1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa mauaji ya New Zealand afikishwa mahakamani

Sylvia Mwehozi
16 Machi 2019

Raia wa Australia Brenton Harrison amefikishwa mahakamani Jumamosi nchini New Zealand kujibu tuhuma za mauaji kuhusiana na shambulio la ijumaa katika mji wa Christchurch ambapo watu 49 waliuwawa kwenye misikiti miwili.

https://p.dw.com/p/3FAhw
Neuseeland | Anschlag von Christchurch | Brenton Tarrant
Picha: Reuters/M. Mitchell

Akiwa amefungwa pingu alisimama kimya mbele ya mahakama ya wilaya ya Christ church kabla ya baadae kurejeshwa rumande bila kujibu lolote.

Mshukiwa huyo atarejea tena mahakamani mnamo April 5 na polisi imesema mashatka dhidi yake yanaweza kuongezeka.

Shambulio la Christchurch ambalo waziri mkuu wa New Zealand amelitaja kuwa la kigaidi ndiyo baya kabisa katika historia ya nchi hiyo na limeongeza kitisho cha usalama katika kiwango cha juu.

Mwanaume mmoja aliyekuwamo katika msikiti wa Al Noor na kunusurika amesimulia kisa hicho akisema mshambuliaji aliingia msikitini wakati walipokuwa katikati ya swala.

"Aliingia na kuanza kushambulia kila mtu aliyekuwamo ndani, kila mahali!", alisema Ahmed Al-Mahmoud, aliyefanikiwa kupenya sambamba na wengine baada ya kuvunja kioo cha dirisha.

Huzuni, waziri mkuu Ardern aungana na waombolezaji

Neuseeland | Anschlag von Christchurch | Gedenken
Waombolezaji wakiweka maua katika eneo la kumbukumbu Picha: picture-alliance/AA/P. Adones

Waombolezaji nchini humo wamewasha mishumaa na kuweka maua katika eneo la kumbukumbu lililowekwa mjini Christchurch. Baadhi ya waombolezaji wameonekana wakiwafariji jirani zao na wengine wakisimama kimya eneo la karibu na misikiti iliyoshambuliwa.

Shughuli ya mazishi imepangwa kufanyika Jumamosi (16.03.2019). Waziri mkuu Jacinda Ardern aliungana na jamii ya Waislamu katika kituo cha wakimbizi mjini Christchurch akisema atahakikisha uhuru wa kuabudu nchini New Zealand. "Ninatoa ujumbe wa upendo na mshikamano kwa niaba ya New Zealand kwenu nyote", alisema Waziri mkuu akiwa amefunika kichwa chake na ushungi mweusi.

Waathirika wengi wa mkasa huo ni wakimbizi na wahamiaji kutoka nchi za Pakistan, India, Malaysia, Indonesia, Uturuki, Somalia na Afghanistan. Waislamu ni asilimia moja ya wakaazi jumla wa New Zealand.

Sheria ya kudhibiti silaha

Waziri mkuu Ardern ameahidi kufanya marekebisho ya sheria ya umiliki wa silaha akisema mshukiwa Tarrant alikuwa na kibali cha kumiliki silaha na alitumia silaha tano. "Ninaweza kuwaeleza jambo moja, sheria zetu za umiliki wa silaha zitabadilika", Ardern aliwaeleza waandishi wa habari.

Nchi hiyo tangu kipindi cha nyuma ilijaribu kudhibiti sheria za umiliki wa silaha. Na kwa mujibu wa takwimu nchini New Zealand kunakadiriwa kuwepo na silaha milioni 1.5 katika taifa lenye wakaazi milioni 5, lakini hata hivyo New Zealand ina kiwango kidogo cha machafuko ya silaha.

Neuseeland | Anschlag von Christchurch | Jacinda Ardern
Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda ArdernPicha: Getty Images/M. Tantrum

Tarrant ambaye ni mzaliwa wa Australia aliishi kwenye kisiwa cha kusini cha New Zealand ana alikuwa ni mwanachama wa klabu ya bunduki ya Bruce, kulingana na ripoti za vyombo vya habari ambavyo vilinukuu wanachama wa klabu hiyo waliosema alikuwa akifanya mazoezi ya kulenga shabaha.

Ulimwengu walaani shambulio

Taarifa  za  shambulio  hilo  zilizusha  hasira  na maombolezi duniani  kote, ambapo  viongozi  wa  dunia walituma salamu za rambirambi na kuelezea masikitiko yao. Rais Donald Trump wa Marekani ambaye alilaani tukio hilo aliloliezea kuwa "mauaji ya kutisha", alisifiwa na mshambuliaji katika mwongozo aliouweka mtandaoni kwamba ni "ishara ya utambulisho mpya wa watu weupe na mwenye dhamira ya kweli".

Viongozi wa kisiasa na nchi za Kiislamu barani Asia na Mashariki ya Kati walipaza sauti zao kulaani vikali uhalifu unaowalenga Waislamu.