Mwaka jana, jopo la majaji lilimtia hatiani Manafort kwa makosa manane, yakiwemo ya kuficha taarifa za mamilioni ya dola alizopata kutokana na kazi zake nchini Ukraine.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Mohammed Khelef